• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
SHANGAZI AKUJIBU: Naogopa kusalitiwa na mume mtarajiwa, nifanyeje?

SHANGAZI AKUJIBU: Naogopa kusalitiwa na mume mtarajiwa, nifanyeje?

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nilikuwa na mpenzi na akaniacha baada ya kunipa mimba. Baadaye nilipata mwingine ambaye nilikuwa na matumaini kwake kwamba atanioa. Muda si mrefu nilimuacha nilipogundua alikuwa na uhusiano na mwanamke mwingine. Sasa nimepata mwingine ambaye yuko tayari kunioa. Shida ni kuwa nimeshindwa kumwamini ingawa sina sababu. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Ninaamini kwamba hali yako hiyo inatokana na hofu kwamba mwanamume huyo anaweza kukutendea ulivyotendewa na hao wengine. Ushauri wangu ni kuwa uende taratibu usije ukajipata tena katika hali hiyo. Jipe muda umchunguze kwanza hadi utakapotosheka kwamba anakupenda na ana nia nzuri kwako ndipo umruhusu kuingia katika maisha yako.

 

Hanitaki tena kwa kuwa wazazi wake wanasema natoka jamii tofauti

Kwako shangazi. Mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka mitatu ameniambia hawezi kunioa kwa sababu wazazi wake wamemkataza kuoa mwanamke wa jamii tofauti na yao. Ninampenda kwa moyo wangu wote na uamuzi wake huo umeniacha hali mbaya. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Uamuzi wa mpenzi wako ni thibitisho kwamba amekubali ushauri wa wazazi wake. Ingawa unasema unampenda, hakuna haja uendelee kuhangaika juu yake ilhali unajua huwezi kumpata kwa sababu amekuelezea msimamo wake.

 

Kijana anipendaye si mwaminifu, sasa nifanye nini?

Shangazi pokea salamu zangu. Ni matumaini yangu kwamba wewe ni mzima. Nina umri wa miaka 23 na ninasoma katika chuo kikuu. Nina urafiki na kijana fulani lakini si mwaminifu kwangu na anasema anataka kunioa. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Uwe ni urafiki au mapenzi, si jambo la busara kuendeleza uhusiano kama huo na mtu ambaye unajua kwa hakika si mwaminifu kwako. Kama kijana huyo si mwaminifu sasa, sidhani atabadilika akikuoa na huenda akawa mbaya hata zaidi.

 

Nampenda lakini ni mtu wa kukasirika bila sababu

Shikamoo shangazi! Nina mpenzi ambaye nampenda sana lakini kuna jambo moja tu ambalo linanitatiza kumhusu. Kuna nyakati ambapo huwa anakasirika bure tu na nikimuuliza kiini cha hasira zake anazua ugomvi. Hali yake hiyo inanitia wasiwasi. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni vigumu kuishi na mtu usiyeweza kuelewa au kutabiri hisia zake kama huyo mpenzi wako. Itakuwa vyema umwelezee unavyohisi kuhusu hali yake hiyo uone kama atajirekebisha. Asipobadilika utaamua iwapo unataka kuendelea naye ama mtaachana.

 

Tulipendana majuzi tu, lakini nahisi ana mwingine

Kwako shangazi. Nilikutana na mwanamume fulani majuzi na tukapendana. Aliniambia hana mpenzi lakini baadaye nikakutana naye akiwa na mwanamke mwingine. Nilipomuuliza aliniambia eti mwanamke huyo ndiye anayemfuata akitaka wawe wapenzi. Sikuamini kauli yake hiyo kwani si kawaida ya mwanamke kumtongoza mwanamume. Nishauri.

Kupitia SMS

Nahisi kuwa mwanamume huyo hajakwambia ukweli kuhusu kinachoendelea kati yake na mwanamke huyo. Inawezekana wamekuwa wapenzi na labda anataka kumuacha lakini bado hajakata kauli na ndiyo maana bado wanakutana. Huenda pia ameamua kujaribu bahati yake kwenu wawili kwa wakati mmoja. Chunguza kwa makini ujue ukweli ndipo uweze kufanya uamuzi.

 

Mume huniacha nikitamani zaidi…

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 30. Nimeolewa na nampenda mume wangu sana. Shida ni kuwa tukianza kula vya chumbani yeye anatosheka haraka sana na kuniacha nikitamani zaidi. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Maana ya ndoa ni kusaidiana na kufaana katika kila jambo na kila hali ili kuidumisha. Ninaamini kwamba hali hiyo ya mume wako inaweza kutatuliwa kupitia ushirikiano wenu kwa pamoja. Tafuta wakati mzuri uzungumze naye kuhusu suala hilo ili muone namna ya kulitatua.

You can share this post!

SEKTA YA ELIMU: Waliopata alama 350-399 katika hali ngumu...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sheng haina mashiko wala miaka...

adminleo