Manchester City ndani ya robo-fainali Carabao Cup
Na MASHIRIKA
MANCHESTER, Uingereza
MABINGWA watetezi, Manchester City wamefuzu kwa robo-fainali ya Carabao Cup baada ya kuinyuka Southampton 3-1 ugani Etihad Stadium, Jumanne usiku.
Kilikuwa kichapo cha pili mfululizo kwa Southampton ambayo Ijumaa ilicharazwa 9-0 na Leicester City kwenye mechi ya Ligi Kuu (EPL) iliyochezewa uwanjani St Marys.
Southmapton chini ya kocha Ralph Hasenhuttl walionekana kucheza vizuri kabla ya kuanza kuchanganyikiwa ambapo walifungwa bao la kwanza dakika ya 20 kupitia kwa beki Nicolas Otamendi kufuatia kona ya Bernard Silva.
Sergio Aguero aliongeza bao la pili na kufanya mambo kuwa 2-0 kabla ya wakati wa mapumziko, likiwa bao lake la 11 msimu huu.
Mshambuliaji huyo wa Argentina aliongeza bao la tatu dakika ya 57, baada ya kuunganisha mpira wa Riyad Mahrez ambao ulimchanganya kipa Alex McCarthy na kupitia katikati ya miguu yake.
Kwa jumla, washindi walichapa makombora 19 yaliyolenga lango la wapinzani ambao hawakufanya shambulio lolote la kujivunia.
Washangilia hadi kipenga cha mwisho
Licha ya kushindwa, mashabiki wa Souhtmapton waliishangilia timu yao hadi dakika ya mwisho kwenye mechi hiyo ambayo walijipatia bao la kuvutia machozi kupitia kwa Jack Stephens lililotokana na kona ya James Ward-Prowse. City, watajua wapinzani wao leo baada ya mechi za jana usiku.
Licha ya mwenendo mzuri wa City, kocha wao Pep Guardiola amedai kwamba kuumia kwa nyota wake kadhaa kunampa wasiwasi kwamba huenda hali hiyo ikagharimu kikosi chake msimu huu.
Matokeo mengine ya mechi za Carabao yalikuwa: Oxford United (1) 4 Sunderland 1 (2), Burton 1 Leicester City 3, Everton 2 Watford 0, Manchester City 3 Southmapton 1, Crawley Town 1 Colchester 3.