• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Fainali ya wanawake ya Cecafa kukutanisha Kenya na Tanzania

Fainali ya wanawake ya Cecafa kukutanisha Kenya na Tanzania

Na GEOFFREY ANENE

KENYA na Tanzania zitafufua uhasama wao kwenye mashindano ya soka ya wanawake ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) wakati Harambee Starlets itavaana na Kilimanjaro Queens katika fainali jijini Dar es Salaam mnamo Novemba 25.

Starlets ilitangulia kuingia fainali baada ya kupapura Burundi 5-0 katika nusu-fainali ya kwanza kupitia mabao ya Jentrix Shikangwa yaliyopatikana dakika ya 54 na 72, nahodha Dorcas Shikobe (14), Mwanahalima Adam (67) na Corazone Aquino (78).

Mabingwa wa makala mawili yaliyopita Tanzania kisha wakaungana na Kenya baada ya kushinda nusu-fainali ya pili japo kwa jasho 1-0 dhidi ya Uganda.

Nahodha wa Tanzania Asha Rashid alifunga bao la ushindi sekunde chache kabla ya kipenga cha mwisho kupulizwa.

Kenya na Tanzania zilikutana katika fainali ya mwaka 2016 nchini Uganda ambayo Watanzania waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Timu hizi zilikutana tena katika makala yaliyopita nchini Rwanda ambapo zilitoka 1-1 katika mashindano hayo yaliyochezwa kwa mfumo wa mzunguko baada ya kuvutia timu tano pekee.

You can share this post!

Rais Kenyatta aagiza timu za uokozi KDF na idara ya polisi...

Tundo moto balaa KCB Edoret Rally

adminleo