• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
AKILIMALI: Donge la Uyoga lapiku mahindi

AKILIMALI: Donge la Uyoga lapiku mahindi

Na RICHARD MAOSI

ILI mkulima aweze kutengeneza hela ndefu kutokana na ukulima wa mahindi ni lazima amiliki vipande vikubwa vya ardhi na asubiri kwa hadi kipindi cha miezi sita hivi ili mavuno yawe tayari.

Hata hivyo, wakulima wa uyoga hawana taabu ya kutumia shamba wala muda mrefu wa kusubiri mavuno yao.

Upanzi wa uyoga hautegemei hali ya hewa, kwani ni shughuli inayoweza kufanyika katika sehemu yoyote hata ndani ya kitalu muradi mkulima azingatie kanuni zote zinazohitajika.

Uyoga aina ya Button ni maarufu katika mji wa wa Nairobi, na viungani mwake ni kwa sababu hiyo Akilimali ilipiga kambi katika mtaa wa Kangemi kilomita 3 hivi kutoka mjini ili kupambanua hali halisi.

Tulikutana na kijana Moses Maurice Ikonya kijana aliyeamua kujiajiri mwishoni mwa 2018, baada ya kuhitimu kutoka chuo Kikuu akaamua kujipatia riziki na kuwaajiri vijana wenzake.

Ikonya ni miongoni mwa wanachama wa Mushroom Growers Association Of Kenya na kufikia sasa, analenga kuwaleta pamoja wakulima kutoka kote nchini wasiokuwa na soko kwa bidhaa hii adimu.

Katika kipande cha ardhi ametengeneza kijumba cha futi 10 kwa 15 mstatili, ambapo anatumia kama hifadhi ya uyoga, anasema kuwa usalama kwa mimea hii ni jambo la kimsingi kabla ya kuanzisha mradi.

Mbali na kukuza uyoga anatengeneza lishe maarufu ya starfry ambayo ni chaguo la wanunuzi wengi wanaofika katika maduka ya kijumla ya kutafuta uyoga na kuambatanisha na Starfry.

“Mbali na kukuza uyoga tunawahimiza wakenya kuchangamkia lishe hii ambayo ni ya manufaa tele katika afya ya binadamu, ni kama vile michicha ya kiasili na sukumawiki,” akasema.

Kwa mtaji wa 150,000 aliweza kununua katoni ya mbegu za uyoga kutoka Afrika Kusini, pamoja na mahitaji mengine kama vile Molasi, mpunga, magunia na mchanga safi ambao haujapuliziwa dawa.

“Kawaida zao la uyoga hufanya vizuri ndani ya chumba chenye giza almuradi mzunguko wa hewa safi na kiwango sahihi cha mchanga uliojazwa ndani ya magunia,” Ikonya alisema.

Ikonya anasema kuwa changamoto inayowalemea wakulima ni upatikanaji wa mbegu za uyoga, ambazo hazikuzwi humu nchini isipokua kuagiza kutoka nchini Afrika kusini jambo lenyewe hufanya wakulima wengi kutozwa hela nyingi za ushuru wa mbegu za kuagiza kutoka nje.

Ikonya anasema kuwa kabla ya kupanda mbegu mkulima atalazimika kuacha mchanganyiko wa mbolea kukolea, kwa kipindi cha mwezi mmoja hivi ili aweke mbegu za uyoga ndani ya mchanga.

Wakati huo akiendelea kugeuzageuza mbolea kwa muda wa mwezi mmoja, huku akimwagilia maji kidogo mchana na jioni kila siku ili unyevu uweze kupunguza kiwango cha joto ndani ya jumba la kukuza uyoga.

“Mchanganyiko huo huanza kupata joto ambalo pia husaidia kuangamiza vidudu hatari, ambao wanaweza kusababisha mkurupuko wa maradhi ambayo ni hatari kwa uyoga,” aliongezea.

Hatimaye kiwango cha joto huteremshwa hadi nyusi 18 hivi kisha dirisha na milango ikafunguliwa ili hewa safi na mwanagaza upate kupenya ndani na kufikia uyoga.

Mabadiliko ya ghafla baada ya kuruhusu mwangaza na hewa safi, ndio hufanya uyoga ukaanza kuchipuka na baina ya siku 45-65 mimea yako huwa iko tayari kwa ajili ya mavuno na mauzo.

Mkulima anaweza kuendelea kupata mavuno yake kwa miezi minne mtawalia bila kukatika. Ikonya alitueleza kuwa anamiliki magunia 300 ndani ya jumba lake maalum la kukuza uyoga, ambapo kila mfuko unaweza kubeba kilo mbili ya uyoga.

Kulingana naye bei ya uyoga inaweza kubadilika sokoni kulingana na mahitaji ya wanunuzi, akipiga hesabu zake kilo moja inaweza kufika 1000 msimu ukiwa ni mzuri.

Mavuno

Kwa jumla anaweza kuvuna kilo 600 ambazo humpatia takribani 600, 000 hii ni endapo mkulima atafuata utaratibu wote unaohitajika kutekeleza aina hii ya kilimo.

Ikonya alieleza kuwa mbali na kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto za ukosefu wa soko kwa bidhaa zao, anashirikiana nao pia kutoa hamasisho kote nchini ili kuhakikisha kuwa wanapata mbegu na mbolea kwa wakati.

Ikonya anashauri serikali ya kitaifa kuwekeza katika utafiti wa uyoga ili wakulima wengi wasiokuwa na uwezo, wapate kujitosa katika kilimo hiki cha aina yake kisichokuwa na ushindani.

“Utafiti utawasaidia wakulima kuzalisha uyoga wa hali ya juu kwa bei nafuu humu nchini na kuuza kwa bei ghali katika mataifa ya nje jambo ambalo litainua maisha ya mkulima wa kawaida,”akasema.

Ambapo malengo yake kufikia sasa na kutengeneza unga unaoweza kutokana na uyoga ,utakaotumika kutengeneza uji na vinywaji vinginevyo vyenye afya mbali na kustawisha kiwanda cha kwanza.

You can share this post!

Kazi bado ngumu kwa Harambee Stars baada ya sare na Togo

UBUNIFU: Taa za koroboi ndizo zilimsomesha na kwa sasa...

adminleo