UKULIMA: Pilipili mboga za rangi mbalimbali
Na SAMMY WAWERU
PILIPILI mboga ni miongoni mwa viungo vinavyotumika katika mapishi ili kuongeza ladha kwenye mlo.
Kwa Kiingereza capsicum pia sweet pepper, kiungo hicho kinapatikana kwa aina tatu ya rangi. Kuna pilipili za kijani, nyekundu na manjano.
Zinaweza kukuzwa eneo tambare na kwenye vivungulio pia mahema, maarufu kama greenhouse.
Kulingana na Emmah Wanjiru, mtaalamu, ukuzaji wa zao hilo kwenye mahema ndiyo bora zaidi. Mjuzi huyo wa masuala ya kilimo anasema hema hupunguza changamoto nyingi zinazoandama pilipili mboga.
“Usambaaji wa wadudu na magonjwa hudhibitiwa kwa kufanya kilimo kupitia vifungulio,” aeleza. Eneo tambarare, wadudu huhama kutoka shamba moja hadi lingine, nayo magonjwa yakichangiwa kusambaa na upepo.
Bacterial wilt ndio ugonjwa sugu kwa pilipili mboga. Magonjwa mengine ni; powdery mildew, damping-off, root rot, bacterial spot, fusarium wilt na downy mildew.
Wadudu wanaoshambulia zao hilo ni vidukari, sota (cutworm), fukusi aina ya pepper, maggots na flea beetles.
Pia, ni muhimu kujua kwamba kilimo cha hema wanaoingia humo sharti wawe na idhini ya mkulima mmiliki.
Greenhouse hutengenezwa kwa chandarua maalum au karatasi ngumu za nailoni, hasa kuezeka paa.
Kandokando, chandarua kinachotumika kinapaswa kuwa na mashimo madogo ya kuruhusu hewa ya Oxijeni kuingia na inayotolewa na mimea kutoka. Kinasimamishwa kwa miti au vyuma.
Aidha, kina mahali pa kuingilia, mlango. Wengi wa wakulima wamekumbatia mfumo wa unyunyiziaji maji kwa mifereji, inayosindikwa ardhini hususan katika shina la mimea.
Mtaalamu Emmah Wanjiru anasema pilipili mboga zinahitaji udongo wenye rutuba ya kutosha pamoja na uchachu (pH) wa kati ya 6.0 – 6.5. Anaonya kwamba usiwe unaotuamisha maji.
Maeneo yanayolengwa yawe na kiwango cha joto, nyuzijoto 15 – 25 kipimo cha sentigredi. Pilipili zinastawi maeneo yaliyo mita 2000, juu ya ufuo wa bahari.
“Pilipili hizo zinaweza kupandwa kupitia mbegu au miche, japo miche ndiyo bora,” asema Wanjiru, akiongeza kwamba miche yake huchukua muda wa siku 45 kitaluni.
Hektari moja inasitiri takriban miche 10, 000 ikipandwa kwa kimo cha sentimita 75 (nafasi kati ya laini ya mashimo) kwa 45 (mche hadi mche).
Kulingana na mtaalamu huyo, upanzi wake hauna ugumu wowote kwani unawiana na ule wa nyanya.
“Muhimu ni kutunza mipilipili kwa mbolea, fatalaiza na maji,” anaeleza Bi Wanjiru.
Anaongeza: “Chaguo la kuikuzia kwenye hema pia inaepusha mimea hiyo kuvunjwa na upepo, kando na changamoto za magonjwa na wadudu.”
Mipilipili ikirefuka, husimamishwa kwa fito na nyuzi.
Mbuvi Mulinge ni mkulima wa piliplili mboga katika kaunti ya Kajiado, na anasema huanza kuvunwa miezi mitatu baada ya upanzi.
“Zao hilo likiwa changa ni kijani, likikomaa huanza kubadili rangi kwa mujibu wa mbegu zake; kijani, nyekundu, manjano na pia zambarau,” anaeleza Bw Mulinge. Hata hivyo, pilipili ya zambarau ni nadra kupatikana hapa nchini.
Aidha, pilipili mboga zinafunwa kwa muda wa kati ya miezi 8 hadi 10 mfululizo.
Mpilipili mboga una uwezo wa kuzalisha kati ya matunda 15 – 25, moja ikiuzwa Sh5 au 10. Gharama ya kuzalisha hektari moja inakadiriwa kuwa karibu Sh150, 000.