Makala

UBUNIFU: Taa za koroboi ndizo zilimsomesha na kwa sasa zinamwezesha kutupa tonge kinywani

November 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na HASSAN POJJO

WAKATI Kitsao Charo “Katunguu” alijiunga na kidato cha kwanza mwaka wa 2003, alikuwa na mawazo ya jinsi familia yake ilivyokuwa ikimtegemea kuiongoza kutoka maisha ya umaskini, akiahidi angewajibikia ‘jukumu’ hilo.

Hali hiyo ilimshinikiza kufanya vibarua mbalimbali kila akifunga shule ili kukidhi mahitaji yake pindi shule ya kwao nyumbani inapofunguliwa akiwa ni kijana mwenye umri wa miaka 19 pekee.

Anasema alianza kung’amua hali halisi ya familia yao kuwa ikiwa kupata elimu, chakula na mavazi ilikuwa shida, hivyo akatia bidii katika masomo, angeishia kuilaumu nafsi yake na kuzidi kuididimiza familia yake ndani ya shimo la umaskini mkuu usio na matumaini.

Charo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 35 na ambaye ni mzaliwa wa kaunti ya Kilifi anatafuta riziki katika kaunti jirani ya Mombasa ambapo anachochewa na msemo usemao ‘riziki ni popote’.

“Ni baada ya kumaliza kidato cha nne katika shule ya upili ya Ngala Memorial ndipo nilipoamua kusaka vibarua katika miji mbali mbali ya ukanda wa Pwani bila mafanikio. Nililazimika kuendeleza biashara iliyokuwa ikinipa pesa za kujilipia karo shuleni ya utengenezaji wa Taa za Koroboi”, asema Charo.

Charo anasema kuwa Taa za Koroboi zimeanza kupoteza umaarufu katika maeneo mengi ya nchi kutokana na kusambazwa kwa umeme mashinani kwani awali alikuwa akipayta pesa nzuri akitaja kuvuna hadi kiasi cha shilingi 900-1000 kwa siku wakati huo.

Aidha, anasema kuwa kwa sasa anaweza kupata kima cha shilingi 500-700 kwa siku japo inamlazimu kusafiri mwendo mrefu hadi mashambani ambako bado taa hizo zinatumiwa kwa wingi.

Anasema kuwa zamani alikuwa akipata shilingi 30,000 tofauti na sasa ambapo hupata kati ya elfu 15,000 na 21,000 kwa mwezi, hali anayoitaja kuwa inafifisha matumaini ya wale wanaojituma kutafuta riziki bila kuajiriwa.

Alikuwa analenga kuweka msingi thabiti wa maisha kwa wazazi wake wakati alipokuwa akifunga shule na kuenda kutengeza taa hizo na alikuwa na uwezo wa kupita mitihani.

Taa za Koroboi ambazo alikuwa akitengeza zilimpa kipato cha kusaidia wazazi wake na kumlipia karo kidogo hadi akakamilisha masomo yake shuleni hapo.

Charo hata hivyo amewataka vijana kutumia ujuzi walionao badala ya kukaa na kungoja kazi za kuajiriwa kwenye kampuni kubwa kubwa nchini.

“Vijana lazima tujipe shuguli za kufanya. Haijalishi umesoma kiwango kipi. Tufanyeni kazi yoyote mradi mwisho wa siku mkono uelekee kinywani. Kazi zimekuwa haba ikizingatiwa kwamba ukanda wa Pwani viwanda vingi vimefungwa,” asema Charo.