Habari njema kugundulika kwa kobe adimu Lewa
Na MAGDALENE WANJA
KOBE aina ya pancake tortoise walio katika hatari kubwa ya kutoweka, wamegunduliwa katika hifadhi ya wanyamapori ya Lewa ambayo iko katika kaunti mbili za Meru na Laikipia.
Kugunduliwa kwa kobe hao saba wanaojulikana kumeashiria kuenea kwa sehemu chache wanakopatikana viumbe hao humu nchini.
Ufumbuzi huo unajiri takribani miezi miwili tu baada ya Kenya kufaulu katika pendekezo lake la kutaka kobe hao kuwekwa katika kitengo cha Appendix I, katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu Viumbe walio katika Hatari ya Kuangamia (CITES), ili kuwachunga dhidi ya biashara haramu.
Hapo hawali, iliaminika kuwa aina hiyo ya kobe wanapatikana tu katika maeneo ya Marsabit na Kusini mwa Kaunti ya Kitui.
Kulingana na taarifa kutoka kwa mbuga hiyo, kobe hao waligunduliwa katika sehemu nne kati ya 14 ambazo zilikuwa na uwezekano wa kuwa na wanyama hao.
“Ufumbuzi huu ndiyo wa kwanza kuwa katika sehemu ya juu (altitude) ambapo kobe hao wanaweza kuishi nchini Kenya.
Msimamizi wa hifadhi hiyo Bw Geofrey Chege alisema kuwa kuna haja ya utafiti wa dharura ili kubainisha mazingira bora zaidi ya aina hii ya kobe kwa lengo la kuwahifadhi.
“Hata ingawa ugunduzi huu una maana sana kwa hifadh hii, kuna umuhimu wa kufanya utafiti zaidi ili kuona jinsi wanavyoweza kuishi vyema,” akasema Bw Chege katika taarifa.
Changamoto
Baadhi ya changamoto ambazo zimechangia katika kupungua kwa aina hiyo ya kobe ni pamoja na uharibifu wa mazingira yao ambayo ni sehemu za misitu na mawe.
Nchi zingine ambapo kobe hao wanapatikana barani Afrika ni pamoja na Tanzania na Zambia.
Kutokana na kuwekwa kwa kobe hao katika kitengo cha Appendix I, biashara za kimataifa za kobe hao zimepigwa marufuku isipokuwa tu katika hali na mazingira yanayohusu utafiti kuhusu viumbe hao.