Nani yuko salama na nani anakaribia kuaga mbio za kufika Afcon 2021 kutoka eneo la Cecafa baada ya mechi mbili za kwanza
Na GEOFFREY ANENE
MATAIFA manane kutoka eneo la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) yanashiriki mechi za makundi za kutafuta tiketi ya kuwa nchini Cameroon mwaka 2021 kwa makala ya 33 ya Kombe la Afrika (AFCON).
Ukumbi huu unamulika jinsi mataifa hayo – Uganda, Kenya, Sudan, Rwanda, Tanzania, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini – yalivyofungua kampeni zao na kuelezea nani yuko salama na nani anakaribia kubanduliwa nje. Nchi za Eritrea na Somalia hazikushiriki mashindano haya nayo Djibouti iliondolewa na Gambia katika mechi ya kuingia makundi.
Kundi B
Uganda ni nambari moja katika eneo la Cecafa kwa kuwa inashikilia nafasi ya juu kutoka eneo hili kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) katika nafasi ya 79. Inaongoza Kundi B kwa pamoja na Burkina Faso kwa alama nne baada ya kukaba nambari 60 duniani Burkina Faso 0-0 mnamo Novemba 13 na kisha kuzaba Malawi inayoshikilia nafasi ya 124 duniani mnamo Novemba 17 kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Emmanuel Okwi na Fahad Bayo. Malawi ni ya tatu kwa alama tatu nayo nambari 162 duniani Sudan Kusini inavuta mkia bila alama baada ya kulimwa na Malawi 1-0 na Burkina Faso 2-1. Cranes ya Uganda itaalika majirani Sudan Kusini katika mechi yake ijayo mnamo Agosti 31 mwaka 2020, siku ambayo pia Burkina Faso itakuwa mwenyeji wa Malawi.
Waganda, ambao watazuru Sudan Kusini mnamo Septemba 8, wanafukuzia tiketi ya kushiriki Afcon kwa mara ya tatu mfululizo. Walirejea katika mashindano haya mwaka 2017 walipomaliza ukame wa miaka 39. Sudan Kusini haijawahi kushiriki Afcon.
Kundi C
Nambari 128 duniani Sudan ililipua Sao Tome & Principe inayokamata nafasi ya 180 kwa magoli 4-0 mnamo Novemba 13 na kuchukua uongozi wa kundi hili. Hata hivyo, baada ya kupepetwa 1-0 na Afrika Kusini hapo Novemba 17, Sudan sasa imetupwa nje ya nafasi mbili za kwanza za kuingia Afcon 2021. Wasudan wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama tatu, sawa na nambari mbili Afrika Kusini inayojivunia rekodi nzuri ya ana kwa ana. Ghana inashikilia nafasi ya 51 duniani. Imejiweka pazuri kuwa nchini Cameroon mwaka 2021 baada ya kulipua nambari 72 duniani Afrika Kusini 2-0 (Novemba 14) na Sao Tome & Principe 1-0 (Novemba 18). Kichapo dhidi ya Afrika Kusini kimeweka Sudan mashakani kwa sababu mechi zake mbili zijazo ni dhidi ya Ghana, ambazo itakuwa na ulazima wa kushinda la sivyo ikose makala matano mfululizo ya Afcon.
Kundi E
Baada ya kushiriki Kombe la Afrika kwa mara ya kwanza kabisa nchini Misri mwaka 2019, Burundi inaonekana iko katika hatari kubwa ya kuwa shabiki mwaka 2021. Ilianza kampeni yake ya kufika Cameroon kwa kuzabwa 2-0 na Jamhuri ya Afrika ya Kati kabla ya kuzimwa 3-0 na Morocco mnamo Novemba 19. Morocco na Mauritania wanashikilia nafasi mbili za kwanza kwa alama nne kila mmoja. Majirani hawa walitoka 0-0 mnamo Novemba 15. Mauritania ilizoa alama tatu siku ya Jumanne ilipobwaga Jamhuri ya Afrika ya Kati 2-0. Jamhuri ya Afrika ya Kati ni ya tatu kwa alama tatu nayo Burundi haina alama. Morocco, Mauritania, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Burundi zinashikilia nafasi za 42, 105, 112 na 143 duniani, mtawalia.
Kundi F
Rwanda pia imeona giza katika mechi zake mbili za ufunguzi kwenye kundi hili baada ya kuchabangwa 2-0 na Msumbiji na 1-0 dhidi ya mabingwa wa zamani Cameroon. Matumaini ya Rwanda kurejea katika Afcon kutoka kundi hili tayari yanaonekana kuwa finyu kwa sababu timu moja ndiyo itafuzu kuungana na Cameroon iliyojikatia tiketi kwa kuwa ni mwenyeji. Nambari 112 duniani Msumbiji inaongoza kundi hili kwa alama nne ilizovuna kwa kupepeta Rwanda 2-0 Novemba 14 na kisha kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Cape Verde inayopatikana katika nafasi ya 77 duniani. Cameroon (nambari 52 duniani) ni ya pili katika kundi hili kwa alama nne nayo Cape Verde iko alama mbili nyuma katika nafasi ya tatu.
Kundi G
Kenya, ambayo inashikilia nafasi ya 108 duniani, inapatikana katika kundi hili. Harambee Stars ya kocha Francis Kimanzi ilianza kampeni vyema ilipokaba nambari 49 duniani Misri 1-1 mnamo Novemba 14 mjini Alexandria. Hata hivyo, ilipata pigo ilipokubali nambari 124 duniani Togo kuikaba 1-1 uwanjani Kasarani mnamo Novemba 18. Sare hizo mbili zinaweka mabingwa hawa wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Senior Challenge) pabaya. Vijana wa Kimanzi lazima wapate ushindi katika mechi zao mbili zijazo dhidi ya Comoros, ambayo imeonyesha dalili za mapema itahangaisha wapinzani katika kundi hili. Wanavisiwa wa Comoros wamekalia juu ya kundi hili kwa alama nne. Comoros, ambayo ni nambari 142 duniani, ililima Togo 1-0 jijini Lome na kutoka 0-0 dhidi ya Misri ilipoalika miamba hao wa Afrika. Kenya na Misri zimezoa alama mbili kila moja, huku Togo ikivuta mkia kwa alama moja. Stars ilishiriki makala ya Afcon yaliyopita nchini Misri ambako iliondolewa katika mechi za makundi baada ya kulazwa na Algeria na Senegal na kuliza Tanzania. Comoros haijawahi kushiriki Afcon nayo Togo inalenga kurejea katika jukwaa la Afrika baada ya kukosa tiketi ya mwaka 2019.
Kundi J
Tanzania, ambayo ilirejea katika Afcon mwaka 2019 baada ya kuwa nje miaka 39, ilianza kampeni za kushiriki makala mawili mfululizo vyema. Ilichapa Equatorial Guinea 2-1 Novemba 15 kabla ya kukubali kipigo cha dozi sawa na hiyo kutoka kwa Libya katika mechi yake ya pili. Nambari 29 duniani Tunisia tayari imeanza kubisha hodi kuingia Afcon kutoka kundi hili baada ya kulipua Libya 4-1 na Equatorial Guinea 1-0. Libya na Tanzania, ambazo ziko katika nafasi za 103 na 133 duniani mtawalia, zinafuata Tunisia kwa alama tatu kila mmoja. Equatorial Guinea iko mkiani bila alama. Tanzania italazimika kufanya kazi ya ziada katika mechi zake mbiliz zijazo dhidi ya Tunisia ili kusalia katika mbio za kuingia Afcon 2021.
Kundi K
Timu ya mwisho kutoka Cecafa inayowania tiketi ya kuwa nchini Cameroon mwaka 2021 ni Ethiopia. Waethiopia walifufua kampeni yao waliposhangaza mabingwa wa mwaka 1992 na 2015 Ivory Coast 2-1 mjini Bahir Dar mnamo Novemba 19. Walia ibex, jinsi timu ya Ethiopia inafahamika kwa jina la utani, ilianza kampeni yake kwa mguu mbaya ilipozamishwa 1-0 na Madagascar mnamo Novemba 16 jijini Antananarivo. Madagascar, ambayo ilishiriki Afcon kwa mara ya kwanza mwezi Juni/Julai mwaka huu, imeanza kunusia kufika Cameroon baada pia kupepeta Niger 6-2 jijini Niamey mnamo Novemba 19.
Ethiopia sasa inaonekana imejiweka pazuri kwa sababu itakutana na Niger katika mechi zake mbili zijazo wakati Madagascar itapimwa vilivyo makala yake na Ivory Coast. Ivory Coast inashikilia nafasi ya 56 duniani nayo Madagascar ni nambari 95 duniani, Niger (107) na Ethiopia (151). Mabingwa wa mwaka 1962 Ethiopia walikuwa katika Afcon mara ya mwisho mwaka 2013. Ivory Coast imeshiriki makala manane yaliyopita. Niger ilikuwa Afcon mara ya mwisho mwaka 2013.
Timu zitakazokamilisha makundi 12 ya kufuzu kushiriki Afcon 2021 katika nafasi mbili za kwanza (isipokuwa kundi la Cameroon) zitajikatia tiketi. Mabingwa Algeria pamoja na Senegal na Nigeria, ambao walimaliza makala yaliyopita katika nafasi ya pili na tatu mtawalia, wameshinda mechi zao mbili za kwanza kwenye makundi H, I na L kwa hivyo wako katika nafasi nzuri ya kunogesha makala yajayo.