Gavana Dhadho ahimiza hatua za kiutu kusuluhisha mzozo wa mpaka
Na CHARLES WASONGA
GAVANA wa Kaunti ya Tana River Dhadho Godhana amewataka viongozi wa kaunti ya Garrisa kukoma kueneza chuki na uhasama kuhusiana na mzozo wa mpaka baina ya kaunti hizo mbili akisema suala hilo linafaa kushughulikiwa kwa amani.
Kwenye kikao na wanahabari alichokiandaa Ijumaa jijini Nairobi, Gavana Godhana alisema suala hilo limeripotiwa kwa asasi husika za serikali na hivyo viongozi wanafaa kukoma kuchochea vita baina ya wakazi wa kaunti hizi mbili.
“Suala hili tayari limeripotiwa kwa Wizara ya Usalama wa Ndani, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC), Makamishna wa Maeneo na wale wa kaunti. Kwa hivyo, watu wetu hawafai kutishwa na viongozi wa Garissa,” akasema Dhadho.
Gavana Dhadho pia alisema amezungumza na wazee kutoka kaunti hizo mbili, kiongozi wa ODM Raila Odinga na mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya ili waliingilie kati mzozo huo wa mpaka.
Oktoba 2019 Gavana wa Garissa Ali Korane na Mbunge wa Fafi Abdikarim Osman walidai kuwa serikali “imenyakua” maeneo ya Mansabubu, Nanighi, Abalatiro na Masalani ambayo yako karibu na mpaka wa kaunti hizo mbili huku wakitumia nguvu kuwafurusha watu wa Tana River kutoka maeneo hayo.
Gavana Korane na Bw Omar waliikashifu serikali kuanza kujenga ofisi za wasimamizi wa wadi, madarasa ya masomo ya chekechea na vituo vya afya katika maeneo ambayo walidai yako katika maeneobunge ya Fafi na Ijara.
“Huu mpaka ambao unasukuma kaunti ya Garissa umbali wa maili sita kutoka kwa mto Tana unafaa kufutiliwa mbali kwa sababu ni wa kikoloni. Hatuwezi kukubali serikali ya Tana River kuingilia himaya yetu kwa kuanzisha ujenzi katika maeneo yaliyoko katika eneobunge la Fafi na Ijara,” Gavana Korane akasema.
Naye Bw Omar alisema kuwa yuko tayari kuwashawishi wakazi wa eneobunge lake la Fafi kuhakikisha “tunakomboa sehemu za Mansabubu na Nanighi.”
Matamshi ya viongozi hao yaliwakera wabunge kutoka Tana River ambao wiki jana walijibu kwa kudai kuwa Mbw Korane na Omar walichochea vita na wanastahili kukamatwa.
Wakiongea na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi wabunge Ali Guyo Wario (Garsen), Said Hiribae (Galole), Ali Wario (Bura) na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti hiyo Rehema Hassan walimtaka Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai kuamuru kukamatwa kwa Gavana Korane na Bw Omar kwa kutisha raia wa Tana River.