NDIVYO SIVYO: Matumizi sahihi ya vivumishi vya pekee hasa -ote na -o-ote
Na ENOCK NYARIKI
SI mara yangu ya kwanza kupambanua tofauti baina ya vivumishi vya pekee ila wakati huu tutaitazama mizizi miwili ya vivumishi hivyo ilivyojikita katika muktadha maalumu.
Kabla ya kuingia katika kitovu cha mjadala ni muhimu kuvitaja vivumishi vya pekee. Hivi vimejengwa kwenye mizizi mitano ambayo ni -ote, -o-ote, -enye, -enyewe na -ingine.
Upekee wa vivumishi hivi hutokana na mambo mawili.
Kwanza, zaidi ya kutumiwa kama vivumishi maneno yenyewe yanaweza kutumiwa vingine. Pili, huchukua viambishi vya pekee mbavyo vimehimiliwa katika mizizi mitano.
Mzizi -enye huonyesha nomino inayomiliki kitu fulani. Jambo moja ambalo ni muhimu kulitaja hapa ni kuwa mzizi huu haupaswi kufuatwa na kitenzi au vifungu tenzi. Kwa mfano, ni makosa kusema ‘chenye aliniambia’ au ‘mwenye anakuja’. Wakati mwingine, kivumishi hiki kinapofuatwa na vitenzi vinavyoanza kwa “ku” huwa vigumu kulitambua kosa kwa sababu vitenzi hivyo pia huweza kutumiwa kama nomino pale inapohitajika.
Mzizi -enyewe nao hutumiwa pale ambapo mzungumzaji anatilia mkazo nomino fulani. Kwa mfano: Dawa yenyewe ndiyo hii. Katika miktadha mingine, mzizi huu unapotumiwa kama kiwakilishi cha pekee unaweza pia kuibua dhana ya umilikaji. Tazama mifano ifuatayo: Chama hiki kina wenyewe; Kwa nini umempiga mtoto wa wenyewe.
Mzizi -ingine nao huibua dhana mbili muhimu ambazo ni “tofauti na” au “zaidi ya”. Mfano: Niletee kikombe kingine; hiki ni kichafu; Mwanafunzi mwingine mgeni ameingia ofisini kwa mkurugenzi. Mjadala wetu utaizunguka mizizi miwili iliyosalia: -ote na -o-ote. Mzizi –ote hutumiwa sana katika sajili ya matatu. Mara kwa mara, utawasikia wapigadebe au makondakta wakisema: “Steji yote ni shilingi ishirini.” Sina tatizo na matumizi ya “steji” maana ni neno lililotoholewa jinsi yalivyotoholewa maneno mengine mengi. Kwa hivyo “steji” na “stendi” kwangu mamoja. Hata hivyo, Kamusi Elezi ya Kiswahili imetoa maelezo yanayoleta tofauti finyu baina ya maneno hayo mawili. Kwa mujibu wa kamusi yenyewe, steji ni sehemu ya abiria iliyojengwa kwa kuinuliwa ili iwe rahisi kwa abiria kupanda kwenye gari. Sasa turejee kwenye kauli tuliyoitanguliza hapo juu: “Steji yote ni Sh20”.
Dhamira ya wazungumzaji huwa ni kuwataarifu abiria kuwa kila steji au stendi ni Sh20 bila kujali umbali.
Lengo la mzungumzaji liwapo ni kuibua dhana ya “kila” au “bila kubagua au kuchagua’’, mzizi mwafaka kuutumia ni -o-ote. Kwa hivyo, tunapaswa kusema: Steji au stendi yoyote ni shilingi ishirini. Mzizi -ote unapotumiwa katika sentensi huleta dhana ya ujumla wa kitu au vitu.