Bunge la kaunti ya Lamu lapitisha hoja wahudumu wote wa bodaboda kisiwani kuwa na leseni
Na KALUME KAZUNGU
BUNGE la Kaunti ya Lamu limepitisha hoja ya kuwataka wahudumu wote wa bodaboda kisiwani Lamu kuwa na leseni za kutekelezea shughuli zao.
Hoja hiyo iliyowasilishwa bungeni na Diwani Maalum, Amina Kale, pia inapendekeza mabango ya makadirio ya mwendo unaokubalika kutumiwa na wahudumu hao wa bodaboda kutundikwa kwenye steji zao na pia barabara na vichochoro wanavyopitia.
Kadhalika wahudumu wa bodaboda wanatakiwa kuhudumu kwenye maeneo maalum ya mji na wala si ndani ya mji huo wa kihistoria ambao ni kivutio kikuu cha watalii.
Hoja hiyo inajiri wakati ambapo kumekuwa na malalamishi ya muda mrefu kutoka kwa wakazi na watalii ambao wamekuwa wakishinikiza kuondolewa kwa wahudumu wa bodaboda ndani ya mji wa Lamu ulioorodheshwa na Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni (Unesco) mnamo 2001 kama sehemu mojawapo inayotambulika ulimwenguni kwa kuhifadhi tamaduni na ukale wake.
Wakati huo huo,Bunge la Kaunti ya Lamu limepitisha hoja nyingine ya kutaka kuchunguzwa kwa baadhi ya wafanya kazi walioajiriwa na Kaunti ya Lamu kwa madai kwamba uajiri wao si wa halali.
Hija hiyo iliwasilishwa bungeni na Mwakilishi wa Wadi ya Witu, Jonathan Baya Mketta.
Hoja hiyo pia inapendekeza fedha za bajeti ya ziada zilizotengwa kwa minajili ya kulipa mshahara wa wafanyakazi hao bandia kufutiliwa mbali.
Baadaye vikao vya Bunge la Lamu vilisitishwa rasmi kwa likizo ndefu na vitarejelewa tena Februari 10, 2020.