UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Tathmini ya kina kuhusu matamshi katika Kiswahili
Na WANDERI KAMAU
MATAMSHI yanayopaswa kufundishwa shuleni nchini Kenya ni yale ya Kiswahili sanifu.
Je, tunapozungumzia matamshi ya Kiswahili sanifu, huwa hasa tunazungumzia matamshi ya aina gani?
Je, yapo matamshi yanayoweza kuhusishwa na Kiswahili sanifu hapa nchini Kenya. Ikiwa yapo, tunaweza kuyatambua vipi?
Matamshi ya Kiswahili sanifu hapa nchini Kenya yanaweza kuhusishwa na taasisi tofauti tofauti zinazotumia lugha ya Kiswahili.
Shule, kwa mfano, ni miongoni mwa asasi hizo.
Ingawa walimu tofautitofauti hutofautiana kwa jinsi wanavyotamka kwa sauti za Kiswahili, inafikiriwa kwamba walimu wengi wa lugha ya Kiswahili wanaweza kubainisha matamshi yaliyo sanifu kutokana na yale mengine.
Si walimu peke yao wanaoweza kufanya hivyo. Baadhi ya watumiaji wa kawaida wa lugha ya Kiswahili sanifu wanaweza pia kubainisha matamshi sanifu ya Kiswahili miongoni mwa matamshi mengine.
Taasisi nyingine zinazohusishwa na matamshi ya Kiswahili sanifu ni vyombo vya habari kama vile redio na televisheni.
Ingawa watumiaji wengi wa Kiswahili nchini Kenya wanaweza kubainisha matamshi ya Kiswahili sanifu na matamshi mengine, jambo hili halimaanishi kuwa wote wanaweza kuyatumia.
Baadhi ya watu wanaweza kutambua matamshi sanifu ingawa wao hawawezi au hawapendi kuyatumia.
Kuwepo kwa matamshi sanifu hakumaanishi kwamba watu wanaozungumza Kiswahili sanifu ndio pekee wanaoeleweka au wanaoelewana.
Ukweli ni kwamba, wazungumzaji wengi hueleweka na kuelewana kwa viwango mbalimbali japo hawatumii matamshi ya Kiswahili sanifu.
Hata hivyo, si wakati wote wazungumzaji hao wanapoelewana vizuri na wazungumzaji wengine wa Kiswahili sanifu.
Baadhi ya wazungumzaji hueleweka tu kwa shida, ilhali wengine hawaeleweki kamwe.
Jambo lingine linalopaswa kueleweka ni kwamba lugha ya Kiswahili ina lahaja zipatazo 15. Kati ya lahaja zote, moja tu ndio msingi wa Kiswahili sanifu.
Kwa hivyo, ingawa kuna wazungumzaji wengi wa Kiswahili katika Pwani ya Afrika Mashariki na kwingineko, siyo wote wanaozungumza Kiswahili sanifu.
Kwa hilo, inatupasa kuelewa kuwa kutamka Kiswahili sanifu hakumaanishi kuzungumza kama Waswahili wote wa Pwani ya Afrika Mashariki kwani wao hawazungumzi kwa njia moja.
Mwalimu anapaswa kuelewa kuwa matamshi atakayofundisha darasani ni yale yanayoweza kueleweka na wazungumzaji wengine wa Kiswahili sanifu, wawe ni wazawa wa Kiswahili au wazungumzaji wa Kiswahili wengine.
Kuzungumza kwa Kiswahili sanifu hakumaanishi kuzungumza kama wazawa wa Kiswahili.
Umuhimu wa kufahamu lugha za kwanza za wanafunzi: Mwalimu anayefundisha matamshi ya Kiswahili sanifu anapaswa kuwa na ufahamu wa fonolojia za lugha za kwanza/mama za wanafunzi wake. Hii ni kwa sababu mengi ya matamshi walio nayo wanafunzi nchini Kenya yanatokana na athari za lughamama.
Ufahamu wa lughamama za wanafunzi utamwezesha mwalimu kulinganisha sauti za lugha ya mama za mwanafunzi pamoja na ya Kiswahili.
Ulinganishaji wa aina hiyo utamwezesha mwalimu kubashiri matatizo ya matamshi yanayoweza kuwakumba wanafunzi wake. Isitoshe, mwalimu anayefahamu muundo wa lugha ya wanafunzi wake anaweza kukabiliana vizuri na matatizo yao ya kimatamshi yanayotokana na athari za lugha zao.
Ili kuufahamu mfumo wa sauti wa lugha ya mwanafunzi, mwalimu atahitaji ufahamu wa masuala kadhaa:
(a) Vitamkwa/ Sauti za lugha
Ingawa baadhi ya vitamkwa au sauti za lugha ya Kiswahili zinafanana na baadhi ya vitamkwa au sauti za lugha nyingine za Kenya, kuna baadhi ya vitamkwa ambavyo havifanani. Kwa hayo, njia moja inayotumiwa na walimu au wanaisimu kubashiria matatizo wanayoweza kuwa nayo wanafunzi au wazungumzaji wa Kiswahili kama lugha ya pili ni ulinganishaji wa vitamkwa vya Kiswahili na lughamama za wanafunzi.
Mwalimu anaweza kufanya hivyo kwa kuorodhesha vitamkwa.
Vitamkwa hupangwa katika jedwali kwa kufuata pahali pa kutamkia na jinsi ya kutamka, kwa mfano, sauti za midomoni, menoni (ufizini), masineni, kaakaani, sauti zenye mguno na, vipua (nazali ving’ong’o).
Baada ya kuonyesha vitamkwa vya kila lugha, hatua ya pili ni kuorodhesha vitamkwa visivyopatikana katika lugha ya kwanza na ambavyo vinapatikana katika lugha ya Kiswahili.
Katika makala yajayo, tutaangazia kwa kina mgawanyiko wa vitamkwa; vile vinapaswa kutamkwa na sehemu maalum vinavyopaswa kutamkiwa.