Habari

Kaunti ya Lamu yatangaza kuchelewa kwa mishahara ya Novemba kwa wafanyakazi wake

December 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na KALUME KAZUNGU

JUMLA ya wafanyakazi 1,010 wa serikali ya Kaunti ya Lamu hawajapokea mishahara yao ya Novemba 2019.

Hii ni kufuatia utata uliopo kwenye serikali ya kitaifa wa kumteua Msimamizi wa Bajeti (CoB).

Kwenye barua rasmi iliyoandikiwa wafanyakazi hao na ambayo Taifa Leo imeona, Katibu wa Serikali ya Kaunti ya Lamu, John Mburu, ameweka wazi kwamba Kaunti bado haijapokea idhinisho la malipo ya mishahara ya wafanyakazi wake kutoka kwa ofisi ya CoB, hali ambayo aliitaja kuchelewesha mgao wa fedha zinazotolewa kwa kaunti kutoka kwa serikali ya kitaifa.

Bw Mburu aliwataka wafanyikazi wote wa serikali ya Kaunti ya Lamu kuwa watulivu wakati ambapo suala hilo linashughulikiwa.

Alisema Lamu ni miongoni mwa kaunti chache za hapa nchini ambazo zimekuwa zikijitahidi kulipa mishahara ya wafanyikazi wake kufikia tarehe 30 ya kila mwezi.

“Licha ya changamoto za mara kwa mara za kifedha hasa kutoka kwa serikali ya kitaifa, kaunti yetu imejitahidi kuhakikisha kila mfanyakazi wa hapa analipwa mshahara wake kufikia tarehe 30 ya kila mwezi kwa miezi yenye siku 30 au 31. Hii ndiyo sababu hatujashuhudia mgomo wowote wa wafanyakazi hapa kwetu kinyume na inavyoshuhudiwa kaunti zingine. Kucheleweshwa kwa mishahara ya Novemba kunatokana na tatizo lililoko kwenye ofisi ya CoB ambalo limeathiri karibu kaunti zote nchini na wala sio Lamu pekee. Ninawasihi wafanyakazi wetu kuwa watulivu wakati tatizo hilo likishughulikiwa na kutatuliwa,” akasema Bw Mburu.