• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Miguna aapa kurudi Kenya kupambana na Jubilee

Miguna aapa kurudi Kenya kupambana na Jubilee

VALENTINE OBARA na WANDERI KAMAU

MWANAHARAKATI aliyefurushwa nchini, Miguna Miguna Jumatatu alirudi Canada na kuapa kurejea Kenya karibuni kuendeleza mapambano yake dhidi ya serikali ya Jubilee.

Hii ni mara ya pili kwa Bw Miguna kurudishwa Canada mwaka huu.

Ingawa wakati alipofika uwanjani JKIA, Nairobi Jumatatu iliyopita alidai hakuwa na paspoti yake ya Canada ambako ana uraia, Jumatatu aliwasilisha paspoti hiyo kwa maafisa wa uhamiaji wa Muungano wa Milki za Kiarabu (UAE) mjini Dubai, ambako amekuwa tangu Alhamisi iliyopita.

Alisema alikataa kuiwasilisha kwa maafisa wa Kenya kwa sababu alikuja nchini mnamo Machi 26 “kama raia mzaliwa wa Kenya”.

Wakili huyo ambaye alidai kujeruhiwa na kutiliwa dawa kabla ya kuondolewa JKIA mnamo Jumatano usiku wiki iliyopita, hatimaye aliondoka mjini Dubai na kuwasili Ontario, Canada, ambako alisema anatarajia kupokea matibabu.

“Baada ya kutibiwa ninanuia kurudi Kenya mara moja na kuendeleza mapambano ya kuboresha hali ya taifa ili kulifanya liwe lenye haki ambayo sisi Wakenya tumekuwa tukitamani kwa miaka 55,” akasema kwenye taarifa.

Zaidi ya hayo, aliwakashifu Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet na Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji George Kihalangwa na kuwaambia hawana haki kutoa maagizo kumhusu kwani walipatikana na hatia ya kukiuka maagizo ya mahakama.

“Wahalifu waliohukumiwa hawafai kutoa maagizo kumhusu raia asiye na hatia. Wanashikilia mamlaka ya umma kinyume cha sheria. Wanatumia mamlaka hiyo kwa njia haramu na kufanya nipitie mateso, ukatili na unyama,” akasema.

Alhamisi iliyopita, Jaji George Odunga aliwatoza watatu hao faini ya Sh200,000 kila mmoja kwa kukaidi agizo la mahakama la kufika mbele yake.

Mwanasiasa huyo alirejeshwa kwa lazima mjini Dubai na serikali ikishikilia kwamba alikataa kutia saini fomu za kuomba upya uraia wa Kenya.

Idara ya Uhamiaji inadai kwamba Bw Miguna alipoteza uraia wake 1998 alipopokea uraia wa Canada, kwa hivyo lazima atume maombi upya ili kuwa raia wa Kenya kisheria. Lakini alisisitiza hatajaza stakabadhi hizo, kwani yeye ni mzaliwa wa Kenya.

Bw Miguna amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Jubilee, na masaibu yake yalianza wakati alipojitolea kumwapisha kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kuwa ‘rais wa wananchi’ mnamo Januari 30.

Alikosoa uamuzi wa Bw Odinga kukubali kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta hivi majuzi, akisema hatua hiyo ni usaliti kwa watu ambao walifariki wakati wa maandamano ya NASA kupinga ushindi wa Jubilee kwenye chaguzi za urais za Agosti 8 na Oktoba 26, 2017.

You can share this post!

Wa Muchomba atawataka wanaume kuoa wake wengi

Mafuriko yatarajiwa tena Aprili

adminleo