Michezo

Kenya juu nafasi mbili kwenye viwango vya ubora vya Fifa

November 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imepaa nafasi mbili hadi nambari 106 duniani katika viwango bora vipya vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ambavyo vimetangazwa Alhamisi.

Mechi zilizosakatwa kati ya Oktoba 20 na Novemba 24 zilitumiwa katika kuorodhesha mataifa 210 wanachama wa FIFA.

Katika kipindi hicho, Kenya ilikabana koo na miamba wa Afrika Misri pamoja na Togo katika mechi za Kundi G za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (Afcon) mwaka 2021.

Harambee Stars ilitoka 1-1 dhidi ya Misri iliyokuwa bila nyota wake Mohamed Salah, mjini Alexandria mnamo Novemba 14 na kuandikisha matokeo sawia dhidi ya Sparrowhawks ya Togo mnamo Novemba 18 jijini Nairobi.

Vijana wa kocha Francis Kimanzi waliingia katika mechi hizo mbili wakishikilia nafasi ya 108 duniani baada ya kuteremka nafasi moja katika viwango bora vya Oktoba 24 walipochapwa 1-0 na Msumbiji jijini Nairobi katika mechi ya kirafiki.

Hata hivyo, Kenya sasa imeruka juu kwa sababu wakati huo ilikutana na Wamisri waliokuwa katika nafasi ya 49 duniani nao Togo walishikilia nafasi ya 124.

Alama za Kenya kwenye orodha hiyo mpya pia zimeongezeka kutoka 1195 hadi 1199.

Misri, ambayo pia ilikabwa 0-0 dhidi ya Comoros katika mechi nyingine ya Kundi G, imeshuka nafasi mbili hadi nambari 51 duniani.

Togo pia imeteremka nafasi mbili baada ya kushangazwa na Comoros 1-0 jijini Lome katika mechi yake ya kufungua kampeni ya kuingia Afcon mwaka 2021.

Comoros, ambayo Kenya itaalika jijini Nairobi mnamo Agosti 31 na kulimana ugenini Septemba 8 katika mechi zake mbili zijazo za kuingia Afcon, imepiga hatua tisa mbele na kutulia katika nafasi ya 133.

Senegal ingali juu ya jedwali la Bara Afrika katika nafasi ya 20 duniani. Inafuatiwa na Tunisia, ambayo imepaa nafasi mbili hadi nambari 27, Nigeria (31 duniani kutoka 35), nao mabingwa wa Afrika Algeria wameimarika kutoka 38 hadi 35 duniani.

Morocco imeshuka nafasi moja. Inashikilia nafasi ya 43. Inafuatiwa na Ghana, ambayo ilichapa Afrika Kusini 2-0 katika mechi ya kuingia Afcon kutoka Kundi C na kuingia mduara wa 50-bora katika nafasi ya 47 duniani.

Cameroon, ambayo itakuwa mwenyeji wa Afcon 2021, imeshuka nafasi moja hadi nambari 53 duniani. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambayo imealikwa kushiriki mashindano ya Afrika na Kati (Cecafa Senior Challenge Cup) mwezi ujao nchini Uganda, imeshuka kutoka nafasi ya 54 hadi nambari 56. Iko bega kwa bega na Mali iliopanda nafasi tatu.

Burkina Faso ni ya 59 baada ya kupaa nafasi moja, nayo Ivory Coast imetupwa chini nafasi tano baada ya kuduwazwa na Ethiopia 2-1 mjini Bahir Dar.

Afrika Kusini inasalia katika nafasi ya 72 duniani. Uganda imekwamilia nafasi ya kwanza katika eneo la Cecafa na katika nafasi ya 77 duniani baada ya kuruka juu nafasi mbili.

Kenya inashikilia nafasi ya pili Cecafa katika nafasi ya 106 duniani kutoka 108, Sudan inasalia ya 128 duniani, Rwanda imeteremka nafasi mbili hadi nambari 131 nayo Tanzania imeshuka nafasi moja hadi nambari 134.

Ethiopia imeimarika kwa nafasi tano hadi nambari 146. Burundi imeporomoka nafasi nane hadi nambari 151 nayo Sudan Kusini ni ya 169 baada ya kusukumwa chini nafasi saba.

Djibouti imepaa nafasi mbili hadi 184 duniani, nayo Somalia imeruka juu nafasi mbili hadi nambari 196. Eritrea inasalia mkiani katika eneo la Cecafa. Haijaorodheshwa kwa sababu haijakuwa ikishiriki mashindano.

Hakuna mabadiliko katika nafasi tano za kwanza duniani zinazoshikiliwa na Ubelgiji, mabingwa wa duniani Ufaransa, washindi wa Copa America Brazil na Uruguay katika usanjari huo.

Croatia imepiga hatua moja mbele hadi nafasi ya sita baada ya kubadilishana nafasi hiyo na Ureno ya gunge Cristiano Ronaldo, ambayo imeshuka nafasi moja hadi nambari saba. Uhispania, Argentina ya Lionel Messi na Colombia zinakamilisha orodha ya mataifa 10-bora duniani, mtawalia.