• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Wazito yalipua Chemelil na kuweka rekodi ya ushindi mkubwa KPL

Wazito yalipua Chemelil na kuweka rekodi ya ushindi mkubwa KPL

Na GEOFFREY ANENE

WAZITO FC imeandikisha ushindi mkubwa kabisa kwenye Ligi Kuu ya msimu huu wa 2019-2020 baada ya kulipua Chemelil Sugar 6-0 uwanjani Kenyatta mjini Machakos, Jumamosi.

Vijana wa kocha Stewart Hall waliongoza 1-0 wakati wa mapumziko kupitia bao la mshambuliaji Elvis Rupia, ambaye alifuma wavuni penalti safi dakika ya 39.

Rupia aliongeza bao la pili dakika ya 47 baada ya kipa wa Chemelil kutema mpira. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Nzoia Sugar na klabu ya Power Dynamos nchini Zambia, alipata “hat-trick” yake dakika tatu baadaye baada ya kumegewa pasi murwa kutoka kwa Derrick Otanga.

Wazito, ambayo haikuwa imeshinda mechi tatu mfululizo, ilizidisha mashambulizi na kuongeza bao la nne kupitia Otanga aliyekamilisha kwa ustadi frikiki ya Ali Hassan dakika ya 73. Otanga alipumzishwa baada tu ya kupata bao hilo na nafasi yake kujazwa na Piston Mutamba.

Rupia alichangia krosi iliyozalisha bao la tano kutoka kwa Victor Ndinya dakika ya 81 kabla ya Mutamba kufunga ukurasa wa magoli dakia ya 87 kipa wa Chemelil alipotema shuti la Joe Waithira.

Kabla ya ushindi huu, mabingwa watetezi na viongozi Gor Mahia ndio walikuwa wamevuna ushindi mkubwa msimu huu walipopepeta Tusker 5-2 mnamo Agosti 31, huku Sofapaka na AFC Leopards zikizamisha Chemelil Sugar 4-0 mnamo Septemba 22 na Septemba 29, mtawalia.

Wazito sasa inashikilia nafasi ya 11 kwa alama 11 kutokana na mechi 11 nayo Chemelil inasalia mkiani kwa alama moja kutokana na idadi sawa ya mechi.

Mechi kati ya Kariobangi Sharks na KCB pia imeshuhudia mabao mengi. Sharks, ambayo iliwakilisha Kenya katika Kombe la Mashirikisho la Afrika mwaka 2018, imekamilisha mechi yake ya saba bila ushindi baada ya kucharazwa 5-2 uwanjani Kasarani.

AFC Leopards imetoka chini mara mbili na kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya wenyeji wake Nzoia Sugar mjini Mumias nayo Gor ikakabwa 0-0 dhidi ya Ulinzi Stars uwanjani Moi mjini Kisumu.

You can share this post!

Kabras Sugar yafanikiwa kuibwaga KCB katika raga wachezaji...

BBI: Mnara wa Babeli

adminleo