• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
Shaurimoyo kushiriki S8PL msimu ujao

Shaurimoyo kushiriki S8PL msimu ujao

Na JOHN KIMWERE

HATIMAYE Shaurimoyo Blue Stars imefuzu kupandishwa ngazi kurejea kushiriki kampeni za kipute cha Super Eight Premier League (S8PL) baada ya kuteremshwa ngazi msimu uliyopita.

Kikosi hicho kimepandishwa daraja baada ya kumaliza nafasi ya nne kwenye jedwali la mechi za Super Eight Daraja la Kwanza na nafasi ya pili kwenye msimamo wa timu za Kanda ya Nairobi East.

Shaurimoyo Blue Stars iliibuka ya nne kwa kuzoa alama 47, baada ya kushinda mechi 13 kutoka nguvu sawa mara nane na kupoteza patashika saba.

Katika Kanda hiyo Shaurimoyo Blue Stars imepandishwa pamoja na Kayole Asubuhi iliyoibuka ya tano kwenye msimamo huo kwa alama 44 sawa na Wenyeji United tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Timu zingine ambazo zimepandishwa ngazi ni Leads United na Deportivo Rongai za Kanda ya Nairobi West zilizomaliza katika nafasi mbili za kwanza kwa alama 64 na 59 mtawalia.

”Nimejaa furaha tele hatimaye tumefuzu kupanda ngazi baada ya kupigana kwa udi na uvumba msimu huu,” kocha wa Shauri Moyo, Ken Odera alisema na kupongeza vijana wake kwa kazi njema waliofanya kwenye michuano ya muhula huu.

Baadhi ya wachezaji wa Wenyeji United walioshiriki kipute hicho. Picha/ John Kimwere

Hata hivyo alikiri kuwa mbio za kinyang’anyiro hicho zilishuhudia ushindani wa kufa mtu na kamwe haikuwa mteremko.

Kadhalika alisema alijaribu sana kusukuma kikosi hicho baada ya kutokuwa nacho msimu uliyopita ambapo kiliteleza na kuteremshwa ngazi kutoka mechi za Super Eight Premier League (S8PL).

Wanasoka wawili wa kikosi hicho walibahatika kunasa tuzo baada ya kufanya kweli kwenye mechi za muhula huu. Rahim Malik aliibuka mfungaji bora baada ya kutikisa wavu mara 11 naye nahodha wake Erick Kyalo alitwaa tuzo ya mchezaji bora.

Kocha huyo alisema baada ya kupata ufanisi huo kwenye mechi za kipute cha juu wamepania kujituma kadiri ya uwezo wao kuhakikisha hawatateremshwa ngazi tena.

Hata hivyo alisema kabla ya kipute hicho kung’oa nanga watalazimika kusaka huduma za wachezaji wapya ili kukiongeza kikosi hicho nguvu kukabili wapinzani wao kwenye michezo hiyo ya S8PL.

Kikosi hicho kinajumuisha: Peter Ngacha, Erick Kyalo (nahodha), Jack Otieno, David Bosire, Rahim Malik, Steven Orimba, Shaban Ndege, Stephen Oduor, Idriss Gerrardo, Ronald Ouma, Goddy Ayemba, Shillingi Abdullah, Alvin Munubi, Henry Oluchiri, Ronnie Otieno, Felix Odhiambo na Isma Omar. Maofisa wake:Erick Ochieng (mwenyekiti), Jeri Mpapa (katibu) na Derick Benja (mweka hazina).

Kinyang’anyiro hicho kilishiriki timu 16 zingine zikiwa: Kisa Allstars, Genesis FC, Rithimitu, Macmillan, R.O.G, RYSA, SC WYSA, Parkroad na Yamabeshte.

Kwenye kampeni za S8PL msimu ujao, Shaurimoyo itapigania ubingwa dhidi ya wapinzani wengine ikiwamo Jericho Allstars, Meltah Kabiria, Mathare Flames, Githurai Allstars, TUK na MASA kati ya zingine.

You can share this post!

Mpango wa Meltah Kabiria kutetea taji msimu ujao

SHINA LA UHAI: HPV, virusi vinavyoendelea kuwa adui wa...

adminleo