Kenya yahifadhi taji mbio za AIMS
Na GEOFFREY ANENE
KENYA ilihifadhi taji la kinadada la Chama cha Mbio za kimataifa za kilomita 42 na ndefu (AIMS) baada ya Ruth Chepng’etich kutawazwa mshindi Ijumaa usiku jijini Athens nchini Ugiriki.
Chepng’etich alipata tuzo hiyo kutokana na mafanikio yake katika kipindi cha miezi 12 iliyopita. Katika kipindi hicho, Chepng’etich alizoa mataji ya mbio za Istanbul Marathon, Dubai Marathon, Istanbul Half Marathon, Seiryu Half Marathon na Bogota Half Marathon pamoja na kushinda marathon kwenye Riadha za Dunia jijini Doha nchini Qatar mnamo Septemba 27.
“Ni heshima kubwa kupokea tuzo hii, hasa katika mji huu ambao marathon ilizaliwa,” alisema Chepng’etich, Ijumaa.
Kinadada wengine kutoka Kenya waliowahi kubeba tuzo hii ya kifahari ni Tegla Loroupe mwaka 1995, 1997, 1998 na 1999, Catherine Ndereba (2001), Mary Keitany (2009, 2011 na 2017), Edna Kiplagat (2013), Florence Kiplagat (2014), Jemima Sumgong (2016) na Gladys Cherono (2018).
Kabla ya kupoteza taji la wanaume kwa Muethiopia Lelisa Desisa MWAKA 2019, Wakenya walikuwa wametwaa tuzo ya AIMS ya wanaume kupitia Benson Masya (1992), Paul Tergat (1996 na 2003), Josephat Kiprono (2001), Samuel Wanjiru (2008), Patrick Makau (2010), Geoffrey Mutai (2011 na 2012), Wilson Kipsang (2013), Dennis Kimetto (2014) na Eliud Kipchoge (2015, 2016, 2017 na 2018).