Makala

MAPITIO YA TUNGO: Wasifu wa Tama; Novela aali iliyosheheni mafunzo kemkem kuhusu uadilifu

November 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Mwandishi: Peter Juma

Mchapishaji: Mwasio Publishers

Mhakiki: Wanderi Kamau

Kitabu: Novela

Jina la Utungo: Wasifu wa Tama

Kurasa: 63

MSINGI wa kimaadili huwa nguzo muhimu ambayo humwezesha mwanadamu yeyote kukabiliana na mawimbi ambayo huandama maisha yake.

Ndio ujumbe mkuu anaowasilisha mwandishi Peter Juma, kwenye novela ‘Wasifu wa Tama.’

Ni hadithi inayomrejelea msichana Tama, mwanawe, Mzee Wanga na mkewe, Bi Wanga. Familia hii inasawiriwa kama ya uwezo wa kadri, lakini inayotilia maanani suala la maadili.

Kinyume na wazee wengine wenye miegemeo wa kihafidhina, Mzee Wanga ni mwenye mtazamo huria, kwani ana kisomo cha haja.

Vile vile, anaibukia kuwa mpenda masomo, hivyo akimsisitizia mwanawe Tama (na wengine) kuhusu umuhimu wa kuzingatia yote mawili; masomo na maadili. Kuu linaloibuka ni kwamba, masikio na akili ya Tama ni kama sumaku.

Anazingatia mashauri ya wazaziwe kwa umakinifu mkubwa, hali inayomwezesha kupita vizuri masomo ya shule ya msingi, ambapo anajiunga na Shule ya Upili ya Tumaini. Akiwa katika shule ya msingi, Tama anaibukia kuwa msichana mwadilifu kimienendo, kiasi cha ‘kuogopwa’ na wavulana.

Alipewa majina mengi ya misimbo mingi, moja likiwa ‘mwanafalsafa.’ Hata hivyo, kinaya kikuu kinaibuka katika shule ya upili, kwani kinyume na alivyodhani, maisha ya hapo yanageuka kuwa ya wanafunzi waliopotoka. Hawana maadili hata kidogo, ila ni watumwa wa anasa. Msimamo wake thabiti unamletea shida, kwani anabughudhiwa na wasichana wenzake ‘waliostaarabika.’

Licha ya hayo, anajitia moyo na kuanza harakati za kuleta mageuzi ya kimaadili katia shule hiyo, iliyokuwa na sifa mbaya sana. Hatua yake ya kwanza inakuwa kujiunga na kundi la dini. Analeta mwamko mpya.

Juhudi zake zinamzalia sifa kochokocho kutoka kwa wanafunzi na walimu. Hata hivyo, hapendeki na wote, kwani baadhi ya wanafunzi wanamsingizia kuwa mwizi.

Juhudi hizo zinaumbuliwa, inapobainika kwamba alikuwa amesingiziwa. Juhudi zake hatimaye zinaigeuza kabisa sura na sifa ya shule hiyo. Tama anaendeleza juhudi zake, anapojiunga na Chuo Kikuu cha Hazina.

Kama ilivyokuwa katika shule ya upili, mazingira ya chuo ni yale yale—utovu wa maadili usiomithilika.

Anajitia kibwebwe ambapo anaungana na Kijana Jabali, wanaoamua kuendeleza harakati za uhamasisho wa kimaadili, hasa matumizi ya mihadarati.

Hilo pia haliwi rahisi, kwani kwa wakati mmoja, anatekwa nyara na watu watatu waliokuwa wa genge la ulanguzi wa dawa za kulevya. Upeo unakuwa pale anapookolewa na polisi. Anafanikiwa kwa kusomea udaktari nje na kuwa nguzo kuu ya mageuz katika nchi yake.

Mbinu kuu inayojitokeza ni matumizi ya nahau na usimulizi wa moja kwa moja. Ni novela muhimu kwa kila mmoja katika jamii.

 

[email protected]