Mpango wa Meltah Kabiria kutetea taji msimu ujao
Na JOHN KIMWERE
TIMU ya Meltah Kabiria imefanya kweli baada ya kupambana mwanzo mwisho na kufaulu kutawazwa bingwa katika ngarambe ya Super Eight Premier League (S8PL) muhula huu.
Kabiria imeibuka timu ya pili kutoka Kanda ya Nairobi Magharibi kutwaa taji baada ya Kawangware United kulibeba mwaka 2016.
Kikosi hicho ambacho hunolewa na kocha, Urbanus Gichui kilitawazwa mabingwa wa kinyang’anyiro hicho baada ya kumaliza kileleni mwa jedwali kwa kukusanya alama 61, moja mbele ya Githurai Allstars.
Githurai, Jericho Allstars, Mathare Flames na TUK kila moja ilikuwa miongoni mwa vikosi vilivyopigiwa chapuo kutwaa taji hilo tangia mwanzo wa michuano hiyo.
Nao wanasoka wa TUK waliteleza na kufunga tatu bora kwa kuzoa alama 53, nne mbele ya Mathare Flames huku MASA kwa kuvuna pointi 51 ikimaliza ya tano.
Kwenye mechi za kukamilisha ratiba ya kipute hicho, Meltah ilifanikiwa kukomoa NYSA magoli 4-0 na kufikisha ushindi wa 19 kati ya mechi 30. Kwenye mechi hizo Meltah ilitoka nguvu sawa mara nne na kupoteza patashika saba.
”Kilichofanya tushinde taji la msimu huu si lingine bali ni uzoefu wa wachezaji wangu kucheza pamoja ndani ya miaka mitatu iliyopita,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa kwa sasa wanapania kujituma kisabuni kwenye juhudi za kutetea kombe hilo katika kampeni za muhula ujao.
Aidha alidokeza kuwa straika wake matata, Collins Omondi alichangia pakubwa ufanisi wa kikosi hicho kwa kuzingatia alikuwa mwiba kwa wapinzani wao.
Mchezaji huyo aliibuka mfungaji bora kwenye mechi hizo alipofanikiwa kutikisa wavu mara 19. Wengine waliochangia ushindi huo walikuwa Sammy Agesa, Wilson Muhoto (nahodha), Francis Wambura, Edward Njire bila kusahau Javan Mukoya.
”Hakika nashukuru wenzangu kwa kujikaza kwa udi na uvumba kwenye mechi za mkumbo wa pili na kufanikisha azimio letu la kubeba taji hilo baada ya kulipigania ndani ya miaka minne sasa,” nahodha huyo alisema na kuwataka wafuasi wao waendelea kuwasapoti kwenye kampeni za mchezo huo miaka ijayo.
Jericho Allstars iliyokuwa mabingwa watetezi iliteleza na kumaliza katika nafasi ya sita kwa kukusanya alama 50. ”Natoa mwito kwa wahisani wajitokeze kutupiga jeki kwenye shughuli zetu za kukuza talanta za wachezaji chipukizi mashinani,” mshirikishi wa michezo hiyo, Athanas ‘Obango’ Obala alisema.
Melta Kabiria inayopatikana katika eneo la Kawangware inajumuisha wachezaji kama: Francis Wambura, Joseph Omassaba, Lewis Mungai, Wilfred Thande, Collins Omondi, Javan Mukoya, Wilson Muhoto (nahodha), Edward Njire, Sammy Egessa, Evans Irungu, Shadrack Maina na John Ng’ang’a kati ya wengine.