• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
MAKALA MAALUM: Anavuna hela kwa maombi na ‘miujiza’

MAKALA MAALUM: Anavuna hela kwa maombi na ‘miujiza’

Na LILLYS NJERU

JE, unaweza kujitolea vipi kumpa Mwenyezi Mungu dhabihu?

Itakuwaje ukiambiwa sadaka yenyewe ndiyo gharama tosha kuombewa na mhubiri au ‘mtumishi’ wa Mungu?

Ninapoelekea katika jumba kuu la Kahawa, lililo katika barabara ya Haile Selassie jijini Nairobi, ninapatana na wachuuzi wakiwashawishi wapita njia kwa kila mbinu wanunue bidhaa zao.

Hata hivyo, wengi wa wapita njia wako katika harakati ya kuhakikisha kuwa hawatachelewa kwa ibada ya kanisa la Jesus Teaching Ministries linalotambuliwa zaidi na wengi kama JTM, lililopo katika jumba hilo.

Nyimbo za injili zinasikika kwa umbali ninapojongelea kanisa hilo, katika lango lake, nakaribishwa na kikundi cha watu watano waliovalia jaketi angavu zenye maandishi yaliyoandikwa kwa kimombo ‘Guest Relations Officer’.

Baada ya kukaguliwa, tunaashiriwa na mmoja wa wasaidizi hao kuwa wanaotembelea kanisa hilo kwa mara ya kwanza wanapaswa kumfuata.

Utaratibu wa kanisa

Baadhi yetu tunatii amri na kumfuata kijana huyo ambaye anatuelekeza katika chumba cha wageni ambapo tunapatana na kikundi kingine cha watu 15 waliovalia fulana zenye maandishi, ‘Guidance and Counselling’, yenye maana kuwa, kazi yao maalum kama washirika wa kanisa hilo, ni kupeana ushauri.

Binti mmoja anajitambulisha na kunieleza kuhusu vitu ambavyo anavitambua kuwa ‘vifaa vya kubashiri’, kulingana na mshirika huyu, vifaa hivi vitanisaidia kuepuka mitego ya ibilisi.

Ananipatia kalamu ya wino na penseli ambazo ananiuzia kwa Sh50 kila moja, ananieleza kuwa pia nitahitaji kibandiko chenye maandishi; ‘JTM Ministries’ ambacho napaswa kukibandika kwa kitanda ili kinisaidie kuwafukuza pepo wachafu.

Kibandiko chenyewe ni cha Sh100 pamoja na ‘mafuta matakatifu’ ambayo ananiuzia kwa bei hio hiyo.

Hata hivyo, binti huyo ananieleza pia kuwa yapo mafuta takatifu spesheli ambayo nahitajika kujipaka mara mbili kila siku na kufunga kwa siku saba, ananiuzia kichupa kimoja kwa Sh 1,000.

Tunapozidi kuongea, mshirika huyo ananieleza kuwa vitu hivyo vya kujikinga dhidi ya minyororo ya ibilisi havitoshi kuondoa visirani vyote na hivyo bado nitahitajika kulipa Sh1,000 kama ‘mbegu’ ya kujitolea kwangu kikamilifu.

Kulingana na binti huyo pesa hizo zitatumika kulipia huduma ya maazimio na dhamira yangu maishani na nilihitajika kuongeza Sh500 pamoja na kujitolea kwa kiasi kisichopungua Sh1,000.

Baada ya kujitolea vilivyo katika matakwa hayo ya kimsingi, ananieleza kuwa nitaweza kupokea maombi ya uponyaji na wokovu ambayo yatanigharimu Sh3,000.

“Ikiwa unataka kumwona mtumishi mwenyewe unapaswa kulipa Sh5,000 ili upewe miadi ya kumwona,” binti huyo ananieleza na kunipa bahasha tatu ambazo napaswa kuweka sadaka hiyo kulingana maelezo yote niliyopokea.

Baadaye ananielekeza kwa mwanamke mwingine ambaye anataka nimpokezekitambulisho changu na kutaka kujua zaidi kuhusu historia na maisha yangu.

Mshirika huyo ananiuliza kama nina shida za kifamilila ambazo zinapaswa kuombewa na baada ya hapo ananipokeza fomu ambayo nafaa kutia saini kuonyesha idhini yangu kwa kanisa kutangaza ushahidi wangu nitakapopokea usaidizi kulingana na matatizo yangu niliyoeleza.

Ninapolitazama kanisa lenyewe nagundua kuwa ni jumba la ghorofa nne na zenye nafasi za takriban watu 300, kila ukumbi ukiwa na zaidi ya televisheni 10.

Kanisa lenyewe linatambulika sana kwa sababu ya Mtumishi Pasta Manyuru ambaye ndiye pia anamiliki chuo cha Aviation na kituo cha televisheni cha Aviation, ambacho hutangaza ibada zake.

Mtumishi wa Mungu ambaye amejivalia suti nyeupe, yupo kwenye mimbari akiwahubiria waumini wake ambao wanashangilia kila mara anapopaza sauti.

Baada ya mahubiri mtumishi huyo anaanza kuomba, pindi tu anaponyosha mikono yake na kuanza kuomba waumini wanaanza kuanguka moja baada ya mwingine.

Jirani aliyeketi kando yangu Bi Wambui Nduta*(si jina lake kamili) ananieleza kuwa tangu alipojiunga na kanisa hilo mnamo 2017 maombi ya mwinjilisti huyu yamemsaidia kupata mafanikio maishani.

Ananieleza kuwa hapo mbeleni angehisi kizunguzungu akiwa kazini, jambo ambalo lilimfanya kushuku kuwa kuna watu ambao hawakufurahia ufanisi wake.

Alilipa Sh 20,000 kuombewa na mtumishi huyu baada ya kununua vitu vilivyoelezewa kuwa muhimu katika harakati hizo za kujitafutia “kinga” dhidi ya visirani vya aina yoyote.

Ninapomuuliza kama ni lazima nitoe pesa nilizoitishwa ingawa sina kazi, ananieleza kuwa napaswa kujitolea na kutoa kama nilivyoitishwa kwani Bibilia imetaja hivyo pia.

“Huwezi kutoa sadaka ya Sh100 ilhali adui wako ametumia Sh100,000 kukufunga ili usinufaike maishani,” alinieleza.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Tuliachana kwa uzembe wake lakini bado...

Kaunti ya Lamu yatangaza kuchelewa kwa mishahara ya Novemba...

adminleo