• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:50 AM
MWANASIASA NGANGARI: Osogo: Alitia misingi sekta ya afya

MWANASIASA NGANGARI: Osogo: Alitia misingi sekta ya afya

Na KEYB

KINACHOPITA akilini unapozungumza na James Charles Nakhwanga Osogo ni kauli ya Shakespeare katika tamthilia yake As you like it: “Ulimwengu ni jukwaa, Na wanaume na Wanawake ni wachezaji; Wana pa kuingilia na pa kutokea; Na mwanamume mmoja katika wakati wake hucheza sehemu tofauti.”

Katika boma lake mtaani Kilimani, Nairobi, ushahidi wa kuzeeka kwa Osogo kwa heshima ni kitukuu wake msichana ambaye hawezi kumuacha babu yake peke yake. Ni wazi kuwa, siku moja msichana huyo atakuja kuelewa kwamba babu yake alikuwa mmoja wa viongozi wa kisiasa wa kwanza, aliyetoa mchango mkubwa kuweka msingi wa siasa uliofanya Kenya kuwa nchi ilivyo kwa sasa.

Osogo alipigana vita vingi vya kisiasa na kusimama imara wakati wa hali ngumu zaidi katika historia ya Kenya.

Mnamo 1975, kwa mfano, kufuatia kifo cha Josiah Mwangi Kariuki, Osogo ambaye alikuwa Waziri wa Afya, aliongoza juhudi za serikali za kuvuruga ripoti ya kamati teule ya bunge iliyomhusisha aliyekuwa kamishna wa polisi Bernard Hinga na kamanda wa kikosi cha kukabiliana na fujo (GSU) Benjamin Gethi na mauaji hayo.

Osogo aliyekuwa mbunge wa Busia Kusini (wakati huu Bunyala), aliwasilisha hoja akiomba bunge “kutambua na kuelewa badala ya kukubali ripoti hiyo.” Mswada huo uliofanyiwa mabadiliko ulishindwa. Wabunge walikasirika na hawakuweza kukubali chochote ambacho kingebadilisha mswada wenyewe.

Osogo anaeleza mazingira ambayo aliwasilisha mswada huo akisema: “Sikuwa na nia mbaya. Nilichotaka kilikuwa ni kuokoa ripoti ya Mwangale. Kilichofanyika ni kuwa ripoti ya awali niliyokuwa nimeona ilikuwa na majina mengi (ya watu waliohusishwa) ikilinganishwa na ile ambayo Mwangale alikuwa amewasilisha bungeni. Ilionekana kuwa Mwangale alikuwa amelazimishwa kuondoa ripoti ya kwanza kwa sababu majina ya baadhi ya wanasiasa wakuu yalikuwemo na baadhi yetu tulikuwa tumeona ripoti hiyo.”

Ikiwa ni kwa sababu ya kuwa upande wa serikali wakati bunge na watu wengi walikuwa wakiipinga ni jambo la mtu kung’amua. Kilicho wazi ni kuwa baada ya mauaji ya JM, maisha yake ya kisiasa yalibadilika na akapadishwa cheo kuwa naibu kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.

Osogo alizaliwa katika kijiji kidogo cha Bukani wilayani Bunyala mwaka wa 1932, akiwa mwana wa pili katika familia ya watoto 10.

Alilelewa katika familia ya Wakatoliki na baba yake alikuwa afisa wa kanisa la kwao.

Kwa hakika, anasema akiwa mtoto, azma yake ilikuwa ni kujiunga na seminari na kuwa padre lakini hili halikutimia. Alijipata katika shule maarufu ya Katoliki ya St Marys Yala, ambayo ilikuza talanta za Wakenya wengi wakati huo.

Wanafunzi wenzake walikuwa ni pamoja na Thomas Joseph Mboya.

Baada ya shule, Osogo aliwazia kujiunga na jeshi, hasa kikosi cha wanamaji lakini nafasi hazikuwa nyingi na akaajiriwa na shirika la reli la Afrika Mashariki ambalo lilikuwa likitoa nafasi za ajira kwa watu wengi enzi hizo. Alipata mafunzo katika taasisi ya mafunzo ya reli jijini Nairobi.

Ikiwa azima yake ya kuwa mwanasiasa, hasa dhidi ya wakoloni ilianza akiwa Yala, kujiunga kwake na taasisi ya mafunzo ya reli kulimhusisha moja kwa moja na ukatili wa ubepari.

Alishuhudia na kushiriki maandamano yaliyoitishwa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi kama Markhan Singh na Kung’u Karumba.

Baada ya kumaliza mafunzo yake, aliajiriwa kama naibu meneja wa kituo cha reli na akahudumu maeneo tofauti Kenya na Uganda.

“Hii ilinipatia fursa ya kusafiri nchi zote mbili na kukutana na watu wengi,” anakumbuka.

Hata hivyo, anaeleza kuwa moyo wake haukuwa katika shirika la reli. Alipenda kazi ya kufunza “ ambayo kwangu ilikuwa karibu na siasa kwa sababu kwa kupatia watu maarifa, unawashawishi kuelekea maendeleo.”

Kilichomfanya kuacha kazi katika shirika hilo ilikuwa ni kubaguliwa kwa waafrika ambao hangevumilia na mara kwa mara alitofautiana na wasimamizi wa reli waliokuwa wakoloni.

Mwaka wa 1953, alijiunga na chuo cha mafunzo ya walimu cha Kagumo na akahitimu baada ya miaka mitatu. Baada ya kuhitimu, Osogo alitumwa Sigalame Intermediate School katika wilaya ya nyumbani kwao ya Busia ambako alijiunga na siasa akiwa diwani katika Nyanza African District Council.

Alihudumu kama mwalimu na diwani kwa wakati mmoja akiwa na umri wa miaka 24.

Baraza la wilaya lilivunjwa baada ya miaka miwili kwa sababu Osogo na wenzake walikuwa wakikosoa serikali ya wakoloni.

Mnamo 1959, Osogo alihamishiwa shule ya Port Victoria Intermediate School na ni mwaka huo alipooa mke wake wa kwanza, Maria.

Hata hivyo, hakukaa sana Port Victoria. Katika kipindi cha mwaka mmoja alitofautiana na serikali ya wakoloni alipoikosoa kwa kunyima jamii yake ya Bunyala haki zao za uvuvi.

Kwa sababu hii alihamishiwa shule ya Kabasaka Intermediate, wilaya ya Nandi na kutengwa na watu wa jamii yake.

“Hili lilinikasirisha lakini nikakubali nikijua kwamba katika mipango yetu, uhamisho huo ulikuwa wa muda kabla ya kurudi kuwahudumia watu kikamilifu,” alisema.

Chama cha Kanu kilipoundwa mwaka wa 1960, Osogo alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kujiunga nacho.

Alionyesha kuwa na uhuru wa kuamua mambo kwa kubaki katika Kanu hata wakati jamii yake ya Waluhya ilihamia Kadu, sababu moja ikiwa mmoja wa viongozi mashuhuri alikuwa ni Muliro, mwakilishi wa pekee wa Elgon Nyanza (Western Province) katika Legco .

“Nilihisi kwamba tulihitaji chama cha kitaifa ambacho kingeunganisha Wakenya wawe na nguvu ya kushinda wakoloni na kwamba mgawanyiko ungetufanya wadhaifu,” aeleza.

Kwenye uchaguzi uliofuatia katiba iliyoandaliwa Lancaster 1961, eneo la Bunyala alilotoka lilikuwa katika wilaya ya Central Nyanza na lilivutia wagombeaji wanane katika uchaguzi. Alijaribu bahati na matokeo yalipotolewa alikuwa wa tatu nyuma ya Odinga na Kodhek.

Baada ya uchaguzi, aliwania kuteuliwa na Kanu lakini nafasi hiyo ilichukuliwa na Walter Odede. Kadu ilimteua Peter Habenga Okondo, ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Osogo.

Kinyang’anyiro cha kwanza kati ya Osogo na Okondo kilikuwa 1963 wakati wa mageuzi ya kisiasa yaliyofuatia uhuru. Kwenye uchaguzi wa kiti cha ubunge cha Ruwambwa, Osogo aliibuka mshindi, ingawa Okondo alikuwa amepigiwa upatu kwa sababu alikuwa mbunge wa kuteuliwa na alikuwa amesoma zaidi.

Okondo alikuwa na digrii ya masuala ya biashara kutoka chuo kikuu cha Cape Town na alikuwa ameshikilia nyadhifa kuu katika wizara ya fedha Kenya na Uganda.

Alipoingia bungeni kwa mara ya kwanza, Osogo aliteuliwa waziri msaidizi wa kilimo chini ya waziri wa kilimo wakati huo Bruce McKenzie.

Uhusiano kati ya Rais Jomo Kenyatta na makamu wake Odinga ulipogeuka na kuwa uadui mkubwa, Osogo alinufaika. Kwenye mabadiliko ya baraza la mawaziri 1966, aliteuliwa waziri wa Habari na Mawasiliano na kuchukua nafasi ya Oneko.

Ushindani wa kisiasa kati ya Osogo na Okondo ulijirudia 1969. Osogo alimshinda Okondo tena lakini kwa kura 600 pekee. Kenyatta alimteua Osogo waziri wa biashara na viwanda.

“Baadhi ya viwanda vikubwa Kenya vilianzishwa nikiwa waziri wa viwanda,” alisema Bw Osogo.

Anataja kiwanda cha Pan African Paper Mills, Firestone Tyre Company (sasa Yana) na kampuni ya sukari ya Mumias kama baadhi ya viwanda hivyo.

Kutoka wizara ya biashara na viwanda, Osogo alihamishiwa wizara ya serikali za wilaya ambapo alibadilisha vituo vingi vya kibiashara kuwa miji.

Mnamo 1974, Okondo alibadilisha mbinu na kuamua kutogombea kiti cha ubunge cha Busia South na akamuunga James Ombere Okoch, ambaye alikuwa na uhusiano wa kifamilia na Osogo. Hata hivyo, Osogo alishinda japo kwa kura chache. Aliteuliwa waziri wa afya wakati ambao sekta hiyo ilikuwa ikikumbwa na changamoto nyingi.

Hospitali kuu ya Kenyatta, iliyokuwa hospitali ya rufaa na ya pekee ilikuwa katika hali mbaya. Madaktari walikuwa wakitisha kugoma wakilalamikia mazingira duni ya kazi na kuishi.

Osogo alipowasilisha mswada wa kuthibiti sekta hiyo, madaktari waliukataa na akatumia ujasiri kutatua shida hiyo.

Ni akiwa waziri wa afya ambapo vituo vingi vya matibabu vilijengwa nchini.

Kenyatta alipokufa 1978, maisha yake yalibadilika na akaanza kukabiliwa na changamoto mpya.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 1979, Osogo alimshinda Okondo tena na Moi akamteua waziri wa kilimo na akaendelea kuwa naibu kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, wadhifa aliotwaa Juni 1975.

Dalili kwamba mambo hayangekuwa mazuri kwa Osogo zilijitokeza wizara yake ilipogawanywa mara mbili miaka ya 1980 na akahamishiwa wizara ya mifugo.

Osogo alipoteza kiti chake cha ubunge 1981 kupitia kesi ya uchaguzi na akapigwa marafuku kugombea kwa miaka mitano.

Kwenye uchaguzi mdogo, Okondo, akiungwa na Kanu hakupingwa. Okondo alishinda tena 1983 na 1988.

Siasa za vyama vingi zilipoanza, Osogo alijiunga na chama cha Ford Kenya na akawa mwenyekiti wa tawi la Busia la chama hicho. Hata hivyo, hakukaa sana katika upinzani Moi alipomshawishi arudi Kanu.

Alishinda kiti cha eneobunge la Bunyala na akateuliwa waziri msaidizi wa biashara, jambo ambalo hakutarajia.

Mnamo 1977, akiwa na Achieng Oneko, mwenyekiti mwenza wa Inter Parties Parliamentary Group (IPPG), walifaulu kuleta mageuzi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo.Kwenye uchaguzi mkuu wa 2002, alishindwa na Raphael Wanjala katika uchaguzi wa kiti cha eneobunge la Budalang’i na akaamua kustaafu siasa.

 

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke

  • Tags

You can share this post!

Raila amtembelea Joho kumjulia hali

KINAYA: ‘Tangatanga’ wamebwagwa sasa wakubali...

adminleo