Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana ya mtindo, sajili na masharti ya matumizi ya lugha katika Kiswahili

December 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MARY WANGARI

KULINGANA na mtazamo huu, dhana ya mtindo inafafanuliwa kama utunzi wa fasihi ya hali ya juu kabisa.

Ufafanuzi au maelezo haya hata hivyo yanatatiza kimaana kwa kuwa hayazingatii kikamilifu mahusiko ya dhana ya mtindo wenyewe.

Yamkini mtazamo huu unalenga ama umbuji au ubunifu wa kurejelea mbinu za kujieleza kama vile matumizi ya tamathali za semi. Hata hivyo, jinsi tunavyofahamu, mtindo ni zaidi ya mbinu hizi.

Mtindo haurejelei tu jinsi waandishi wanavyoandika bali pia njia mbalimbali zinazotumiwa na watu ama kuongea au kuandika katika hali za kawaida za kila siku. Mtindo hivyo basi ni jumla ya namna lugha inavyotumiwa na wanajamii.

Sajili/Rejista – Kwa mujibu wa Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (1990), dhana ya sajili au rejista ni lugha inayotumika katika muktadha maalum. Sajili hutumika katika kupambanua lugha inayofaa katika miktadha mbalimbali katika jamii.

Vigezo mbalimbali vinavyotumika kutofautisha sajili moja na nyingine ni kama vile: msamiati, miundo ya lugha, uundaji wa sentensi, kupanda na kushuka kwa sauti, mnyambuliko wa vitenzi na kadhalika.

Sajili ni sehemu ya umilisi wa mawasiliano ambao kila mzungumzaji huwa nao. Umilisi huu humwezesha mwanajamii au mzungumzaji wa lugha fulani kubadili matumizi ya lugha, kuteua vipengele fulani vya matamshi, msamiati na mambo mengineyo katika miktadha anuai. Halliday (1964) anahoji kwamba, sajili hutofautiana kutokana na vipengele vikuu vitatu ambavyo ni pamoja na: mada inayozungumziwa, uhusiano kati ya watu wanaowasiliana kwa mfano ni mazungumzo kati ya mzazi na mtoto, kati ya marafiki au mzee na kijana. Na tatu, njia ya mazungumzo inayotumika, je ni andishi, zungumzi au ishara?

Chimbuko la Sajili – Sajili huenda ziliibuka kutokana na mikatale ya kijamii. Wanajamii huwa na miiko mbalimbali inayohusu jinsi lugha inavyofaa kutumiwa. Kwa mfano haifai kutumia lugha inayotumika harusini katika hafla ya mazishi. Kwa mantiki hii, ni bayana kwamba lugha huwa imegawika katika sajili mbalimbali kutokana na Imani za watu na pia kukidhi mahitaji ya muktadha.

Aidha, chimbuko lingine la sajili huenda lilitokana na hali ya kugawanyika kwa jamii katika makundi mbalimbali ya kazi ili kujikimu. Kila kundi kisha hubuni msamiati mahsusi unaoelezea hali, mazingira pamoja na zana za kazi. Ni kutokana na upekee huu wa wazungumzaji ambapo sajili anuai zilizuka.

Hali hii pia inaweza kunasibishwa na ukuaji wa binadamu kimaendeleo. Kadri ya jinsi binadamu alivyozidi kukua na kuendelea kijamii, kisiasa na kiuchumi ndivyo jinsi kazi mbalimbali zilivyojitokeza na hivyo kukawa na lugha maalum ya kuelezea hali hizo. Kwa mfano, maendeleo katika nyanja ya sayansi na teknolojia yamesababisha kuzuka kwa sajili ya kisayansi na kiteknolojia ikiwemo kubuniwa kwa istilahi maalum zinazotumika katika nyanja hiyo.

Dhana ya masharti ya matumizi ya lugha

Wanaisimu Crystal na Davy (1969) na Kitsao (1988), wameshughulika kwa kina kuhusu dhana ya masharti ya matumizi ya lugha. Dhana hii inaweza kufafanuliwa kama mambo yanayomwongoza mzungumzaji au mwandishi katika kuteua sajili inayofaa katika mawasiliano yake.

Crystal na Davy (ibid) wameyaita mambo haya kama mawanda ya matumizi kimuktadha ambapo wameyaainisha katika vipengele vinane ambavyo ni: ubinafsi, lahaja, wakati, kazi, hadhi, namna ya kuwasilisha, upekee na aina ya mazungumzo.

Msomi Kitsao kwa upande wake ameyaainisha masharti ya mazungumzo katika vitengo tisa ambavyo ni pamoja na: mazingira, uhusiano, cheo, hali, madhumuni, kichwa cha mazungumzo, lugha azijuazo mtu, tabaka na malezi na umri.

Kwa kuangazia mtazamo wa Kitsao (ibid) tunaweza kufafanua vipengele hivyo vya masharti kwa jinsi ifuatavyo:

Mazigira – Kwa mfano mtu anapokuwa afisini anatakiwa kutumia lugha rasmi lakini anapotangamana na marafiki zake anaruhusiwa kutumia lugha isiyo rasmi, inayosheheni utani, ucheshi na kadhalika, Vilevile, kuambatana na mazingira kwa mfano katika ibada ya mazishi, lugha inayotakiwa kutumika ni ile inayoashiria huzuni, kuwapa pole pamoja na kuwafariji waliofiwa.

Uhusiano – Mahusiano yaliyopo baina ya wanajamii husababisha lugha kutumiwa lwa mtindo fulani unaostahili. Kwa mfano, lugha kati ya mzazi na mtoto inapaswa kuwa ya heshima na unyenyekevu. Katika jamii ya Kiafrika, si kawaida kwa wazazi na watoto kutaniana ama mtoto kuwaita wazazi wake kwa majina yao kwa mfano.

 

[email protected]