• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 2:55 PM
MWITHIGA WA NGUGI: Itabidi tuache upumbavu wa kupofushwa na wanasiasa

MWITHIGA WA NGUGI: Itabidi tuache upumbavu wa kupofushwa na wanasiasa

Na MWITHIGA WA NGUGI

AMA kweli Kenya imekuwa na kilio kingi kama ‘Shamba la Wanyama’, kuanzia kilio cha umaskini, hali ngumu ya maisha, udanganyifu katika mitihani na hata wizi wa kura, huku matokeo yakiwa ni kuupata uongozi mbaya na watumishi wa umma wasiofaa.

Kila baada ya miaka mitano kwa hakika huwa tuna bahati kama ya mtende na hasa ya kuwachagua viongozi wetu katika ngazi mbalimbali.

Hata hivyo, kama wapigakura waliolaaniwa na mababu zao mara nyingi sisi huangalia mifuko na fedha za wanasiasa na badala ya kuwachagua viongozi wenye nia na maono ya kuyaboresha maisha yetu, tunaishia kuyachagua majitu yenye matumbo yasiyoshiba yasiyokijali kizazi cha kesho na yenye uchu wa ufisadi na ubadhirifu.

Majuma kadhaa yaliyopita tumeshuhudia wanasiasa wazito na wenye majina makuu wakirandaranda na kutikisa ‘kijiji’ cha Kibra huku wakisaka kura za walalahoi wa mtaa huu, haja yao kuu ikiwa ni kupata kiti cha ubunge cha kibra.

Taswira inayojitokeza wazi ni kuwa, Wakenya wangali bado wanaiabudu miungu midogo kwa jina la wanasiasa, ambao kila siku wanawakilisha tabaka la ‘Tumbo Lisiloshiba’, na badala ya kumchagua kiongozi kwa mtazamo wa maadili na uwezo wake, kinachotawala kwa mapana ni siasa za pesa nane na ununuzi wa kura kwa wananchi wenye njaa.

Hata hivyo, sisi kama wazalendo kila siku tutazidi kutumia kalamu zetu, kuandika yalo mema kwa taifa letu. Hatutaruhusu ukabila, ufisadi na upumbavu wa kisiasa kutunyima nafasi ya kulijenga taifa letu.

Umaskini wetu wa muda haufai kutugeuza mazuzu wa kuwasujudu wanasiasa na propaganda zao, huku taifa likiendelea kuzama kwenye bahari kuu la madeni na ufisadi.

Wakati wa kufikiria upya kuhusu hatima ya kizazi cha kesho umetimia, na hili ni jambo ambalo linambidi kila mja kuliwazia, kwa miaka mingi Wakenya wengi wamekuwa na falsafa kuwa wahitajipo kiongozi lazima awe ni mwenye pesa, mali na jina tajika kutoka kwa familia ‘teule’, jambo ambalo limetufeli kwa miaka na dahari.

Kiongozi si lazima awe tajiri na ndiposa sote tumezaliwa tukiwa na talanta mbalimbali.

Mbona basi tutawaliwe na kasumba ya hongo wakati wa uchaguzi?

Msingi wa kujenga nchi unahitaji ari na bidii ya kila mja pasipo kuangalia mlo unaotokana na jitihada za mtenda kazi.

Kwa uhakika, ninatamani siku ile ambapo Wakenya tutajikomboa kutoka kwenye silisili hatari za utumwa ya ukabila na hatimaye tuweze kuiga mfano faafu wa nchi yetu jirani ya Tanzania na tujifunze kuwa Wakenya badala ya kushabikia ukabila.

Tusisahau, kila siku tunalia shida na umaskini lakini haya yote tunajitakia wenyewe.

 

[email protected]

You can share this post!

MUTUA: Demokrasia iko hatarini eneo la Afrika Mashariki

FUNGUKA: ‘Hutaamini ninavyohifadhi kumbukumbu ya...

adminleo