• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:55 AM
VITUKO: Pengo na Soo wajipata kwenye mtego wa panya kwake Nafoyo

VITUKO: Pengo na Soo wajipata kwenye mtego wa panya kwake Nafoyo

Na SAMUEL SHIUNDU

SINDWELE alizipenda likizo za Desemba kwani zilitanguliwa na mitihani ya kitaifa kisha zikatamatishwa na sherehe za Krismasi.

Siku za mitihani zilitoa fursa ya mapumziko na kumhakikishia uhuru wa kubugia kinywaji chake bila woga wa kubambwa na serikali wala wasiwasi ya kuchelewa kazini.

Nyakati kama hizi za mitihani, vijana wa serikali huwa na kazi muhimu ya kuangalia mitihani. Raha na utulivu ulioje?

Ndiposa akawahakikishia wenzake kuwa hawakupaswa kuhofu lolote pale sebuleni kwa Nafoyo.

Wakatulia na kuendeleza gumzo. Habari za kukamatwa kwa Tumbo zilikuwa zingali kwenye ndimi za wenyeji wa eneo hilo. Habari hizi zilitawala kila mazungumzo mtaani. Kadri habari zenyewe zilivyosambaa ndivyo zilivyorashiwa chumvi na pilipili kulingana na ubunifu wa kila msimuliaji.

“Nasikia alijiendea alipotiwa pingu,” Soo alisimulia.

“Acha kujiendea. Alijaribu kujitetea kuwa mkewe alikuwa kahimili na angejifungua wakati wowote.” Sindwele alichangia kauli.

“Mbona hawakumhurumia jamani?” Pengo alijitia imani bandia.

“Huruma itoke wapi? Nasikia askari alimpongeza kwa kazi nzuri na kumkumbusha kuwa iliyosalia sasa ni kazi ya mkunga,” Sindwele alitoa kauli iliyowakuna wenzake. Wakaangua kicheko. Walicheka hadi wakajisahau. Hawakugundua ishara ilipotolewa.

Hawakujua mwenyeji wao na wateja wengine walivyotoweka. Hawakuwaona askari wawili waliojitoma humo sebuleni na mwingine akafululiza hadi chumbani. Walipozinduka, walikuwa mateka.

Kutorokea mlango wa nyuma

Sindwele aliingia chumbani ili akatorokee kwa mlango wa nyuma lakini humo chumbani akamkuta askari akiukomelea mlango huo wa nyuma. Akajibanza nyuma ya jungu la busaa Lililokuwa mekoni. Pombe iliyomjaa kichwani ilimdanganya kuwa hangeonekana nyuma ya jungu la busaa.

Askari aliyekuwa chumbani aliligonga jungu hilo teke zito. Likapasuka. Likamwaga busaa mekoni na kutapakaza vigae sakafuni kote.

Mpasuko wa jungu, mtapakao wa vigae na sauti ya ‘tssssss!’ kutoka mekoni vilimtia Sindwele kiherehere. Pombe kichwani mwake ikamwambia kuwa risasi zilikuwa zikifyatuliwa humo chumbani. Akachukua tahadhari kabla ya hatari. Akaamua kujisalimisha kabla ya kufikiwa na risasi.

“Msinifyatue tafadhali! Niko hapa! Msiniue! Nina watoto wadogo wanaonitegemea,” Sindwele alipaza sauti.

Pengo na Soo walitamani kumcheka mwenzao lakini wakachelea kwa sababu hali yake na yao ilikuwa kama hali ya gunia na mkeka. Walijua kuwa wangemtania mwenzao kuihusu kauli hii ya kuwa na watoto wadogo waliomtegemea. Wakati huo wangemcheka na kupigishana viganja huku wakiigiza jinsi mwenzao aliyvojitetea. Lakini si wakati huo. Wakati huo walipaswa kuwazia namna ya kujinasua kwenye mtego wa panya walimojipata.

You can share this post!

Pesa ndizo kiini cha kuvunjika kwa ndoa ya Linturi, korti...

Aliyekuwa mhariri wa Taifa Leo kuzikwa Alhamisi

adminleo