Makala

KILIMO NA BIASHARA MASHINANI: Ni mkulima wa mazao mseto Taveta anayewashauri wakulima wenzake

November 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LUDOVICK MBOGHOLI

JOSEPH Lom Kwiya, 63, ni mkulima wa miaka mingi katika eneo la Ibura lililoko Kisumu Ndogo, kaunti ndogo ya Taveta, gatuzi la Taita Taveta.

Ni mkulima ambaye tayari ameimarisha shughuli za ukulima wa mazao mseto katika wadi ya Mboghoni, na bidii yake ya mchwa imemwezesha kuwa mkufunzi kwa wakulima chipukizi wanaotegemea kilimo kama uti wa mgongo.

“Nilianza ukulima wa mahindi, nduma na ndizi pekee, lakini kadri miaka ilivyokuwa ikisonga, niliamua kuanza ukulima wa mazao mbalimbali kwa lengo la kuboresha ustawi zaidi,” aliambia Akilimali katika mahojiano shambani mwake.

“Nilishawishika kufanya hivi kutokana na ushauri niliopata kutoka kwa wakulima waliokuwa wajuzi na waliobobea kwenye mchanganyiko wa upanzi wa mazao tofauti,” anaelezea.

Anadai mtaji mkubwa aliokuwa nao aliuwekeza kwenye ukulima wa ndizi, lakini alipoona manufaa alijituma kuongeza bidii kuhakikisha anaongeza mazao mengine zaidi.

“Nilitumia mtaji mkubwa kwenye upanzi wa zao la ndizi kabla ya kujishughulisha na ukulima wa mahindi na mboga,” anadokeza.

Hata hivyo, mzee huyo hakukata tamaa alipoarifiwa na wakulima waliomtangulia, kuwa endapo anataka kufaulu zaidi, afanye kilimo mseto kama hatua ya kujiongezea mapato ya kibiashara.

“Nilihisi ushauri huo ulikuwa bora zaidi kwangu, kwani shamba hili ni kubwa lenye upana wa ekari nane na kulilima lote kujitosheleza ni kuanzisha kilimo mseto kwa kuchanganya mazao ya sampuli mbalimbali,” anasema.

Miongoni mwa mazao anayokuza ni pamoja na miembe ambayo haijali misimu ya upanzi wala uvunaji wake.

“Hapa niliwekeza mbegu ya miembe aina spesheli ya sikio punda, ambayo kamwe haihitaji msimu wa ukuzaji na mavuno. Ni mbegu ambayo hukuwa na hata kufikia mavuno mara tatu au nne kwa mwaka,” anaeleza.

Aidha mkulima huyu anasimulia zaidi kuhusu ukuzaji ndizi akisema kuna sampuli za mbegu zinazotoa mikungu pacha ya ndizi.

“Hata niliweka mbegu ya migomba inayotoa mikungu pacha ya ndizi, aina hii ya mbegu huwezi kuipata kwengineko, ni aina ya ndizi inayotoka kwenye jamii ya ‘ndizi mshale’, na niliifumania katika miteremko ya maeneo ya mashambani kando ya mlima Kilimanjaro -Moshi maeneo yanayomilikiwa na jamii ya Wachaga nchini Tanzania” anaeleza.

Hata hivyo, mkulima huyu amekuwa kielelezo kwa wakulima wachanga, ambao idadi kubwa hujifunza kilimo kutoka kwake.

“Vijana wengi hujitosheleza kimafunzo kutoka kwangu. Sijisifii kuwa bora miongoni mwa wakulima bora, ila mafanikio ya juhudi zangu kwenye ukulima ndiyo yanayowavutia wakulima vijana,”

“Vijana wanaonijia hutoka maeneo ya Kiwalwa, Mrabani, Kimala na hata wachache hutoka Chala na Njukini. Huwa wanaelekezwa na wanaonifahamu na wakija wanatoka na mbegu za mazao wanayohitaji,” anasema.

Mbali na shughuli zote hizo za ukulima, Mzee Joseph pia anajishughulisha na uvuvi kwenye mito iliyoko karibu na shambani kwake.

“Siangalii tu kilimo mseto cha mazao na matunda, bali pia najishughulisha na uvuvi,” anaeleza.

“Hapa Ibura Kisumu Ndogo kuna mito mingi midogo midogo iliyojaa samaki wa kila sampuli. Kuna perege, dagaa na hata kambale,” anasema.

Anaongeza, “Si vizuri ikiwa naendeleza shughuli ya ukulima mahali hapa penye mito yenye samaki, halafu baada ya kazi za siku nirejee nyumbani bila kitoweo.”

Uvuvi

Anaeleza kuwa yeye huvua samaki mara mbili kwa wiki na kupelekea familia yake.

“Unaweza kuvua perege mkubwa wa nusu kilo, au kambale mwenye uzito wa takriban kilo moja na zaidi, na vuno hilo ni kubwa” aambia Akilimali.

Mkulima huyu anasema ingawa amekuwa akiwapa ushauri baadhi ya wakulima wanaomjia yeye pia anahitaji kushauriwa.

“Wakulima wenzangu wamekuwa wakija hapa wakitaka ushauri, lakini ninapowashauri nami pia hutaka ushauri wao mahala nahisi nimekwama” anaelezea .

“Mimi hujiendeleza zaidi ninapopata ushauri kutoka kwa wenzangu, maafisa wa kilimo huwa hawafiki hapa kuniongoza, badala yake najiongoza mwenyewe kutokana na ushauri wa wenzangu,” anaongeza.