• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
RIZIKI: Kilimo kinamsaidia pakubwa

RIZIKI: Kilimo kinamsaidia pakubwa

Na SAMMY WAWERU

KWA zaidi ya miaka minane ambayo alikuwa kwenye ndoa maisha yalikuwa shubiri kwa sababu anazodai ni “dhuluma nilizopitia.”

Kipindi hicho, Bi Sarah Magiri anasema siku alizotabasamu ni chache mno.

Licha ya masaibu aliyopitia, alijipata kujaza pengo kukimu mahitaji ya familia yake.

“Dhuluma za ndoa zikitajwa ninafahamu bayana athari zake. Wakati mwingine tungelala njaa,” asimulia Bi Sarah.

Mambo yalitokota kwa anachosema mumewe kuwa mateka wa pombe. Sarah ambaye ametoka Taita anaiambia Taifa Leo walipochumbiana na siku za kwanza kwenye ndoa, maisha yalikuwa matamu.

Yalianza kuenda segem nege miaka miwili baadaye, mume alipoanza kubugia mvinyo kiasi cha kuasi majukumu yake kama kichwa cha familia; mume na baba wa mtoto wao mmoja.

Isitoshe, aligeuka kuwa mtu wa vita, na ni hatua ambayo washauri wa masuala ya ndoa wanahimiza muathiriwa kuondoka mara moja katika uhusiano wa aina hiyo ikiwa hautaimarika.

“Mwanandoa, mume au mke akigeuka kuwa mwenye vita na juhudi za kumrekebisha zigonge mwamba, tunashauri mwathiriwa aombe talaka au atoke kwenye hiyo ndoa mara moja,” Dayan Masinde, mtaalamu na mshauri wa masuala ya ndoa ahimiza.

Ni takriban miaka kumi sasa tangu Sarah akate kauli hatakuwa mtumwa wa ndoa iliyosheheni madhila. Alipochukua hatua nyingine, alihamia jijini Nairobi na kazi iliyomkaribisha ni ya uyaya.

Alifahamu fika kuwa yeye ndiye mama na baba wa mwanawe, hivyo basi asingetaka mzaha na kazi. Kwenye mtihani wa kidato cha nne, KCSE, Sarah alikuwa amefanya vyema kwani alizoa alama C+ na alichoweka kama akiba akiwa yaya kwa muda wa miaka miwili mfululizo, alikitumia kusomea stashahada ya masuala ya kilimo.

Bi Sarah Magiri (kushoto). Picha/ Sammy Waweru

Ni kupitia jitihada zake katika taaluma hiyo, Sarah alianza kupata mialiko ya kutoa ushauri nasaha na maelezo ya kitaalamu kwa wakulima. Kazi ya kwanza aliyoangukia ni kwa mkulima mmoja kaunti ya Kiambu, ambaye ana kiunga cha matunda mbalimbali na miti.

Chema chajiuza kibaya chajitembeza, Sarah, 38, anasema akiendelea kutoa huduma hizo sifa zake zilienea miongoni mwa wakulima akapata kandarasi nyingine eneo la Athi River, kaunti ya Machakos.

“Wakulima wanaimarika kupitia mitandao, ambapo kuna makundi yanayowaunganisha pamoja na wataalamu na wateja,” aeleza.

Mtaalamu huyo kwa sasa ameajiriwa katika duka moja la uuzaji wa bidhaa za kilimo mjini Thika. Anafichua kwamba kando na ajira hiyo, anaendelea kupata mialiko ya kutoa mashauri ya kitaalamu.

“Wateja wangu wengi wanatoka eneo la Kati,” asema Sarah, pia akijumuisha Nairobi, Machakos, Kitui, na Makueni.

Eneo la Kati linafahamika kuimarika katika sekta ya kilimo, hasa ukuzaji wa mboga za aina mbalimbali na matunda. Kaunti za Kati na ambazo ni tajika katika shughuli za kilimo ni Nyandarua, Kiambu, Murang’a, Kirinyaga na Nyeri. Zingine ni Embu, Meru na Laikipia.

Eneo la Kati pia huzalisha majanichai na kahawa. Bi Sarah hata hivyo anasema nasaha na ushauri anaotoa unaegemea mimea na mazao yanayochukua kati ya mwezi mmoja na miezi mitatu kuanza kuvunwa.

Wakati wa mahojiano alisema amepata nafasi kaunti ya Nairobi kuunda kivungulio (greenhouse) ili aingilie kilimo kwenye mahema.

“Ni rahisi kukuza nyanya, pilipili mboga na hata mboga kwenye hema,” akasema.

Aghalabu, mkulima akiwa na kadri ya mtaji wa Sh70,000 anaweza kuingilia kilimo cha hema. Kinasifiwa kudhibiti usambaaji wa wadudu na magonjwa kwani huwa kimeezekwa.

Gharama ya dawa dhidi ya wadudu na magonjwa inaendelea kuwa ghali, suala linalolemaza juhudi za wakulima wengi nchini.

  • Tags

You can share this post!

Mkubali masharti au muondoke, Magufuli aambia Wachina

KCB inavyojiandaa kwa kipute cha voliboli

adminleo