HOFU CHELSEA: Vijana wa Frank Lampard wana kibarua dhidi ya Aston Villa
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
FRANK Lampard ataongoza kikosi chake cha Chelsea dhidi ya Aston Villa akikumbuka vichapo viwili mfululizo vya majuzi.
Tangu atue ugani Stamford Bridge, Lampard amekuwa na rekodi nzuri kama kocha, kabla ya kushindwa 2-1 na 1-0 na Manchester City na West Ham United.
Kufikia sasa, Chelsea wamo katika nafasi ya nne jedwalini, lakini Lampard ana wasiwasi kuhusu Tottenham Hotspur ambao wanawafuata kwa karibu.
Chini ya kocha Dean Smith, Villa wataingia uwanjani siku chache tu baada ya kutoka sare 2-2 na Manchester United, Jumapili.
Matokeo hayo ya kujivunia yamewapa vijana hao imani ya kuandikisha matokeo mengine mazuri dhidi ya timu kubwa.
Baada ya Olivier Giroud kushindwa kuvuma dhidi ya Aston Villa, huenda Lampard akaamua kuanza na Tammy Abraham ambaye amepata nafuu baada ya kuumia walipocheza na Valencia katika pambano la UEFA lililomalizika kwa 2-2.
Wakati huo huo, beki Antonio Rudiger na Ross Barkley wako katika hali nzuri ya kurejea, lakini Ruben Loftus-Cheek anaendelea kuuguza jeraha tangu aumie wakicheza na New England Revolution FC kwenye mechi ya kirafiki mwishoni mwa msimu uliopita.
Kwa upande mwingine kocha Smith atamkaribisha Anwar El Ghazi aliyekuwa akisumbuliwa na jeraha la goti, lakini Keinan Davis na Jed Steer hawatakuwa kikosini.
Jose Peleteiro anatarajiwa kuanza, lakini Frederic Guilbert anaendelea kukaa nje kutokana na adhabu ya marufuku.
Wanaotarajiwa kuwakilisha Chelsea ni: Kepa, James, Zouma, Christensen, Azpilicueta, Jorginho, Kante, Kovacic, Hudson-Odoi, Abraham na Pulisic.
Villa itakuwa na Heaton, El Mohamady, Konsa, Mings, Targett, McGinn, Luiz, Hourihane, El Ghazi, Wesley na Grealish.
Chelsea imekuwa ikisumbuliwa na majeraha kwa wachezaji wake muhimu tangu msimu uanza, lakini Lampard amekuwa akitumia nafasi zao kujaribu makinda ambao wameonyesha kiwango cha juu.
Mbali na N’Golo Kante ambaye amekuwa akikosa mechi kadhaa muhimu kutokana na jeraha, Rudiger hajacheza tangu Septemba dhidi ya Wolves alipoumia mara tu baada ya kurejea, baada ya Reece James na Callum Hudson-Odoi kutoonekana uwanjani kwa mwezi mzima.
Kwingineko, Liverpool watakuwa nyumbani kuikaribisha Everton katika mechi inayotarajiwa kuzua upinzani mkali.
Vijana hao wa kocha Jurgen Klopp ambao hawajapoteza mechi yoyote wanaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa pointi 40 baada ya kujibwaga uwanjani mara 14.
Mechi za leo kwa ufupi ni: Chelsea na Aston Villa, Leicester City na Watford, Southampton na Norwich City, Wolves na West Ham United, Manchester United na Tottenham Hotspur, kisha Liverpool na Everton.