WALIBORA: Ufumbuzi wa Kiafrika kwa Matatizo ya Afrika
Na KEN WALIBORA
KUDIDIMIA kwa utashi wa bidhaa za Afrika nchini Marekani, Ulaya na kwingineko kumechochea ari ya nchi za Kiafrika kufanya biashara zenyewe kwa zenyewe.
Tokeo la ari hii ni kuundwa kwa Mwafaka wa Soko Huria Barani, yaani Afrika African Continental Free Trade Area (AfCFTA).
Kwa kweli bara hili litapata hasara kubwa sana endapo litaendelea kutegemea masoko ya nje ya mipaka yake ili kuwa na maendeleo endelevu.
Yamkini sasa Afrika imebaini kwamba ipo haja kuchukua hatua mwafaka kulipatia ufumbuzi suala hili, ufumbuzi wa Kiafrika kwa matatizo ya Afrika.
Jiji kuu la Ethiopia, Addis Ababa mnamo Novemba 26 hadi 27, 2019, litakuwa mwenyewe au mwenyeji wa mazungumzo kuhusu utekelezaji wa Mwafaka wa Soko Huru Afrika.
Kongomano hilo litawajumuisha wadau toka asasi za serikali na zisizo za serikali pamoja na wafanya biashara kote barani kujadili utekelezaji. Wajumbe hao 70 watapata fursa nzuri ya kuelewa na kupanga mikakati ya utekelezaji wa mwafaka huo wa kurahisisha biashara baina ya mataifa ya Kiafrika kwa kuondoa vikwazo zisivyokuwa na tija.
Mataifa ya Afrika yameng’amua kwamba wale waitwao washirika wa kimaendeleo kutoka mataifa yaliyoendelea, huenda hawataka hasa kwa dhati Afrika iendelee bali ibakie nyuma sikuzote.
Ni dhahiri kwamba kwa sasa mataifa haya ya Kiafrika yameazimia kujikwamua yenyewe kwa kufanya biashara yenyewe kwa yenyewe ili kuepuka kurubuniwa na wanafiki wa dunia.
Kubuniwa kwa Mwafaka wa Soko Huru Afrika mnamo Mei 2019 ni matokeo ya juhudi za pamoja za miongo mingi zenye lengo la kutangaminisha biashara kote barani Afrika ili kuliwezesha kushindana vilivyo na mabara mengine.
Ni muhimu kutambua hamasa ya mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAM) kushiriki katika biashara ya wao wao. Taarifa ya sekretarieti ya JAM ya 2018 inataja kwamba biashara baina ya nchi za Afrika Mashariki iliongezeka kutoka dola bilioni 5.98 mwaka 2018 toka dola bilioni 5.46 mwaka uliotangulia wa 2017.
Isitoshe, tukio la kihistoria la kutia saini mkataba wa AfCFTA kulikotekelezwa na mataifa 44 kutoka jumla ya 55 barani Afrika, lilitokea kwenye jiji la Kigali, Rwanda katika eneo la Afrika Mashariki.
Aidha mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kenya ikiwemo, yalikuwa miongoni mwa yale ya kwanza kabisa kuidhinisha mwafaka huo.
Hapana shaka kubuniwa kwa Mwafaka wa Soko Huru Barani Afrika kunaendena na mawanio ya waasisi wa mataifa ya Afrika kama vile Kenneth Kaunda, Kwame Nkrumah, Jomo Kenyatta na Julius Kambarage Nyerere.
Afrika haiwezi kuendelea kuwa mtegemezi wa washirika wanafiki katika harakati zake za biashara. Inapaswa kupanga mikakati ya kujitegemea kwa kufanya biashara ndani na baina ya mataifa yake kuwa rahisi. Vinginevyo, Afrika itajikuta inadidimia tena kwenye lindi la ukoloni mpya huku iking’ang’aniwa tena kama mpira wa kona kutokana na rasilmali zake!