• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MAN-CITY KINANUKA: City kupelekea Burnley hasira

MAN-CITY KINANUKA: City kupelekea Burnley hasira

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

MANCHESTER City watakuwa leo Jumanne wageni wa Burnley katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani Turf Moor.

Crystal Palace watakuwa wenyeji wa Bournemouth ugani Selhurst Park katika mchuano mwingine.

Kufikia sasa, Man-City wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 29, tatu zaidi kuliko Chelsea wanaofunga mduara wa nne-bora.

Kwa upande wao, Burnley na Palace wanajivunia alama 18 kila mmoja, huku pengo la pointi mbili pekee likitamalaki kati yao na Bournemouth wanaoshikilia nafasi ya 12 kwa alama sawa na West Ham United na Newcastle United.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City watashuka dimbani wakipania kujinyanyua baada ya kujikwaa dhidi ya Newcastle United wikendi iliyopita. Wakipepetana na Newcastle uwanjani St James’ Park, vijana wa Guardiola walilazimishiwa sare ya 2-2; matokeo ambayo yaliwasaidia viongozi Liverpool kufungua mwanya wa alama 11 kati yao na mabingwa hao watetezi wa taji la EPL.

Kichapo au sare nyingine kwa Man-City huenda kikazamisha kabisa chombo chao cha matumaini ya kutia kapuni ubingwa wa EPL muhula huu.

Kulingana na Guardiola, kubwa zaidi katika maazimio yao kwa sasa ni kusajili ushindi katika takriban kila mchuano kwa matarajio kwamba Liverpool nao watateleza.

Ingawa pengo la pointi 11 ni kubwa kwa Man-City kuziba, ni jambo ambalo kocha Guardiola amesisitiza kwamba linawezekana. Mnamo Disemba mwaka jana, kusuasua kwa Liverpool kileleni mwa jedwali la EPL kuliwachochea Man-City kutoka nyuma kwa alama saba na kuwapokonya taji la EPL mdomoni.

Ingawa hivyo, dalili zote zinaashiria kuwa haitakuwa rahisi kwa Liverpool ya kocha Jurgen Klopp kupoteza alama zozote hivi karibuni hasa ikizingatiwa kuwa wamesajili sare moja pekee kutokana na jumla ya michuano 14 iliyopita.

Hata hivyo, huenda pigo la kuzikosa huduma za Fabinho anayeuguza jeraha na kipa Alisson Becker anayetumikia marufuku kukatikisa uthabiti wa Liverpool katika michuano kadhaa ijayo.

Guardiola amesisitiza kuwa msimu huu tatizo ni kushindwa kwa waajiri wake kujaza pengo la aliyekuwa nahodha Vincent Kompany ambaye alibanduka uwanjani Etihad msimu jana.

Wakisubiriwa na ratiba ngumu zaidi mbele yao, itawajuzu Man-City kusajili ushindi katika mechi ya leo ili wapate hamasa itakayowatambisha katika mchi nane zijazo.

Baada ya kuvaana na Burnley, Man-City watachuana na Man-United ugani Etihad kabla ya kuwaendea Dinamo Zagreb na Arsenal ugenini. Watawaalika Leicester City kabla ya Sikukuu ya Krismasi kisha kuvaana na Wolves na Sheffield United kwa usanjari huo.

Chini ya kocha Sean Dyche, Burnley watakuwa na kibarua kigumu cha kujinyanyua leo kutokana na kichapo cha 2-0 walichopokezwa na Crystal Palace wikendi iliyopita. Baada ya kuwaalika Man-City, Burnley watakaopania kutegemea sana Ashley Barnes na Chris Wood, watachuana na Tottenham Hotspur ya kocha Jose Mourinho wikendi hii.

Man-City watakosa huduma za Sergio Aguero, Leroy Sane, Aymeric Laporte na Oleksandr Zinchenko. Guardiola huenda akawadumisha Nicolas Otamendi, John Stones, Rodri, Bernardo Silva na Joao Cancelo katika kikosi chake cha kwanza kitakachokamilishwa na Raheem Sterling, Kevin de Bruyne na Gabriel Jesus. Kwa upande wao, Burnley ambao wamepigwa jeki na marejeo ya Johann Berg Gudmundsson, Ashley Westwood na Matej Vydra, watayakosa maarifa ya Charlie Taylor ambaye nafasi yake huenda ikatwaliwa ama na Robbie Brady au Jeff Hendrick.

Katika jumla ya mechi 22 ambazo zimewahi kukutanisha vikosi hivi awali, Man-City wamepoteza mchuano mmoja pekee huku wakisajili ushindi mara saba.

You can share this post!

Onyo kali kwa wanaotumia watoto kuuza chang’aa

Lalama kuhusu mazingira mabovu ya usahihishaji KCSE

adminleo