MWITHIGA WA NGUGI: Hii ni hujuma serikali kuzitelekeza shule za umma
Na MWITHIGA WA NGUGI
SHULE za umma kwa muda mrefu zimekuwa ndilo kimbilio la wanyonge ambapo wengi wanaamini kulingana na uwezo wao ndipo mahala pa kujipatia elimu angalau kwa kiwango nafuu kulingana na mapato yao.
Lakini kizungumkuti cha mambo ni kuwa, shule nyingi za umma ziwe ni za msingi au za upili kwa miaka mingi zimekuwa kama vinyago iwapo si mahame yasiyokuwa na hadhi ya kuigwa mahala popote duniani.
Si mara moja au mbili, tumeona kwenye vyombo vya habari picha za watoto wakisomea chini ya miti, huku viti vyao vikiwa ni mawe sugu ya porini.
Hakuna haja ya kupoteza muda kuandikia mate ilhali wino upo, ukweli sharti usemwe na kuandikwa.
Wazazi wengi nchini wameshindwa kuvumilia kuendelea kuwasomeshea watoto wao katika shule za umma kutokana na hali ya kudorora kwa elimu katika shule hizo, na kwa bahati mbaya wengine wanawapeleka kwenye shule za kibinafsi, zisizokuwa na miundo mbinu faafu ambayo hivi majuzi miongoni mwayo tumeona ikifungwa na mingine vilevile ikisababisha maafa kwa watoto wetu.
Ni wazi kwamba hata wakati wa mwanzilishi wa taifa letu, serikali yake ililenga kuufukuza ujinga kupitia elimu kwa wananchi wake, jambo ambalo hadi wa leo linastahili kupewa kipaumbele na viongozi wa sasa.
Hatufai kuona Kenya ikigawanyika kwa misingi ya kitabaka, eti ukienda Garba Tulla au Moyale shule za umma taswira unayopata ni madongoporomoka kwa jina la shule za umma.
Ama kweli, tutatarajia matokeo ya aina gani baada ya mitihani ya kitaifa iwapo kuna wanafunzi ambao hawajawahi kuona kuta za darasa na wengine wenye hata kupata mwalimu wa kuwafundishia chini ya mti ni kitendawili?
Huu si wakati wa kuchezea elimu ya watoto wetu na lazima serikali iweze kuusawazisha uga wa elimu yao.
Hatufai kusahau kwamba, kizazi cha sasa ndicho tegemeo la taifa letu la kesho, na tusipowapa msingi bora wa kielimu basi tutakuwa tumefeli kabisa kama taifa.
Kwa wanasiasa wetu huu ndio wakati wa kubuni sera za kuzinusuru shule zetu za umma.
Kwa wafanyakazi wote wa umma ikiwemo kuanzia wabunge hadi wawakilishi wa wadi, twafaa kuwa na sheria kuwa lazima watoto wao kwa lazima wawasomeshee katika shule za umma.
Hili likifanyika kila mara wao watakuwa wa kwanza kushughulikia matatizo na changamoto zinazozikumba shule hizi.
Na si hivyo tu, ikiwezekana washurutishwe pia kutumia hospitali za umma na wala wasipewe mwanya wa kutumia hospitali za kibinafsi wala za ughaibuni.
Kwa kufanya hivyo, itakuwa ni afueni kwa mlalahoi ambaye hatimaye atapata huduma bora za elimu na za afya.