Habari

Seneti yapitisha pendekezo serikali iruhusiwe kukopa hadi Sh9 trilioni

November 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Seneti limepitisha pendekezo la kuidhinisha marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Serikali Kuu hivyo kuiruhusu kukopa hadi Sh9 trilioni.

Ni hatua itakayoiwezesha kupata fedha kuendesha mahitaji yake mwaka huu 2019.

Maseneta 30 kati ya 47 wamepiga kura kuunga mkono pendekezo la serikali la marekebisho ya sehemu ya 26 (1) (a) ya Sheria kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma, 2015 (PFM Act) ili kutoa idhini na mwanya kwa serikali kukopa zaidi ya asilimia 50 ya jumla ya utajiri wa nchi.

Pendekezo hilo liliwasilishwa na kaimu Waziri wa Fedha Ukur Yatani katika bunge hilo wiki jana.

Kufikia mwezi Juni 2019 mzigo wa madeni ya Kenya ulikuwa Sh5.8 trilioni; kiasi ambacho mashirika ya kifedha ya kimataifa kama vile Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) yalisema ni juu zaidi kwa serikali kuweza kumudu.

Katika ripoti yake ya hivi punde WB inahoji Bajeti ya Kitaifa ya mwaka huu ya kiasi cha Sh3.02 trilioni ikisema serikali haiwezi kutimiza malengo yake, kwani inazongwa na mzigo mzito wa madeni.

“Bajeti inapaswa kuundwa kutokana na mipango mahususi kuhusu makisio sahihi ya mapato na matumizi ya serikali kuhakikisha kuwa deni la serikali liko katika kiwango ambacho inaweza kumudu,” Mwanauchumi mkuu wa WB Peter Chacha alisema katika ripoti hiyo aliyoitoa wiki jana.

Bw Yatani ambaye alichukua usimamizi wa wizara kutoka kwa Waziri wa Fedha aliyesimamishwa kazi Henry Rotich wiki jana alisema ikiwa maseneta hawatakubali ombi lake huenda serikali ikashindwa kufadhili shughuli zake.

Yatani alisema serikali sasa iko tayari kuanza mchakato wa kupanga upya mpango wa ulipaji wa madeni ya serikali.

Hatua ya kwanza, akasema, ni kuachana na mikopo inayotozwa riba ya juu na kuanza kukopa mikopo yenye masharti nafuu na riba za chini.

“Tunataka kutumia pesa hizo za mikopo kulipa madeni ya zamani na yenye riba kiwango cha hadi asilimia 9.5 ambayo inaathiri uchumi wetu,” Bw Yatani akawaambia maseneta.

Maafisa wa serikali wanasema kwa kupata idhini kutoka kwa maseneta, serikali sasa itaweza kupokea mikopo ya kima cha Sh421 bilioni kutoka kwa mashirika ya kifedha ulimwenguni.

Mikataba ya mikopo hiyo ilikuwa imeandaliwa lakini haikuwa imetiwa saini kutokana na kizingiti cha kisheria kinachoizuia serikali kukopa zaidi ya asilimia 50 ya kiwango cha utajiri, yaani Sh6 trilioni.

Mwishoni mwa Oktoba 2019 Waziri wa Fedha Ukur Yatani aliitaka seneti kuunga mkono pendekezo la serikali la kutaka iruhusiwe kuchukua mikopo ya hadi Sh9 trilioni kutoka kiwango cha sasa cha Sh6 trilioni.

Alirai kwa kuhofia huenda pengine shughuli za serikali zikakwama chini ya sheria za sasa ambazo zimekuwa zikiizuia kukopa zaidi ya Sh6 trilioni.

Akiongea alipofika mbele ya kamati ya pamoja ya seneti kuhusu sheria mbadala na Fedha na Bajeti Bw Yatani alisema wakati huu serikali haiwezi kutenga fedha za kufadhili miradi ya maendeleo kwa sababu haiwezi kukopa zaidi.

Bw Yatani alitoa mfano wa Mpango wa Serikali wa Utoaji Huduma za Matibabu kwa Wote (UHC), usambazaji wa stima mashinani na ile ya miundombinu kama baadhi ya miradi ambayo itaathirika kutokana na uhaba wa pesa ikiwa serikali haitaruhusiwa kukopa zaidi.

“Nawaomba enyi maseneta muidhinishe mabadiliko kwa sheria ya usimamizi wa fedha ili tuweze kukopa hadi Sh9 trilioni, walivyofanya wenzenu wa Bunge la Kitaifa wiki jana. Ikiwa mtakataa ombi hili, basi tutatumbukia kwenye shida kubwa kama taifa kwani hatuna njia nyingine ya kupata hela,” akasema alipokuwa akimjibu Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot aliyetaka kujua kile kingefanyika ikiwa seneti ingekataa ombi hilo.

Wakati huo Bw Cheruiyot alionya serikali dhidi ya kuendeleza mtindo wa kuweka mipango ya matumizi ya fedha ilhali haina fedha hizo wala haijui itakakozipata.

“Bw Waziri, huenda tunataka kuwaunga mkono katika utekelezaji wa miradi inayoendelea, lakini mtindo wa kuanza kukopa ili kuanzisha miradi mipya hairuhusiwi,” akaonya Bw Cheruiyot wakati huo.

Katika barua iliyotuma kwa seneti mnamo Oktoba 15, 2019, Wizara ya Fedha iliiomba seneti kukubali kuidhinisha marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Serikali Kuu, kanuni ya 2015, sehemu ya 26 (1) (c).

Waziri alitaka kanuni ya 26 (1) ilifanyiwe mabadiliko kwa kufuta maneno “asilimia 50 ya Jumla ya Utajiri wa Nchini (GDP) katika thamani halisi ya sasa.”

Kiwango cha madeni ya Kenya kilifikia Sh6 trilioni mnamo Agosti 2019 baada ya taifa hili kukopa Sh200 bilioni zaidi ndani ya kipindi cha miezi miwili. Lakini sasa Wizara ya Fedha inataka iruhusiwe kukopa Sh3 trilioni zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa chini ya sheria ya sasa.

Chini ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Serikali ya 2015, inayotumika sasa, serikali inaruhusiwa kukopa hadi asilimia 50 ya GDP pekee. Lakini mapema Oktoba, wabunge wa bunge la kitaifa waliifanyia mageuzi sheria hiyo na kuweka kiwango hicho kuwa Sh9 trilioni kama ilivyopendekezwa na Wizara ya Fedha.