Habari

Kalonzo aelekea kwa Ruto?

November 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

HUENDA kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akabuni muungano wa kisiasa na Naibu Rais William Ruto, hii ikiwa ni baada ya kuibuka migawanyiko mikubwa wakati wa uchaguzi mdogo wa Kibra katika mirengo ya Nasa na Jubilee.

Tangazo la ODM kwamba itakatiza uhusiano kati yake na vyama tanzu ndani ya muungano huo, na hatua ya magavana watatu wa kaunti za Ukambani kuunga mkono mgombea wa chama hicho katika uchaguzi huo, zimetajwa kama sababu zilizomsukuma Kalonzo kukumbatia ushauri wa kusaka mshirika mpya.

Magavana hao ni; Alfred Mutua (Machakos), Charity Ngilu (Kitui) na Profesa Kivutha Kibwana (Makueni) ambao walimfanyia kampeni Benard Imran Okoth, aliyeibuka mshindi.

Duru ziliambia ‘Taifa Jumapili’ kwamba, hata kabla ya uchaguzi wa Kibra ufanyike wiki jana, Dkt Ruto amekuwa akimrushia chambo Bw Kalonzo kwa kuwatuma wandani wake kama sehemu ya maandalizi kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Hii ni baada ya kambi yake kung’amua kuwa haitapa uungwaji mkono wa dhati kutoka ngome ya Rais Uhuru Kenyatta ya Mlima K nya baada ya hesabu za siasa za eneo hilo kuvurugwa na handisheki.

Na japo Bw Musyoka alitangaza kuwa chama chake kinaunga mkono mgombeaji wa Ford Kenya katika uchaguzi huo Hamisi Butichi, hakufika Kibra kumpigia debe mgombeaji huo.

Lakini Mbunge wa Embakasi Kusini Julius Mawathe na aliyekuwa Mbunge wa Kathiani Wavinya Ndeti walimpigia debe mgombea wa Jubilee McDonald Mariga wakidai kufanya hivyo kwa ‘idhini’ ya kiongozi huyo wa Wiper.

“Ndio, tunazungumza na Wiper. Na tumepiga hatua kubwa zaidi kufikia sasa,” akasema mbunge mmoja kutoka Rift Valley ambaye aliomba tulibane jina lake.

Madharau

Mbunge wa Kathiani, Bw Robert Mbui alisuta ODM kwa kuendeleza kampeni za kila mara za kudunisha washirika wake ndani ya Nasa, akisema hiyo ni ishara kuwa hakitaki kudumisha uhusiano wao.

“Hatuwezi kuendelea kufanyakazi na watu kama hawa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022; sharti tutafute marafiki wengine ambao watatuheshimu,” akasema mbunge huyo ambaye ni naibu kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa.

Naye Mbunge wa Kitui ya Kati, Makali Mulu alisema Wiper inatafuta mshirika mwenye heshima na watakayemtegemea katika siku zijazo.

“Wenzetu wa ODM walisema hawako tayari kushirikiana nasi. Basi nasi tunatafuta washirika wapya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022. Tunafanya mazungumzo kutimiza lengo hilo,” akasema.