Sarah Cohen ataka achukue nguo katika makazi yanayotajwa 'eneo la tukio'
Na RICHARD MUNGUTI
MJANE wa bwanyenye Tob Cohen, Sarah Wairimu Kamotho aliyekanusha shtaka la kumuua mumewe miezi mitatu iliyopita, Jumatano ameomba mahakama imruhusu aende katika makazi yao kuchukua nguo zake na bidhaa nyinginezo ikiwa ni pamoja na gari.
Kupitia kwa wakili Philip Murgor, Bi Kamotho aliyeachiliwa kwa dhamana ya Sh4 milioni amesema anahitaji nguo, gari ambalo halitumiki na vifaa vingine kutoka kwa jumba la kifahari lenye thamani ya Sh400 milioni.
“Mshtakiwa anataka kuchukua nguo kutoka kwa makazi yake ya hapo awali alikokuwa akiishi na Cohen aliyeuawa usiku wa Julai 19/20, 2019,” Bw Murgor amemweleza Jaji Stellah Mutuku anayesikiza kesi hiyo.
Sarah ameeleza mahakama kuwa anatumia pesa nyingi kununua nguo na bidhaa nyingine ilhali zimefungiwa katika makazi yake ya kifahari ya Kitisuru.
Mahakama ilipomwachilia kwa dhamana ilimwamuru Sarah asirudi katika makazi hayo bila idhini ya mahakama kwa vile “ni mojawapo ya ushahidi utakaotegemewa na mahakama wakati wa kuamua kesi ya mauaji dhidi ya Sarah.”
Katika afidaviti aliyowasilisha mahakamani, Sarah ameeleza kuwa anahitaji mavazi yake yanayofungiwa katika makazi yao na mumewe marehemu.
Pia amesema anahitaji kuondoa gari moja ambalo halitumiki lililoegeshwa katika makazi hayo mtaani Kitisuru, Kaunti ya Nairobi.
Lakini ombi hilo limepingwa na upande wa mashtaka na wakili anayemwakilisha Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) Donald Kipkorir.
‘Si pahala hivi hivi’
Mahakama imeelezwa kwamba Sarah hawezi kufika mahakamani tu na kueleza anataka aruhusiwe kurudi katika makazi yake ya hapo awali kuchukua vifaa.
“Makazi yake ya zamani ni ushahidi utakaotegemewa katika kesi hii na kamwe hawezi kuruhusiwa kurudi kule vivi hivi,” kiongozi wa mashtaka amemweleza Jaji Mutuku.
Bw Kipkorir ameibua suala iwapo mahakama iko na mamlaka ya kuruhusu ombi la mshtakiwa kabla ya kesi kusikizwa na kuamuliwa.
Mahakama imefahamishwa kuwa maiti ya Cohen ilikutwa imetupwa ndani ya tangi la maji katika makazi hayo.
Jaji Mutuku amemwamuru Sarah awasilishe ombi rasmi ndipo mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) na DCI wawasilishe majibu.
Kesi itatajwa tena Novemba 5, 2019, kwa maagizo zaidi.