Makala

RIZIKI: Haba na haba ya mapishi inamsukumia gurudumu la maisha

November 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

PEMBEZONI mwa barabara inayounganisha mtaa wa Mumbi na Mwihoko, Kaunti ya Kiambu, Muthoni Njeri ni mwenye shughuli chungu nzima kwenye hoteli yake.

Aliingilia uwekezaji huo miaka mitano iliyopita, baada ya kujaribu kazi mbalimbali bila mafanikio.

Njeri ambaye amesomea kozi ya masuala ya mapishi, anaiambia Taifa Leo kwamba alikuwa ameajiriwa kama mhudumu wa mkahawa mmoja jijini Nairobi. Anasema ilikuwa kazi ya kijungu jiko.

“Nilikuwa nikiingia kazini thenashara na kutoka ni usiku, saa tano. Isitoshe, mshahara ulikuwa kiduchu,” aeleza Njeri. Kulingana naye, alikata kauli kuiacha na kutafuta njia mbadala kusukuma gurudumu la maisha.

Mwaka 2013 alitafuta chumba eneo la Mumbi, katika barabara ya kuelekea Mwihoko, akaingilia shughuli za mapishi.

Ilimgharimu mtaji usiozidi Sh30, 000, ikiwa ni pamoja na vyombo vya mapishi, kodi na leseni kutoka kwa halmashauri ya kaunti na idara ya afya. “Kodi ni ya hoteli ni Sh4, 500 kila mwezi,” aeleza mjasirimali huyo.

Hata ingawa itangulizi haukuwa rahisi, Njeri anasema ukakamavu, bidii na ustahimilifu, ni hulka zilizomuwezesha kuimarisha biashara yake.

Huandaa chakula kama maharagwe kwa chapati, wali, ugali kwa nyama na kitoweo cha mboga. Njeri pia hupika ndengu, maharagwe asilia (minji), kunde, mukimo na kande almaarufu githeri. Vinywaji anavyoandaa ni chai na uji.

Bei ya mlo wake ni kati ya Sh40 – 100. Sababu hasa ya kuchagua pembezoni mwa barabara ya Mumbi – Mwihoko, ni kuhudumia watumizi wake (wa barabara) kama vile wahudumu wa matatu, tuktuk na pikipiki.

“Watumizi wa barabara hii ndio wateja wangu wengi,” Njeri ambaye ni mama wa mtoto mmoja akasema.

Wanaofanya shughuli za ujenzi eneo hilo hususan wa majengo pia ni wateja mfanyabiashara huyo.

Bi Muthoni Njeri, mmiliki wa hoteli eneo la Mumbi, Kaunti ya Kiambu. Picha/ Sammy Waweru

Michael Murimi mpishi katika mkahawa mmoja wa kifahari Nairobi anasema uwekezaji katika hoteli unapaswa kuzingatia maeneo na uwezo wa wakazi walioko katika mangizira yanayolengwa. Kwa mfano, eneo linalojikaza kukua kiuchumi kuwaandalia chakula ghali huenda muwekezaji akakosa kuafikia matakwa yake.

“Maeneo yanayovutia watalii mapochopocho wanayoandaliwa ni bei ghali, kinyume eneo lenye wafanyabiashara wa kadri na biashara ndogondogo,” aeleza Bw Murimi, kauli yake ikitiliwa mkazo na Muthoni Njeri.

Njeri pia anasema kiwango cha usafi kinapaswa kuwa cha hadhi ya juu. Hali kadhalika, wanavyopokelewa wateja, kuongeleshwa na kuwahudumia ni masuala muhimu kuzingatia.

“Lugha iwe ya heshima. Mapokezi na huduma ziwe za kuridhisha ili mteja arejee na mwenzake,” afafanua.

Anaongeza: “Nimeshuhudia baadhi ya hoteli zikifungwa, wateja kuhama kwa sababu ya kuwakosea heshima. Biashara ni kubembeleza mnunuzi.”

Hoteli ya Njeri imeimarika na kuendelea kunoga ambapo wafanyabiashara wenza na walio karibu huagiza chakula, mbali na wateja anaolenga.

Siku yake huanza saa moja na kutia nanga mwendo wa saa kumi na mbili za jioni. Ana mfanyakazi mmoja.

Aidha, Njeri pia hupokea mialiko ya nje ya mapishi maarufu kama ‘outside catering’, katika hafla kama vile harusi na utoaji wa mahari, miongoni mwa zingine.