UEFA YAREJEA: Borussia Dortmund yakaribisha Inter Milan
Na MASHIRIKA
PARIS, UFARANSA
NYOTA Jadon Sancho atarejea leo Jumanne katika kikosi cha Borussia Dortmund kitakachochuana na Inter Milan katika kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) uwanjani Signal Iduna Park, Ujerumani.
Dortmund watashuka dimbani wakijivunia huduma za wachezaji wote wa haiba kuba isipokuwa kipa Roman Burki na kiungo Marco Reus waliopata majeraha wakati wakisakata mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) dhidi ya VfL Wolfsburg wikendi iliyopita.
Chini ya kocha Lucien Favre, Dortmund watakuwa na ulazima wa kusajili ushindi katika mechi ya leo hasa ikizingatiwa kwamba walipoteza mchuano wa mkondo wa uliowakutanisha jijini Milan mwezi uliopita.
Kufikia sasa, Dortmund na Inter wanajivunia alama nne kila mmoja na wanashikilia nafasi ya pili katika Kundi F nyuma ya Barcelona ambao wamejizolea jumla ya alama saba kutokana na mechi tatu zilizopita.
Huku Barcelona wakipigiwa upatu wa kutamalaki kilele cha Kundi F, mshindi katika mchuano wa leo kati ya Dortmund na Inter atakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufuzu kwa hatua ya 16-bora.
Sancho anarejea kikosini baada ya kupumzishwa wikendi iliyopita katika mchuano wa Bundesliga uliowashuhudia waajiri wake wakivuna ushindi wa 3-0 uliotamatisha rekodi nzuri ya kutoshindwa kwa Wolfsburg.
Matokeo hayo yalichochewa na hamasa iliyowashuhudia Dortmund wakiwazamisha Borussia Monchengladbach 2-1 katika raundi ya pili ya kipute cha DFB Cup mapema wiki jana.
Wakicheza dhidi ya Wolfsburg, Dortmund walitegemea pakubwa huduma za wavamizi Mahmoud Dahoud na Achraf Hakimi katika safu ya mbele. Hata hivyo, walipatwa na pigo la kuyakosa maarifa ya nahodha Reus aliyepata jeraha la mguu katika dakika ya 30.
Ingawa Reus amedokeza uwezekano wa kuunga kikosi cha kwanza cha waajiri wake katika mchuano wa leo Jumanne, kocha Favre amesisitiza kuwa huenda akamweka benchi kwa minajili ya gozi la Klassiker litakalowakutanisha na Bayern Munich mwishoni mwa wiki hii.
Kufikia sasa, Dortmund wanashikilia nafasi ya pili katika msimamo wa jedwali la Bundesliga kwa alama 19, tatu nyuma ya Mochengladbach wanaoselelea kileleni. Zaidi ya Sancho, Dortmund watapigwa jeki zaidi na marejeo ya washambuliaji Julian Brandt, Thorgan Hazard, Mario Gotze na Paco Alcacer.
Wanne hao wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza Dortmund ambacho kitapania leo Jumanne kutia kapuni alama tatu muhimu ili kuwapiku Inter na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kusonga mbele kwa hatua ya mwondoano pamoja na Barcelona ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).
Inter ambao kwa sasa wananolewa na kocha Antonio Conte, walilazimishiwa sare ya 1-1 na Slavia Prague katika mchuano wao wa kwanza kabla ya kupepetwa na Barcelona kisha kuwapokeza Dortmund kichapo cha 2-0.
Kwa upande wao, Dortmund waliwapiga Slavia 2-0 kabla ya kuwalazimishia Barcelona sare tasa katika mchuano uliowakutanisha uwanjani Signal Iduna mnamo Septemba 17.
Kikubwa zaidi kinachowaaminisha vijana wa Conte ni ubora wa fomu inayojivuniwa na kikosi chake kwa sasa katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Inter wanashikilia nafasi ya pili ligini kwa alama 28, moja nyuma ya mabingwa watetezi Juventus baada ya kusajili ushindi mara mbili na kuambulia sare moja katika mechi tatu zilizopita.
Pigo la pekee kwa Inter ni ulazima wa kuyakosa maarifa ya kiungo Danilo D’Ambrosio na mvamizi Alexis Sanchez wanaouguza majeraha. Kukosekana kwao kutampisha Romelu Lukaku ambaye kwa sasa anaongoza jedwali la wafungaji bora katika Serie A kwa mabao tisa.
Liverpool yakaribisha Genk
Katika mechi nyinginezo za leo Jumanne, mabingwa watetezi wa UEFA Liverpool watakuwa wenyeji wa Genk kutoka Ubelgiji.
Liverpool kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili katika Kundi E kwa alama sita, moja nyuma ya Napoli ambao watapepetana na Red Bull Salzburg ya Austria.
Red Bull wanashikilia nafasi ya tatu kundini kwa alama tatu, mbili zaidi kuliko Salzburg wanaokokota nanga mkiani.
Chelsea watakuwa wenyeji wa Ajax Amsterdam ya Uholanzi katika mchuano mwingine unaotarajiwa kuwa wa kusisimua zaidi. Chini ya kocha Frank Lampard, Chelsea watakuwa na ulazima wa kusajili ushindi katika mechi hiyo ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele kwa pamoja na Ajax waliowabandua Real Madrid na Juventus katika kivumbi cha UEFA msimu jana. Miamba wa soka ya Uhispania, Valencia watakuwa wenyeji wa Lille kutoka Ufaransa.