• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
CHOCHEO: Kuepuka dhiki baada ya talaka

CHOCHEO: Kuepuka dhiki baada ya talaka

Na BENSON MATHEKA

KESI yake ya talaka ilipokuwa ikiendelea, Joyce hakuwazia jinsi maisha yangekuwa baada ya ombi lake kukubaliwa.

Alichotaka wakati huo ilikuwa ni kuachana na mumewe na kumsahau kabisa. Hata hivyo, miaka saba baada ya kupata talaka, angali anamkumbuka.

“Maisha yangu hayajakuwa ya kawaida. Nimekuwa nikichanganyikiwa. Ingawa sikuwa na budi kuomba talaka, haijakuwa rahisi kwangu kukumbatia maisha mapya bila ndoa,” asema.

Wataalamu wanasema kuomba talaka, kupata talaka na maisha baada ya talaka ni mambo tofauti.

“Ndoa yako inapoisha, huwa sio rahisi kuzoea maisha ya kuishi peke yako. Lakini watu wanafaa kuelewa kuwa kuna maisha baada ya talaka na matumaini ya maisha ya furaha kama mwanamke singo tena,” asema mwanasaikolojia Debra Simba wa shirika la Maisha Mema jijini Nairobi.

Badala ya kusononeka baada ya talaka, mtu anafaa kushughulika kujenga upya maisha yake. Wataalamu wanasema kwa watu wengi huwa inawachukua miaka miwili kukubali maisha yao mapya baada ya talaka.

“Kuna wanaokubali hali yao haraka na kusonga mbele na maisha bila kusononeka na kuna wanaochukua muda mrefu. Hata hivyo, kwa wastani, mtu anafaa kukubali hali yake baada ya miaka miwili,” aeleza.

Debra asema badala ya kusononeka, mtu anaweza kushughulika na masuala ya kumletea mabadiliko kama vile kujiongezea masomo, kujiunga na vikundi vya watu waliopitia hali sawa awali na hata kusaka marafiki wapya.

Katika makala aliyochapisha mtandaoni, mwanasaikolojia Jenifer Freed anasema kuanza uhusiano mpya wa mapenzi punde tu baada ya talaka kuna hatari zake ikiwa ni pamoja na kuangukia mikononi kwa watu wanaotumia hali yako kukuongezea masononeko.

“Hii ni kwa sababu huwa kuna pengo katika maisha ya aliyepata talaka. Mtu anafaa kujipa muda wa kuomboleza, kujirudia na kujipanga ili asijipate katika uhusiano mbaya zaidi kuliko wa awali,” asema Dkt Freed.

Wataalamu wanakubaliana kuwa marafiki wa dhati huwa wanasaidia mtu kukubali hali yake anapopata talaka.

“Kuwa karibu na marafiki wa dhati kunakusaidia kuepuka kuchukua hatua inayoweza kukuletea majuto kama vile kuzama katika ulevi wa kupindukia, kuwasiliana na mchumba wako wa zamani, kumtumia jumbe za kuudhi au kunyanyasa mpenzi wake mpya,” asema Freed.

Yaumiza

Kwa vile talaka huwa inaumiza mtu hasa ikiwa hakuitarajia, wataalamu wanasema mtu wanafaa kuepuka ushawishi wa kuchukua hatua zinazoweza kuwatumbukiza katika shida.

“Hakikisha kila hatua unayochukua inakupa amani na furaha zaidi badala ya majuto,” aeleza Debra. Hii, anaeleza, inawezekana kwa kutafuta ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu.

“Marafiki wanaweza kukufaa kwa kukutuliza, lakini wataalamu wakiwemo wa masuala ya kiroho watakujenga zaidi na kukupa ushauri upate mwelekeo,” aeleza Debra.

Mtaalamu huyu anasema watu wanafaa kuelewa kuwa talaka ni utaratibu unaoendelea hata baada ya wanandoa kutengana mahakamani na mtu anafaa kujivumbua upya na kutafuta marafiki wasiomkumbusha ndoa iliyovunjika.

“Epuka kujadili mara nyingi uliyopitia mikononi mwa mchumba wako wa zamani na utumie muda huo kutia bidii kuimarisha maisha yako,” aeleza.

Japo wataalamu wanasema sio makosa kuanza uhusiano mpya wa kimapenzi, mtu hafai kuwa na haraka kuanza kufanya mapenzi.

“Utafiti umeonyesha kuwa watu wanaoanza uhusiano wa mapenzi na kula uroda punde tu baada ya talaka hujuta. Chukua muda kabla ya kupatia mtu mwingine moyo na mwili wako,” aeleza Debra.

Anasema baadhi ya watu hupenda kuwatumia wale wanaopata talaka wakiamini wanahitaji kutimiziwa haja zao za kimwili na mahitaji mengine huku wakiwadaganya watawasaidia kuepuka masononeko.

You can share this post!

Korti yatoa agizo TSC iendelee kushirikiana na Knut

Wasomaji wa Kiswahili wapenzi wa Taifa Leo wakongamana...

adminleo