RIZIKI: Upishi unamsukumia gurudumu la maisha
Na SAMMY WAWERU
RATIBA ya Caroline Wanjiku, kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi ni yenye shughuli tele kuhudumia Wakenya, kwa njia ya kuzima makali ya njaa.
Ofisi yake ni mkahawa ulioko Zimmerman, Kaunti ya Nairobi.
“Hii ndiyo ofisi yangu, ndiyo hukimu mahitaji ya familia yangu pamoja na kunisomeshea watoto,” Wanjiku ambaye ni mama wa watoto wawili akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano.
Msimu wa likizo, wanawe humfaa kwa kumsaidia kufanikisha shughuli mbalimbali.
“Kifungua mimba, nimemsomesha kupitia hii kazi na mwaka huu (2019) alifanya mtihani wa kitaifa darasa la nane, KCPE na nimejiandaa kwa shule yoyote ile atakayopokea mwaliko,” akasema, akidokeza kuwa anapania kujiunga na Shule ya Upili ya Wasichana ya Loreto.
Alifungua hoteli hiyo ipatayo miaka 10 iliyopita, baada ya kukosa kazi asilani ya taaluma aliyosomea katika taasisi ya juu ya elimu.
Hata hivyo, hajutii kamwe kwa uamuzi aliofanya kuamua kufanya biashara ya chakula.
“Nilihangaika kuzuru ofisi moja hadi nyingine nikitafuta ajira. Mawazo yangu sasa yametulia baada ya kuanzisha biashara ya upishi,” anasema Caroline.
Anafafanua kwamba ilimgharimu mtaji wa Sh25, 000 pekee kuanzisha biashara hiyo ambayo imenoga.
Hupika chakula asilia kama vile mukimo (mchanganyiko wa mahindi, maharagwe, viazi na majani ya maboga, vyote vikapondwapondwa), kande pia pure maarufu kama githeri. Githeri ni mchanganyiko wa mahindi na maharagwe au punje za kunde, nafaka hizo zinachemshwa hadi kuiva.
Vilevile, mama huyo huandaa chapati, ambazo husafu kwa maharagwe au njahi. Caroline pia hupika mchele mweupe na wali, anaousafu kwa maharagwe au njahi.
Bei yake ni nafuu, kati ya Sh40 hadi Sh70.
“Ninalenga wapangaji na wanaofanya shughuli za ujenzi. Pia, kuna waseja wasiopata muda wa mapishi, wote huwahudumia,” anaeleza.
Hakuna kazi isiyokosa changamoto, Caroline anasema mfumuko wa bei za bidhaa hususan nafaka wakati mwingine humuweka katika njiapanda kutathmini upya bei ya mlo.
Hilo hasa linatokana na kupanda kwa gharama ya maisha na uchumi ambao unazidi kuwa ghali. “Awali, chakula ninachoandaa hakikuzidi Sh60. Kufuatia mfumuko wa bei ya nafaka, nililazimika kuongeza Sh10 zaidi kwa mlo ulioathirika. Mahitaji ya wateja yanapaswa kuangalia, ili niendelee kuwahifadhi,” afafanua.
Mwaka huu, wafanyabiashara wengi wakiwamo wenye kampuni, wamefunga kazi na kuchuja wafanyakazi kwa kile kinatajwa kama kudidimia kwa kiwango cha uchumi.
Dennis Muchiri, mchanganuzi wa masuala ya biashara na uchumi anasema hilo linachangiwa na mazingira tata ya biashara, akionya iwapo serikali haitatathmini kanuni zake, huenda mambo yakazidi unga. “Ushuru ghali haukuzi uchumi, badala yake unauzorotesha. Ni hatari katika mazingira ya biashara,” atahadharisha Bw Muchiri.
Mambo yalianza kuenda mrama 2018, serikali ilipoanza kutoza mafuta ushuru, VAT, asilimia nane.
Caroline Wanjiku anasema licha ya hilo amejikakamua kuhakikisha wateja wanapata huduma na bidhaa zake kwa bei nafuu. “Ninalenga faida kidogo, ambayo itanisitiri katika biashara kwa muda mrefu. Mikahawa ni mingi na ina ushindani mkuu,” asema.
Ameajiri msichana mmoja, na anasema hivi karibuni anapania kupanua hoteli hiyo kwa sababu ya ongezeko la wateja.