• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sheng haina mashiko wala miaka – Wallah Bin Wallah

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sheng haina mashiko wala miaka – Wallah Bin Wallah

Na CHRIS ADUNGO

GURU Ustadh Wallah Bin Wallah anashikilia kwamba Sheng haina msingi wowote wenye uwezo wa kutikisa uthabiti wa Kiswahili.

Kulingana na mwalimu na mwandishi huyu maarufu ndani na nje ya Afrika Mashariki, yeyote anayehisi kwamba Sheng ni tishio kwa maendeleo ya Kiswahili ni sawa na mtu anayetishwa na kivuli chake!

“Kivuli hakimpigi mtu!” anasema Guru Ustadh Wallah Bin Wallah kwa kusisitiza kwamba wengi wa watu wanaotumia Sheng hukirudia Kiswahili Mufti kila wanapojipata katika mazingira rasmi kwa mfano ya darasani.

“Mtu yeyote katika nchi ya Kenya anapoongea na mwenzake, ana uwezo wa kuongea lugha yake ya nyumbani. Akienda shuleni, hujua ni wakati wa kuzungumza Kiswahili, tena Kiswahili Mufti! Vivyo hivyo, huyo anayeongea Sheng angepelekwa darasani, hawezi akapeleka Sheng!” anatanguliza.

“Kwa nini tufikirie kwamba Sheng ni tishio kwa makuzi ya Kiswahili ilhali nchi ya Kenya ina zaidi ya makabila 40? Kwa nini tusiseme kuwa hata hizi lugha zetu za asili ni tishio? Nani wamewahi kulaumiwa kwa kuzungumza lugha yao ya nyumbani? Kwa nini basi tuwalaumu vijana wawili au watatu wa mitaani wanapoongea Sheng? Sheng haina shida yoyote maanake kila lugha ina pahali pake!” anasema Guru Ustadh ambaye ni mmiliki wa WASTA Kituo cha Kiswahili Mufti katika eneo la Matasia, Ngong mjini.

Hii hapa fasili ya Sheng kwa mujibu wa Guru Ustadh Wallah Bin Wallah – Doyen wa Kiswahili anayejivunia kuandika vitabu vingi vya kutia moyo na kumshajiisha yeyote mwenye azma ya kujiendeleza maishani na kitaaluma.

“Sheng si lugha. Sheng ni upuzi wa watu wawili au watatu au vijana tu wa mitaani ambao hutumia maneno yao ya ajabu ajabu ili waelewane wao kwa wao. Kila wakati, hiyo Sheng haina mashiko wala miaka. Mwaka ule walitumia maneno yale, yakapotea. Mwaka huu wanatumia maneno haya na wataacha.”

Uandishi wa Wallah Bin Wallah siku zote umepania kumchochea mwanafunzi pamoja na mwalimu kujitambua, kisha kujiboresha katika jitihada za kuyasaka malezi bora ya kiakademia. Mvuto na mguso uliomo ndani ya vitabu vyake vyote una uwezo wa kubadilisha kabisa mkondo wa fikira na mitazamo ya wengi wasiofahamu uzito, ukubwa na utamu wa thamani ya kujifunza Kiswahili bora.

Nina hakika hutabaki jinsi ulivyo wala kuendelea kuwaza kwa namna ulivyozoea pindi utakapofanikiwa kusoma ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho wa kitabu chake chochote. Kulingana na Wallah Bin Wallah, ipo haja ya kuielewa lugha kuwa kielelezo cha utamaduni na njia mahsusi ya kuelezea na kusambazia utamaduni wenyewe. Katika maana hii, Kiswahili kina kama nafasi kuwa ya kuwa wenzo na mbinu maalumu ya kuelezea utamaduni asilia wa Mwafrika.

Utamaduni ni jumla ya mfumo wa asasi, amali, mielekeo, fikira na desturi zinazoitambulisha jamii fulani katika kipindi fulani cha historia. Dhana ya utamaduni pia hutumiwa kuelezea jamii ya watu iliyostaarabika, kuelimika au kuendelea katika vipengele fulani vya maisha. Jamii au kikundi hicho husika sharti kiwe kinatambuliwa na kinajitambulisha kama jamii moja. Mfumo wa imani na fikira unaotokana na utaratibu wa elimu, mafunzo na mila au desturi unaosababisha kukomaa kwa watu wa jamii fulani pia unaweza kuitwa utamaduni.

Lo Liyong (1972) amefafanua utamaduni kama “jumla ya shughuli, kumbukumbu, matumaini, mipango ya baadaye ya jamii fulani pamoja na ndoto na maono yao”.

Sheng ni mfumo wa mawasiliano ambao umesanifiwa na vijana hasa wale wanaoishi katika sehemu za mijini. Mfumo wenyewe hufuata muundo wa sarufi ya Kiswahili na lugha nyinginezo za Kibantu huku ukitumia maneno mengi mapya ya kubuniwa na ya mkopo kutokana na lugha mbalimbali kikiwemo Kiingereza na lugha nyinginezo za Kiafrika.

Maelezo haya ya kijumla kuhusu maana ya Sheng yametolewa pia na wasomi kama vile marehemu Katama Mkangi ambaye aliueleza msimbo huu kuwa lugha mseto au lugha “kiunzi” ya kizazi kipya cha vijana wa mijini (1984).

Pia Ogechi (2002) na Shitemi (2001) wanakubaliana na maoni hayo kwamba Sheng ni msimbo wa kijamii unaotumiwa hasa na vijana wa mijini na mashambani nchini Kenya. Maelezo haya yanatoa baadhi ya sifa za kimsingi zinazoutambulisha msimbo huu.

Kwa mujibu wa Mukhebi (1986), Sheng ni tukio la kitamaduni ambalo linafungamana sana na mawazo au fikira, hisia na matakwa ya watumiaji wake.

Anaeleza kuwa wazungumzaji asilia wa Sheng waligundua kuwa kutokana na hali na mazingira yao ya kifukara katika mitaa ya jamii yenye mapato ya chini, wasingeweza kupata elimu yao na kuwasiliana kupitia kwa Kiingereza pekee. Walihitaji mfumo wao wenyewe. Kutokana na ufahamu wao duni wa Kiingereza, iliwawia vigumu vijana hao kujifunza masomo mseto kwa Kiingereza, masomo yaliyokuwa ya kimsingi katika mitaala ya shule za msingi wakati huo.

Kuna nadharia mbalimbali zinazojaribu kueleza chimbuko na asili ya Sheng. Hata hivyo, nadharia kuu ni mbili; nadharia ya uhuni na nadharia ya msimbo wa vijana amabzo tutazijadili katika makala yajayo.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Naogopa kusalitiwa na mume mtarajiwa,...

Shule binafsi zafanya vyema katika KCPE 2019

adminleo