• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
UFUGAJI: Ng’ombe wa maziwa sasa ndiyo ajira yake

UFUGAJI: Ng’ombe wa maziwa sasa ndiyo ajira yake

Na RICHARD MAOSI

KATIKA jamii nyingi zinazoendesha kilimo biashara, aina ya kilimo kwa mujibu wa utafiti ni ufugaji wa ng’ombe kwa ajili ya maziwa na nyama, ndio maana utunzaji wa ndama ndio hatua ya kwanza katika upatikanaji wa mifugo wengi siku za usoni.

“Lengo la kila mkulima ni kujiajiri na ajizatiti kuhakikisha kuwa anayapata maziwa mengi wakati wowote ule bila kukatika ili ajiinue kiuchumi na kujiongezea ujuzi kulingana na mahitaji ya wanunuzi” huu ndiyo ushauri wa Julius Kipkosgei Arusei mfugaji wa ng’ombe aina ya Freshian kutoka eneo la Biribiriet Kaunti ya Nandi.

Anasema alianzisha mradi wenyewe yapata miaka 15 iliyopita na ng’ombe wanne tu, akiwa na kusudi la kujitengenezea ajira badala ya kutegemea kazi za kuajiriwa.

Alieleza Akilimali kuwa hajawahi kununua maziwa, bali ndiye msambazaji wa maziwa katika kaunti ya Uasin Gishu na Nandi, akitumika kama kielelezo cha mkulima anayejipatia hela nzuri kutokana na mifugo.

“Unaweza kuyakama maziwa pia ukayaongezea thamani kwa kutengeneza bidhaa kama vile maziwa gururu yaani yoghurt na cheese,” Arusei asema.

Anaeleza kuwa ng’ombe wa maziwa ni biashara kama biashara nyingine ile, mradi mfugaji aelewe mahitaji ya kumtunza, kumkinga dhidi ya mkurupuko wa maradhi na mazingira mwafaka ya ufugaji, ikizingatiwa kuwa kaunti ya Nandi inapatikana katika nyanda za juu kwenye Bonde la Ufa.

Ngombe wa Freshian ni wenye asili ya kigeni na wana sifa ya kutoa maziwa mengi yenye protini, wana mabaka ya rangi nyeupe na nyeusi huwa wakubwa kwa umbo na wenye kilo baina ya 500-600.

Wanahitaji angalau kilo 110 ya chakula kila siku na lita 60 za maji kila siku, pia wana uwezo wa kuzalisha lita 40 -50 za maziwa kila siku maziwa yenye kiwango kidogo cha mafuta,Lakini kulingana na Arusei anasema ng’ombe wake hutoa baina ya lita 20-30 ya maziwa kila mmoja.

Nyasi aina ya napier grass pamoja na viazi vitamu vilivyosagwa ni miongoni mwa viungo muhimu vinavyoweza kuongezea maziwa ya mkulima ubora hasa baada ya ng’ombe jike kuzaa.

Anawakumbusha wakulima kuwapa mifugo wao virutubisho tajiri vya wanga (carbohydrates) kama vile mabaki ya mimea inayotoa mafuta kwa mfano mbegu za pamba na mabuwa ya mahindi yaliyosagwa na kuchanganywa vyema.

“Ikumbukwe kuwa wakati wa utoaji wa maziwa ng’ombe hupoteza kiwango kikubwa cha calcium, kwa hivyo ni jambo la busara endapo madini haya yatapakikana ndani ya lishe,” akasema.

Aliongeza kuwa kwa sababu nchi ya Kenya inapatikana katika eneo la joto jingi hivyo basi pana haja ya kukabiliana na kupe ambao bado ni changamoto kwa afya ya mifugo wengi na wamekuwa wakisababisha maradhi ya East Coast Fever.

Mfanyakazi Arap Too katika boma la mkulima Julius Arusei anasema ng’ombe wa freshian wanaweza kutoa baina ya lita 40-50 ya maziwa kila siku. Picha/ Richard Maosi

Wakati wa kukamua yeye hutumia vyombo safi na pia husafisha chuchu vizuri ili kuangamiza vimelea vya bakteria ambao wanaweza kusambaza maradhi kama vile milk fever na homa ya maziwa.

“Inafaa ng’ombe awe akipewa chakula chake katika sehemu ambayo ni sawa na ile ya kukamiwa ili apate fursa ya kutulia katika mawazo yake kwa kuyazoea mazingira yake. Aidha hali hii itasaidia kutengeneza urafiki na mkulima,” aliongezea.

Arusei hulazimika kuvuna na kuhifadhi mazao ya ziada katika ghala, ili kuwafaa mifugo wako msimu wa kiangazi, wakati ambapo upatikanaji wa malisho sio rahisi, akiamini kuwa malisho yaliyokauka vizuri ni bora kuliko nyasi za kawaida.

Mara nyingi akilazimika kuchanganya madini yanayohitajika katika mwili wa ngombe, kwa kutumia lishe mbalimbali kama vile hay na mollaseses angalau mara mbili kila siku na kuambatanisha nyasi za kawaida.

Anasema ni lazima mkulima ajizatiti kuchunguza kuwa mifugo yake haijachanganywa na kuunda kizazi chotara ambao huwa na kiwango kidogo sana cha maziwa.Ngombe chotara huwa na kinga kidogo ijapo katika swala la kukabiliana na maradhi.

“Hali itakayowaokoa wakulima wengi sasa ni uvumbuzi wa kiteknolojia utakaokuja na mbinu za kupata mifugo wanaokula kiwango kidogo cha lishe,” anashauri.

Pia anawaomba wakulima kutengeneza vyama vya ushirika ili kuunda soko la pamoja kwa bidhaa zinazotokana na mifugo hususan maziwa ambayo bei yake si imara.

You can share this post!

AKILIMALI: Kilimo cha nyanya ni dhahabu kwake

Bwawa Uhuru latapika maji na kuathiri baadhi ya wakazi wa...

adminleo