• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Ahamia kwao kuhepa mke msumbufu

Ahamia kwao kuhepa mke msumbufu

Na TOBBIE WEKESA

SANGO, BUNGOMA

MLOFA mlevi aliyechoshwa na visirani vya mkewe, aliamua kuhamia kwa nyumba ya mamake, akilalamika kwamba mke anamuonyesha dharau mbele ya wageni.

Kulingana na mdokezi wetu, jamaa alikuwa ametembelewa na mashemeji siku mkewe alizua kisanga.

Inasemekana mke alisimama mbele ya wageni na kumuamrisha kufyata mdomo wake asizungumzie wageni hao.

“Wewe unafaa kuzungumza tu mbele ya walevi wenzako. Hapa utaharibu mambo. Keti chini haraka,” mke alimkaripia.

Penyenye zasema baada ya wageni kuondoka, jamaa alianza kuhamisha kila kitu kilichokuwa chake hadi kwa nyumba ya mamake mzazi.

“Uliona sifai kusimama wala kuzungumza mbele ya ndugu zako. Hatutakaa wanaume wawili kwa nyumba moja,” mlofa alimuambia mkewe.

Mwanadada alibaki kushangaa asijue la kufanya.

“Hata mimi nina mama yangu na ako na nyumba kubwa sana. Narudi kwake. Kaa hapo na ukitaka kuwaita ndugu zako basi waite uishi nao,” polo alimfokea mke huku akienda zake.

Duru zinasema kuwa, mwanadada alijaribu kumshawishi mume asiondoke lakini wapi!

“Umezoea kunikosea heshima. Haya madharau yako yalianza pindi tu nilipopeleka mahari kwenu. Ningejua, walahi singepeleka hata ng’ombe mmoja kwenu,” kaka alijutia.

Mdokezi anatuarifu kuwa, kalameni alifululiza moja kwa moja hadi kwa boma la mamake.

“Kwangu sikanyagi tena. Huyo mwanamke akichoka kuishi hapo arudi kwao akae na ndugu zake. Madharau yake yamezidi,” alimueleza mamake.

Mama mzazi alibaki kinywa wazi asijue jinsi ya kumsaidia kijana wake.

Yasemekana baada ya siku tatu mkewe alienda kumrai mama mkwe amshawishi jamaa arudi nyumbani, akiapa kutomdharau tena.

You can share this post!

MBURU: Viongozi watakao wakazi wazaane wamejaa ubinafsi

Trump kupatanisha Misri, Ethiopia kuhusu mto Nile

adminleo