Starlets waingia mkondo wa pili kufuzu Kombe la Afrika
Na GEOFFREY ANENE
HARAMBEE Starlets ya Kenya, She-polopolo ya Zambia na Mighty Warriors ya Zimbabwe zimeingia raundi ya pili ya mashindano ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika la Wanawake mwaka 2018, Jumapili.
Starlets ilisonga mbele kutokana na bao ililofunga katika mechi ya mkondo wa kwanza ilipobwaga Crested Cranes ya Uganda 1-0 mjini Machakos mnamo Aprili 4.
Bao hili la beki Lilian Adero liliwezesha Kenya kujikatika tiketi ya kukutana na Equatorial Guinea katika raundi ya pili na mwisho mwezi Juni mwaka huu kwa sababu mechi ya marudiano jijini Kampala ilimalizika 0-0 Aprili 8.
She-polopolo, ambayo ilipepetwa 3-0 na Starlets katika mechi ya kujipima nguvu Machi 25, iliingia raundi ya pili baada ya kubandua nje Tanzania kwa mabao ya ugenini. Ilikaba Tanzania 3-3 jijini Dar es Salaam hapo Aprili 4 kabla ya kulazimishiwa sare ya 1-1 katika mechi ya marudiano uwanjani Nkoloma.
Rachael Kundananji aliweka Zambia bao 1-0 juu dakika ya kwanza kabla ya Tanzania kusawazisha 1-1 kupitia Mwanahamis Omar dakika ya 72.
Zimbabwe ilifuzu kwa jumla ya mabao 4-0. Ilizaba Brave Gladiators 2-0 jijini Windhoek hapo Aprili 5 kabla ya kuiongeza dozi sawia katika mechi ya marudiano jijini Harare, Jumapili. Zambia na Zimbabwe zitakutana katika raundi ijayo.
Washindi wa raundi ya pili wataingia Kombe la Afrika litakaloandaliwa nchini Ghana kutoka Novemba 17 hadi Desemba 1 mwaka 2018.
Matokeo (Aprili 8, 2018):
Uganda 0-0 Kenya
Zimbabwe 2-0 Namibia
Zambia 1-1 Tanzania