Habari

Mvua iliyopitiliza kiwango yatarajiwa wiki hii – idara ya utabiri wa hali ya hewa

November 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wameonywa kujiandaa kwa mvua iliyopitiliza kiwango wiki hii kutokana na kiwango cha joto kuongezeka katika Bahari Hindi.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa ilisema Jumanne kuwa kiwango cha joto katika bahari Hindi kimeongezeka, hali inayofahamika kama Indian Ocean Dipole, inayotokea kila baada ya miaka 10 na kusababisha mvua iliyopitiliza kiwango inayoweza kusababisha mafuriko na uharibifu Afrika Mashariki.

Naibu Mkurugenzi wa idara hiyo, David Gikungu alisema kwenye taarifa kuwa mvua iliyopitiliza kiwango ilitarajiwa kuanza usiku na kuendelea kuongezeka kwa wiki moja.

Tayari watu 1 milioni wameathiriwa na mafuriko nchini Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Ethiopia na Tanzania na wanasayansi wanasema hali inaweza kuwa mbaya zaidi mvua inapoongezeka wiki hii.

Kulingana na Bw Gikungu, mvua inatarajiwa kuzidi Milimita 40 kufikia Alhamisi na kuendelea hadi Jumapili, Novemba 24 2019.

Alisema kutakuwa na vipindi vya jua katika muda ambao mvua inatarajiwa kunyesha wiki hii.

Wiki jana, Naibu Mkurugezi wa Idara ya Utabiri wa hewa Stella Aura alionya kuwa kiwango cha joto katika Indian Ocean Dipole kinaweza kusababisha mvua kubwa na mafuriko.

“Mafuriko ya ghafla yatatokea hata katika maeneo ambayo hayatanyesha na yanaweza kuwa makubwa na yenye kasi kuliko yatakavyoonekana,” alisema Bi Aura.

Tahadhari

Alishauri Wakenya kuepuka kuendesha magari au kuvuka maeneo yaliyofurika maji na kuepuka kujikinga mvua chini ya miti au majengo yaliyo na dirisha za vyuma wasipigwe na radi.

Aidha, Bi Aura aliwaonya watu wanaoishi maeneo yanayokumbwa na hatari ya maporomoko ya ardhi hasa karibu na milima ya Aberdare Ranges, Mlima Kenya na magharibi mwa Kenya.

Kulingana na Shirika la Msalaba mwekundu nchini, mvua inayoendelea kunyesha imesababisha vifo vya watu 48 na kuacha mamia bila makao nchini.

Wiki jana, mvua kubwa iliponda kaunti ya Mombasa na kuharibu barabara na nyumba kujaa maji. Wakazi waliohofia kuzuka kwa maradhi kufuatia mafuriko hayo.