• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Hofu Bandari kwa matokeo duni, sasa waita mkutano

Hofu Bandari kwa matokeo duni, sasa waita mkutano

Na ABDULRAHMAN SHERIFF na GEOFFREY ANENE

KOCHA wa Bandari FC, Bernard Mwalala anapanga kuitisha mkutano wa dharura wa wachezaji, maafisa wa benchi la ufundi na viongozi wa klabu hiyo kujadili tatizo linalokabili timu hiyo ambayo imeshinda mechi moja pekee kutoka 10 zilizopita.

Katika mahojiano baada ya Bandari kuchapwa 2-0 na viongozi wa Ligi Kuu, Gor Mahia, katika uwanja wa Mbaraki mnamo Jumapili, Mwalala alisema lengo la mkutano huo ni kutafuta suluhisho.

“Hivi sasa ni mechi nne mfululizo hatujapata ushindi ligini. Kuna tatizo ambalo tunastahili kukaa chini na viongozi ili tulitatue,” alisema bila kufafanua tatizo lenyewe.

Alifichua kuwa baada ya mapumziko timu ilipobanduliwa nje ya mashindano ya Kombe la Mashirikisho la Afrika (CAF), aliwaandaa wachezaji wake akitarajia matokeo mazuri. Badala yake, hakuna matunda yoyote yaliyopatikana dhidi ya AFC Leopards na Gor Mahia.

“Mapumziko yalitusaidia, lakini ajabu ni kuwa hali ya uchezaji wa wanasoka wangu imerudi chini. Tuna mechi ngumu dhidi ya Tusker ugenini. Ninaamini tutakuwa tumepata suluhuhisho,” alisema kabla ya kufichua kutoridhishwa kwake na safu zote za ulinzi, kati na ushambuliji na pia wachezaji kucheza bila ya kuelewana.

Dhidi ya Bandari, Gor ya kocha Steven Polack ilipata mabao ya ushindi kupitia kwa Samuel Onyango dakika ya 45 na Francis Afriyie (48). Mshambuliaji wa Bandari, William Wadri alipoteza penalti.

Licha ya kuwa vijana wa Mwalala wanatapa wakati huu, Bandari wataalikwa na Tusker uwanjani Kenyatta mjini Machakos mnamo Desemba 1 wakijivunia rekodi nzuri ya ushindi mbili na sare moja dhidi ya wanamvinyo hao katika mechi tatu zilizopita.

Bandari pia itaingia mchuano huo na motisha ya kuzaba Tusker 3-1 zilipokutana mara ya mwisho mwezi Mei mwaka huu. Baada ya kukamilisha ligi ya msimu 2018-2019 katika nafasi ya pili nyuma ya Gor Mahia na hata wengi kutarajia itakuwa mgombeaji halisi wa taji msimu huu, Bandari imesikitisha msimu huu.

Mwalala na vijana wake walikuwa na maandalizi mema ya msimu huu walipozuru nchini Afrika Kusini na pia kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) kwa mara ya kwanza.

You can share this post!

Maseneta wamuunga Yatani kuzinyima fedha kaunti zenye...

CCM yajizolea asilimia kubwa ya viti uchaguzi wa mitaa...

adminleo