• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Harambee Starlets mawindoni kuzoa ushindi dhidi ya Djibouti

Harambee Starlets mawindoni kuzoa ushindi dhidi ya Djibouti

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya soka ya wanawake ya Kenya almaarufu Harambee Starlets itarejea uwanjani Chamazi leo Jumanne na ari ya kutafuta ushindi wake wa pili mfululizo kwenye mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), itakapokutana na Djibouti jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Katika mechi hii ya Kundi B, Starlets italenga kuvuna ushindi mkubwa dhidi ya washiriki hao wapya waliokaribishwa katika ulingo wa kimataifa kwa kuzabwa 13-0 na Uganda mnamo Novemba 17.

Vipusa wa kocha David Ouma walifungua kampeni yao kwa kushangaza Ethiopia 2-0 kupitia mabao ya Jentrix Shikangwa na Cynthia Musungu.

Idadi ya magoli huenda ikaamua timu mbili zitakazoingia nusu-fainali kutoka kundi hili ikiwa Ethiopia italemea Uganda baadaye leo. Inamaanisha kuwa Kenya haihitaji tu ushindi dhidi ya Djibouti ya kocha Mfaransa mwenye asili ya Tunisia, Sarah M’Barek, bali ushindi mkubwa.

Baada ya kuchapa Ethiopia, Ouma alisema ilikuwa muhimu Kenya kuanza mashindano haya vyema inapolenga kuimarika yanapoendelea.

“Idara tunayohitaji kuimarisha zaidi ni upigaji wa ikabu. Bado safari ni ndefu, lakini tunalenga kufanya vizuri hata zaidi tutakapomenyana na Uganda katika mechi yetu ya mwisho ya makundi (Novemba 21),” aliongeza.

Starlets ilisikitika mwaka 2018 ilipomaliza katika nafasi ya nne kati ya mataifa matano yaliyoshiriki baada ya kupata ushindi mmoja pekee – dhidi ya wenyeji Rwanda.

Kundi A linajumuisha Tanzania, Burundi, Sudan Kusini na Zanzibar. Tanzania ilipepeta Sudan Kusini 9-0 nayo Burundi ikalemea Zanzibar 5-0 katika siku ya kwanza ya mashindano mnamo Novemba 16.

Sudan Kusini yaipiga Zanzibar

Jumatatu, Sudan Kusini, ambayo inashiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza kabisa, iliduwaza Zanzibar inayorejea baada ya kukosa mwaka 2018, kwa mabao 5-0.

Waliofungia Sudan Kusini ni Amy Lasu dakika ya 24 na 82, Suzy Iriamba (39) na Aluel Garang (77). Nahodha wa Zanzibar, Mwajuma Abdallah pia alijifunga dakika ya 62. Tanzania na Burundi zilitarajiwa kulimana baadaye jana.

Sudan Kusini itarejea uwanjani hapo kesho kuvaana na Burundi nayo Zanzibar ipepetane na Tanzania. Mechi za nusu-fainali ni Novemba 23, huku ile ya kutafuta mshindi wa medali ya shaba na fainali ni Novemba 25.

Kikosi cha Kenya: Wachezaji – Annette Kundu, Vivian Nasaka, Nelly Sawe, Dorcas Shikobe, Ruth Ingosi, Corazone Odhiambo, Topista Situma, Sheril Angachi, Mwanalima Adam, Cynthia Shilwatso, Janet Bundi, Judith Osimbo, Monicah Odato, Lucy Akoth, Mercy Airo, Siliya Lumasia, Jentrix Shikangwa, Lydia Akoth, Wincate Kaari, Elizabeth Wambui.

You can share this post!

Uholanzi kukosa difenda nguli inapokabili Estonia

Gor Mahia yarejea nyumbani na kumulika ligi kuu

adminleo