Makala

Madampo yanavyogeuzwa 'mazalio' ya mbu na kuwa kero

November 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

UTUPAJI holela wa taka katika baadhi ya mitaa Kaunti ya Kiambu na Nairobi umekuwa mojawapo ya changamoto zinazozingira wakazi, suala hilo likihusishwa na uchafuzi wa mazingira.

Ukizuru mitaa kama vile Githurai, Mumbi, Progessive na Toezz iliyoko Kaunti ya Kiambu, na Mwiki, Zimmerman, Kariobangi, Kayole na Mathare, miongoni mwa mingine, hutakosa kutazama baadhi ya maeneo yenye taka zinazotoa uvundo.

Licha ya serikali za kaunti kupaswa kuwajibikia, hali hiyo inaendelea kuwa tete. Katika kaunti hizo mbili; Nairobi na Kiambu, idadi ya watu ni kubwa, hivyo basi majengo ya kuishi ni mengi na yanapatikana katika mazingira yayo hayo.

Ili kuzoa taka, serikali za kaunti hutoa tenda kwa mashirika ya binafsi na ambayo yanapaswa kutekeleza jukumu hilo kikamilifu.

Hata hivyo, yanahitaji kushirikiana kwa karibu na wamiliki wa nyumba za kupangisha almaarufu landilodi.

Kila mwezi, wapangaji hutozwa kodi fulani ya shughuli hiyo shabaha ikiwa taka zikusanywe ili zisitapakae.

Katika mtaa wa Githurai, mambo yanaendelea kuwa segem nege kwa kinachotajwa kama utupaji wa taka kiholela. Baadhi ya wakazi wanalalamika kwamba taka kwenye majaa, zimekuwa makazi ya mbu – mdudu hatari na anayeaminika kuambukiza na kuendeza ugonjwa wa Malaria.

“Baada ya taka kama vile chupa za plastiki, mikebe na mifuko ya nailoni kukusanywa, wanarundika katika sehemu moja. Ndio, tunaelewa ‘bidhaa’ hizo zinahifadhiwa kwa manufaa mengine kama vile kuzitumia tena, lakini sasa zimekuwa kero kwa sababu zimegeuka kuwa makazi ya mbu,” mwenyeji mmoja akaambia Taifa Leo.

Kulingana na mkazi huyo aliyeomba tusichapishe jina lake, eneo la Reli analoishi, limesheheni taka hizo ambapo usiku mbu wanahangaisha watu. Taswira ni ile ile mtaani Mumbi, Progressive, Zimmerman na hata Mwiki.

Hata hivyo, katika mitaa iyo hiyo kuna maeneo chache yanayojali usafi wa mazingira.

“Ni jukumu letu kama wakazi na malandilodi kuhakikisha taka zinakusanywa na kupelekwa zinakofaa, ila si kuzitupa kiholela,” Eunice Wanjiku, anayeishi eneo la Carwsh, pembezoni mwa Thika Superhighway akasema.

Mama huyo ambaye pia ni mpangaji, anapendekeza malandilodi wenza kuweka sheria kali katika uhifadhi wa mazingira.

“Kila mpangaji anapaswa kutoa ada ya kukusanya taka, halafu zipelekwe zinakofaa,” anahimiza.

Halmashauri ya kitaifa ya mazingira, Nema, kwa ushirikiana na idara husika hasa mazingira chini ya serikali ya kaunti na ile kuu, wanapaswa kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha mazingira ni salama.

Ni muhimu kukumbusha asasi hizo kuwa utupaji wa taka kivoloya ni kiini cha maradhi mbalimbali kama vile Homa ya Matumbo na Kipindupindu. Taka zizo hizo ndizo huziba mitaro ya majitaka. Kimsingi, mazingira chafu si salama kwa binadamu.