• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
MSHAIRI WETU: Alex Maingi Ndungi almaarufu ‘Malenga Mamboleo’

MSHAIRI WETU: Alex Maingi Ndungi almaarufu ‘Malenga Mamboleo’

Na CHRIS ADUNGO

MBALI na kupitisha ujumbe maalum kwa wanajamii, ushairi ni sanaa ambayo imeibukia kuwa kipengele mahsusi cha burudani.

Ushairi ni fani pevu ya fasihi ambayo mbali na kutoa picha kamili ya jamii na kuwasilisha mawazo ya mtunzi, pia huinua kiwango cha umilisi wa lugha.

Katika kusoma, kukariri au kughani; mashairi huhimiza, huelimisha, huonya na kukemea maovu yanayofanywa na wanajamii kwa njia taratibu.

Hivyo, mashairi hulenga kupitisha ujumbe wa mafunzo mbalimbali na kuipa jamii mwelekeo. Haya ni maoni ya mshairi Alex Livingstone Maingi Ndungi almaarufu ‘Malenga Mamboleo’.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Nilizaliwa katika eneo la Muthetheni, Kaunti ya Machakos, nikiwa kitindamimba katika familia ya Bw Jackson Ndungi na Bi Felista Rhoda Ndunge.

Ulisomea wapi?

Katika Shule ya Msingi ya Miu D.E.B na kutamatisha masomo ya msingi shuleni Sunrise Academy, Makueni. Nilijipatia elimu ya sekondari katika

Shule za Upili za St Martins Utithini, Kimuuni na Kibauni, zote katika Kaunti ya Machakos. Nilijiunga baadaye na Chuo Kikuu cha Chuka, Kaunti ya Meru ninakosomea kwa sasa shahada ya B.A.

Nani na nini kilichokuchochea kuupenda ushairi? Nilipenda ushairi nikiwa mwanafunzi wa shule ya upili. Nilichochewa zaidi na upekee wa tungo katika kurasa za mashairi kwenye gazeti hili la ‘Taifa Leo’ na pia mafunzo ya mwalimu wangu, marehemu Bi Teresa Mwendwa (Mola amlaze pema penye wema).

Ulitunga lini shairi lako la kwanza?

Mnamo 2013 nikiwa mwanafunzi wa kidato cha pili. Mada ilikiwa ‘Mauti’. Nilipata ari zaidi ya kuuchangamkia ushairi wa Kiswahili katika chuo kikuu baada ya kujiunga na vyama vya ‘Writers Guild Chuka’ na Chama Cha Kiswahili cha Chuo Kikuu cha Chuka (CHAKICHU).

Mashairi yako huegemea zaidi mada zipi?

Hupania kuzamia mada zinazojadili masuala ibuka katika jamii, mapenzi, uongozi na nasaha kwa vijana. Wakati mwingine, marafiki zangu huniomba kuwatungia mashairi kuhusu mada tofauti wanazonipendekezea.

Nini hukuongoza kuteua mada za mashairi yako?

Mara nyingi, mimi hunuia kutoa ushauri kuhusu masuala tofauti kama mapenzi na maisha ya kila siku ya mwanajamii wa kawaida. Pia huchochewa kukejeli viongozi wanaofanya mambo yasiyofaa katika jamii, kutoa maonyo na hata kuzindua.

Unahitaji muda kiasi gani kutunga shairi moja?

Muda wa kutunga hutegemea uzito wa mada husika. Ninaweza kuchukua muda wa takriban dakika 30 kutunga shairi la tarbia lenye beti sita, kwa mada nyepesi. Mada nzito huweza kuchukua siku kadha kwa kuwa huhitaji utafiti wa kina kabla ya kuibua na kufululiza wazo kupitia beti.

Mbona mashairi ya arudhi?

Napenda mashairi ya arudhi kwa sababu ya mtiririko wake unaovutia. Pia yanadhihirisha kiwango cha ukomavu wa mtunzi.

Nini maoni yako kuhusu mashairi huru?

Huwa yana upungufu kwa sababu yanakiuka kanuni za utunzi. Hata hivyo, mwandishi anapaswa kuzingatia mtiririko wa mawazo katika utunzi wake.

Ushairi umekuvunia tija gani?

Nimewahi kutuzwa cheti kutoka Chama cha Kiswahili cha Chuka (CHAKICHU). Ushairi pia umenipa umaarufu na kunikutanisha na marafiki wengi. Nimepokea hongera nyingi pia kutoka kwa wasomaji wa mashairi yangu katika kumbi mbalimbali, hasa katika gazeti hili la Taifa Leo aghalabu kila wikendi.

Una mipango gani ya baadaye kuhusiana na ushairi?

Mungu akinijalia, nitachapisha diwani za ushairi katika siku za usoni.

Unakabiliana na changamoto zipi katika safari yako ya kukuza ushairi?

Mienendo hasi ya baadhi ya watu kuhusu ushairi na fasihi kwa jumla. Pia, watu wengi hawapendi kusoma.

Mbali na kutunga na (au) kughani mashairi, unafanya nini kingine?

Huwa naandika hadithi fupi na riwaya ambazo natumai zitachapishwa hivi karibuni. Pia huwa nashiriki uigizaji.

Unawashauri nini chipukizi na watangulizi wako kitaaluma?

Nawahimiza chipukizi watie fora zaidi bila ya kuchoka. Ninawaomba washairi wa zamani wazidi kuwa mwangaza na kielelezo cha kuigwa machoni mwa limbukeni wanaoibukia katika sanaa hii.

You can share this post!

SEKTA YA ELIMU: Serikali ichukue hatua madhubuti kuhusu...

SHANGAZI AKUJIBU: Nimepata fununu mke ana mimba na sidhani...

adminleo