VITUKO: Soo aridhia wadhifa mpya wa kusimamia mtihani wa KCSE
Na SAMUEL SHIUNDU
WAJUAO husema kuwa cha mwenzako kikinyolewa, chako unatia maji.
Mkuu mpya wa Elimu katika wilaya ya Sidindi aliujua msemo huu na kuuthibiti barabara. Hakutaka kufikwa na yaliyomfika mtangulizi wake.
Mkuu huyu hakuwa mgeni Yerusalemu kwani alifahamu fika masaibu ya bwana Tumbo yaliyosimuliwa hapo Sidindi. Pamoja na azma hiyo ya kutahadhari kabla ya hatari, alikuwa binti mbichi aliyedhamiria kudhihirisha kuwa mabinti kama yeye walikuwa na uwezo wa kuchapa kazi vyema kuliko wanaume kama Tumbo.
Alipokabidhiwa ukuu wa elimu, aliwahangaisha wote waliolegea kwenye shughuli za kusimamia mithani. Alizuru shule za wilaya hiyo bila taarifa kwa nia ya kuwafumania waliotepetea kazini. Aliwakaripia waliotenda sivyo, baadhi waliandikiwa barua za kuwaonya na wengine wakafurushwa papo hapo. Miongoni mwa waliofurushwa ni msimamizi wa mitihani katika shule ya upili ya Bushiangala.
Huyu alitimuliwa kwa kuanzisha mtihani kabla ya wakati uliofaa. Aligonga kengele mapema. Mwenyewe alipoulizwa kisa na maana akasema kuwa kengele ilimponyoka na kuanguka. Ilipoanguka ilitoa mlio na hapo wanafunzi wakaanza mtihani.
“Sikukusudia kuiliza. Ililia kiajali,” alijitetea.
Mkuu wa elimu hakumsikiliza. Alibwata maneno mengi yasiyochapishika. Hatimaye akamtaka aondoke na asirejee tena hapo shuleni. Msimamizi akaufyata na kuchanga miguu. Aliondoka kwa furaha ya kuondokewa na nakama hiyo ya kusimamia mitihani.
Ni baada ya kufurushwa kwa msimamizi huyu, ndipo Soo alipopokea simu kuwa alihitajika kuutwaa usukani wa kusimamia mitihani. ‘Unahitajika katika shule ya upili ya Bushiangala kusimamia mitihani. utalipwa kuanzia siku ya kwanza’ ndivyo ujumbe kutoka makao makuu ya elimu wilayani ulivyoahidi. Aliposhauriana na wenzake, walimhimiza.
“Utajikusanyia vijipeni vya Krismasi,” Sindwele alimuusia.
“Isitoshe, hutaandamwa na kisirani cha kukutika malevini na kutishiwa kutiwa nguvuni kama ilivyotukia wiki iliyopita!” Pengo alishereheshea.
Soo alikumbuka jinsi walivyobambwa na askari nyumbani kwa Nafoyo wiki iliyopita. Alikumbuka jinsi Sindwele alivyojaribu kujificha nyuma ya jungu la waragi. Akakumbuka jinsi askari mmoja alivyolipasua jungu hilo na kiherehere kilichomkumba Sindwele hadi akaomba asifyatuliwe risasi. Alikumbuka jinsi yeye pamoja na Pengo walivyolazimishiwa mitungi ya chang’aa na misokoto ya bangi. Akakumbuka walivyolazimika kuzunguka mbuyu ili kujinasua kutoka kwa mtego huo. Akaafikiana na Pengo kuwa kama angekuwa kwenye mitihani Jumatano hiyo, labda nakama ya wiki iliyopita haingemkuta. Akaridhia wito wa baraza la mitihani.
“Kesho asubuhi nitafika shuleni Bushiangala kuyatwaa majukumu hayo,” aliwatangazia wenzake.
Wakamtakia heri.