Imran Okoth aapishwa rasmi kuanza majukumu ya ubunge Kibra
Na CHARLES WASONGA
BENARD Otieno Okoth ‘Imran’ ameapishwa rasmi Jumanne kuanza kutekeleza majukumu yake akiwa mbunge wa Kibra baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi mdogo uliofanyika Novemba 7, 2019.
Aliapishwa na karani wa bunge la kitaifa Michael Sialai bungeni katika kikao cha alasiri mbele ya Spika wa bunge hilo Justin Muturi.
Mbunge Maalum Maina Kamanda na mwenzake wa Mathare Anthony Oluoch ndio wamemsindikiza Bw Okoth kuingia bungeni na kumwelekeza hadi eneo la kula kiapo.
Bw Kamanda ambaye ni mbunge wa chama tawala cha Jubilee, ni miongoni mwa wanasiasa wa chama hicho waliompigia debe Bw Okoth alipowania kwa tiketi ya chama cha ODM na kuibuka mshindi kuwa kuzoa kura 24,636.
Naye mgombeaji wa Jubilee McDonald Mariga ambaye kampeni zake ziliongozwa na Naibu Rais William Ruto akisaidiana na wabunge kadha wa mrengo wa ‘Tangatanga’ alikuwa wa pili kwa kupata kura 11,230.
Aliyeshikilia nambari tatu ni aliyepeperusha bendera ya ANC Eliud Owalo aliyejizolea jumla ya kura 5,275 huku Khamisi Butich wa Ford Kenya akiwa wa nne kwa kupata kura 260 pekee.
Jumla ya wawaniaji 24 walishiriki katika kinyang’anyiro cha kujaza nafasi hiyo iliyosalia wazi kufuatia kifo cha Ken Okoth mnamo Julai 26, 2019, baada ya kuugua kansa ya utumbo.
Fujo zilishuhudiwa katika maeneo kadha katika eneobunge hilo baada ya watu fulani kudai kuwa walikuwa wakiwahonga wapigakura.
Baada ya wabunge wa mrengo wa ‘Tangatanga’ walihangaishwa na watu waliodaiwa kuwa kundi la vijana waliokuwa wakilinda kura.
Baadhi ya wabunge wa mrengo wa ‘Tangatanga’ waliojiopata pabaya siku hiyo walikuwa pamoja na Didmus Barasa (Kimilili), Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Malulu Injendi (Malava), na aliyekuwa Seneta wa Kakamega Dkt Boni Khalwale.