Makala

AKILIMALI: Kilimo cha nyanya ni dhahabu kwake

December 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMUEL BAYA

KILA ukulima unapochukuliwa na kuendelezwa kwa njia njema, basi unaweza kumpa mwenye kuuendeleza fursa nzuri ya kimaisha.

Kilimo bora ndiyo uti wa mgongo wa taifa hili na kila mwanya unapotokea kuendeleza sekta hiyo, kila mmoja hana budi kujikaza na kustawisha ajenda hiyo.

Hiyo ndiyo iliyokuwa taswira kamili ya Bw David Kimari mwenye umri wa miaka 41 ambaye baada ya kukumbatia kilimo cha nyanya na mahindi katika eneo la Subukia, kaunti ya Nakuru maisha kwake yamekuwa mazuri.

Matokeo ya juhudi zake za kurauka kila asubuhi na kuondoka jioni katika kipande cha ardhi cha ekari moja na robo yameanza kuonekana kwani anafurahia kazi ya mikono yake.

Nimekuwa mkulima katika eneo hili la Solai nikikuza nyanya na mahindi. Ni ukulima ambao una changamoto nyingi lakini wakati wa kuuza mazao, bila shaka huambatana na faida kubwa akasema.

Aliambia Akilimali kwamba amekuwa akikuza nyanya kwa zaidi ya miaka 20 katika eneo hili na kilimo hiki ndicho ambacho kimemsaidia kupambana na changamoto mbalimbali za maisha.

Amefundisha watoto wake hadi sekondari na wengine wanaendelea kusoma kwa sababu ya ukulima; kwa ufupi, hajutii kuwa katika sekta hii.

Alisema kuwa kwa sasa sanduku la nyanya sokoni linauzwa kwa Sh3,000 lakini akaongeza kwamba bei ya mbolea na vifaa vyingine vya ukulima ni ghali.

Nilianza kulima hapa mwezi wa Agosti baada ya kukodisha na kuanza kutayarisha shamba. Kwa sasa hivi nimevuna mara mbili. Katika awamu ya kwanza, nilivuna masanduku saba na kujipatia Sh21,000. Lakini sasa ninatarajia kuuza nyanya nyingi zaidi, akaongeza.

Kwa sasa mkulima huyu ambaye ni baba wa watoto watano alisema kilimo kimemwezesha kuilisha familia yake, huku akitumaini kwamba biashara hiyo itaendelea kuimarika.

Wakati nilipoanza kuvuna nyanya hapa, nilianza na mavuno ya masanduku mawili lakini sasa kiwango cha mavuno kinaendelea kupanda.

Kinachofanyika ni kuwa kila unapoendelea kuvuna, ndipo pia unapoendelea kupata masanduku mengi zaidi. Kwa mara ya pili nilivuna nyanya masanduku saba. Kila unavyozidi kuvuna, ndivyo pia unavyozidi kupata nyanya nyingi, akasema mkulima huyu.

Aidha, mkulima huyu aliongeza kwamba anatarajia kuvuna masanduku 40 atakapovuna tena mwezi huu.

Mimi soko langu la nyanya liko mjini Nakuru lakini pia changamoto ni wakati wa kuangalia bei ya nyanya. Wakati kuna nyanya nyingi bei huwa chini ila wakati nyanya zinapoadimika basi bei yake pia huwa juu, akasema Bw Kimari.

Hata hivyo, mkulima huyu asema kuwa licha ya kilimo hiki kuwa na faida, tatizo ambalo analazimika kukabiliana nalo ni bei ya juu ya pembejeo za kilimo pamoja na mbolea na dawa za kukinga nyanya kutokana na wadudu waharibifu.

Pesa nyingi katika kilimo hiki huenda katika kununua pembejeo za ukulima pamoja na mbolea. Endapo bei ya pembejeo za ukulima itakuwa chini, hata bei ya mazao ikiwa chini sokoni, tutaweza kupata faida kubwa. Lakini ikiwa mbolea na dawa itakuwa juu, itakuwa vigumu sana kwa mtu kunawiri katika sekta hii, akasema mkulima huyo.

Katika kipande hicho cha ardhi ambapo anakuza nyanya, mkulima huyo alisema kuwa kila wakati wa kupiga dawa, hutumia kiasi cha Sh10,000.

Katika huu ukulima, kuna vitu vingi ambavyo utatumia kuhakikisha kwamba nyanya zimekuwa vizuri. Dawa na mbolea zinatuumiza sana katika kilimo hiki na kuna ulazima wa kuzitumia.

Vile vile huwa tunaweka vijiti vya kusimamisha mmea huu, kamba za kufungia nyanya, na mifereji ya kuvuta maji kutoka kwa bwawa lililoko karibu. Hizi zote ni gharama ambazo kama mkulima lazima upitie, akasema Bw Kimari.

Alisema kuwa licha ya changamoto hizo biashara hii imekuwa ya baraka kubwa kwake na anashukuru kwa sababu inampa mapato mazuri.

Ninashukuru kwamba biashara hii imenisaidia kimaisha na siwezi kulalamika.

Wakati mwingine Mungu anakubariki na unapofika sokoni, unakuta bei iko juu na unauza vizuri.

Mara nyingine unaweza kuuza nyanya kwa Sh5,000 kwa kila kreti, akasema Bw Kimari.

Mwaka wa 2005, aliuza kreti 100 kwa bei ya Sh5,000 na kujiwekea pato zuri.

Nimekuwa nikiuza nyanya hapa na wakati huo, nakumbuka nilikuwa na biashara nzuri sana. Mapato niliyopata yaliniwezesha kuendeleza familia yangu. Nimejenga nyumba na kununua ardhi katika maeneo mbalimbali kupitia kwa biashara hii, akasema.

Anawataka Wakenya wajitahidi kila mahali walipo, watie bidii hasa katika kilimo kwa sababu ni uti wa mgongo wa biashara na maisha.

“Mimi kila nikiraukia katika shamba hili, ninajua kabisa kwamba baada ya muda fulani, nitapata faida. Haya ndiyo matarajio ambayo kila Mkenya anafaa kuwa nayo,” asema Bw Kimaru.